Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuna Wanyama mmoja tu, hakuna mwingine

WANYAMA Pict


WIKI ile nyingine iliyopita, Victor Wanyama Mugubi alitangaza kustaafu soka la kulipwa. Nimekumbuka mengi kuhusu Wanyama. Kijana kutoka Muthurwa pale Nairobi aliyekwenda duniani kutimiza ndoto zake. Na kweli alizitimiza.


Tanzania ina Mbwana Samatta pekee, Kenya ina watu watatu. Dennis Oliech, McDonald Mariga na Victor Wanyama Mugubi. Kama kuna mwingine unaweza kumwongeza ni Michael Olunga. Victor alifika mbali zaidi.

PAZI 01

Katika wote hao, Wanyama anabakia kuwa Mkenya wa kwanza kucheza Ligi Kuu England. Na hakucheza kama mchezaji wa kawaida, alicheza kama staa akitokea Celtic ya Scotland kwenda Southampton ambako aliuwasha moto kabla ya kwenda Tottenham Hotspurs.

Wanyama, mpole kama alivyo, nilikutana naye Nairobi wakati huo akiwa mchezaji wa Southampton. Nilikwenda kufanya naye mahojiano nikiwa mwandishi wa gazeti la Mwanaspoti na alinipokea vema.

Sikushangaa kwa nini alinipokea vema kwa sababu mwaka 2013 nilisafiri kwenda Parma Italia kufanya mahojiano na kaka yake, McDonald Mariga na alishanitambulisha kwa Wanyama. Wote wawili ni watu wazuri. Wana utu.

Kuna watu wamekuwa wakiendelea kujiuliza kama Wanyama na Mariga ni ndugu kwa sababu majina yao ya mbele ni tofauti. Ndiyo, ni ndugu. Baba mmoja, mama mmoja. Ni utamaduni wa Wakenya au wazungu kuwa na majina ambayo jina la mbele yanaweza kuwa tofauti. Hata hivyo, McDonald Mariga jina lake kamili ni McDonald Mariga Wanyama.

PAZI 02

Nilikutana na Wanyama katika makazi yake Nairobi akanisimulia ugumu wa kucheza Ligi Kuu England. Sio wengi wamefanikiwa na ndio maana Samatta anabakia kuwa Mtanzania wa kwanza na wa mwisho hadi sasa kucheza ligi hiyo.

Ndiyo maana hadi  sasa Wanyama anabakia kuwa Mkenya wa kwanza na wa mwisho kucheza ligi hiyo. Wakati nafanya mahojiano na Wanyama alikuwa ni staa wa Southampton. Na baadae alikwenda Tottenham Hotspurs ambayo ilikuwa ya moto.

Unaikumbuka Spurs ile? Wanyama alikuwa anasimama kwa nyuma. Mbele yake kulikuwa na Moussa Dembele, Christian Eriksen, Dele Alli, Son Heung Min na Harry Kane. Katika Tottenham ile Wanyama pia alikuwa staa. Hakuwa mchezaji wa kawaida.

PAZI 03

Wanyama mwenyewe aliniambia hata ukimuona mchezaji ni goigoi Ligi Kuu England basi fahamu sio goigoi. Hauwezi kuwa goigoi ukacheza England. Inawezekana aina ya mchezaji anacheza taratibu lakini ana nguvu kubwa miguuni mwake au mwilini mwake.

Wanyama ameacha alama mbalimbali nyuma yake. Alama ya kwanza ni unaweza kuwa mchezaji wa hali ya juu bila ya kujali wapi ulikotokea. Jambo hili limekuwa likiwaathiri wachezaji wengi kisaokolojia.

Limekuwa likiwaathiri pia mashabiki wa soka ambao vichwani wanaamini ni wachezaji wa mataifa fulani ndio wanaweza kufika katika ngazi za juu katika mpira.

Kijana kutoka Muthurwa pale Nairobi, kama ilivyo kwa kijana kutoka Mbagala kule Dar es salaa, Samatta walicheza Ligi Kuu England.

PAZI 03 (1)

Wazungu wana ule msemo wao, Against all odds. Huku uswahilini huwa tunasema ‘dhidi ya vipingamizi vyote’.

Wanyama aliweka mguu wake sehemu ambayo ungeweza kuvunjika. Akaenda zake Sweden, kisha Ubelgiji, halafu Scotland na mwishowe akaishia England akicheza Spurs kama staa. Siyo kazi rahisi.

Huku England Wanyama hakuwa na vigezo vyovyote vya kucheza kwa maana ya kanuni zao kwa sababu Kenya haikuwa miongoni mwa nchi 70 katika ubora wa soka duniani.

Hata hivyo Southampton walilazimika kumwombea kibali maalumu kama ambavyo Aston Villa walifanya kwa Samatta.

Baada ya kutamba England chini ya Kocha Mauricio Pochettino ambaye ndiye pia alikuwa kocha wake, Southampton na kisha akamchukua Spurs, Wanyama alitimkia zake Canada Kwenda kumalizia maisha yake ya soka.

Kwa kucheza England, tena katika kiwango cha juu, Wanyama anaacha kwa vijana kwamba haijalishi umetoka Kenya, Tanzania au Brazil, unaweza kucheza England. Ni suala la uwezo wako tu na kujituma kulikopitiliza.

PAZI 05

Kama unashindwa kupata mafanikio katika kiwango cha juu ni kwa sababu hauonyeshi ubora wako. Kumbe mchezaji wa Argentina na mchezaji kutoka Malawi wana nafasi sawa katika jukwaa la soka popote duniani.

Baada ya kukaa na Wanyama pale Nairobi niligundua kitu tofauti kabisa kati yake na mastaa wengi wa soka nchini ambao wanaonekana kuridhika na majina yao.

Victor alionekana mpole, mtiifu na mwenye nidhamu. Siyo tu kwangu ambaye nilikuwa mgeni wake, bali pia hata kwa dada yake wa kazi nyumbani.

Kuhusu Harambee Stars? Wanyama alijikuta samaki mkubwa katika bwawa dogo. Ni kama ilivyomtokea Samatta. Ni kama ilivyowatokea wachezaji wengi wakubwa duniani kama vile George Weah au Ryan Giggs.

Ghafla unakuwa mchezaji mkubwa katika taifa dogo kisoka. Hakuna unachoweza kufanya.

Sawa, Lionel Messi ni mchezaji mkubwa kisoka. Mmoja kati ya wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea duniani. Lakini alikuwa pia anatoka taifa moja na kina Sergio Aguero ambao ni wachezaji wakubwa. Ni kesi tofauti na kina Wanyama na Samatta.

Pamoja na kila kitu lakini Wanyama hakuwa na maringo katika kuichezea timu yake ya taifa.

Alisimama kama alama ya timu na katika utaratibu wa sasa mchezaji anayecheza kwa mafanikio zaidi nje ya taifa lake ndiye ambaye anakuwa nahodha wa timu. Wanyama alijikuta akiwa nahodha wa Harambee Stars.

Hakukuwa na maringo kutoka kwake. Wachezaji wa aina yake mara nyingi wanahofia zaidi kuumia wakiwa katika majukumu ya timu za taifa wakihofia namba zao klabuni. Wanyama hakuwa mchezaji wa aina hiyo.

Amestaafu soka na anataka kujikita katika kazi ya ukocha. Haijalishi atapata nini katika ukocha lakini katika taifa la Kenya na Afrika Mashariki na kati, Wanyama ameacha alama.

Hakuna rekodi ambayo hauwezi kuifuta kama kuwa mtu wa kwanza kufanya jambo.

Itabakia hivi hivi kwamba Victor Wanyama ni mchezaji wa kwanza kutoka Kenya kucheza ligi kuu ya England.

Hakuna unachoweza kuiba kutoka katika historia hii. Yeyote ambaye atafanikiwa tena hawezi kuvunja rekodi hii. Kuna Victor Wanyama mmoja tu. Mmoja tu.