Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ligi ya mfalme Charles ilivyojaza makapteni feki, kina Odegaard

PAZIA Pict


NYAKATI zimekwenda wapi? Sijui. Unarudisha nyakati nyuma wakati ulipokuwa unakutana na wachezaji ambao wangeweza kuweka mguu sehemu ambayo ungeweza kuvunjika. Mchezo wa wanaume ulichezwa na wanaume. Wavulana wasingeweza kucheza mchezo wa wanaume.


Katika zile vita za wanaume alikuwa anachaguliwa mwanaume zaidi asimamie wanaume vitani. Nafasi ya unahodha haikuwa lelemama sana Ligi Kuu England, lakini labda mabadiliko ya tabia nchi yameiingia hadi uwanjani.


Nilikuwa nawatafakari manahodha wa timu kadhaa hasa za wakubwa katika Ligi Kuu England. Ligi kuu ya wakoloni wetu. Ipo katika mikono ya mfalme Charles kwa sasa. Wakati ule tukitazama ligi hiyo kwa muda mrefu nchi yake ilikuwa chini ya mama yake. Malkia Elizabeth.

Pale kwangu nina Martin Odegaard. Nazungumzia Arsenal. Nahodha fundi wa mpira lakini sifa za unahodha sidhani kama anazo. Mtulivu, anajali zaidi mpira wake. Hana maneno kwa mwamuzi wala kwa wachezaji wenzake.

Ogedaard anaupenda zaidi mpira wake mguuni uongee lakini hana hamasa kwa wenzake linapokuja suala la kusaka ushindi. Yupo kama hayupo. Utamhukumu kwa ubora wake mguuni, lakini siyo kwa hamasa ya mchezo mzima.

PAZ 05

Zamani Arsenal walipita kina Tony Adams na Patrick Vieira. Watu wa shoka. Siyo tu walikuwa mafundi, lakini walikuwa wanaume haswa. Futi nyingi kwenda hewani, wapambanaji na mwisho zaidi walikuwa majemedari.

Kama ungenipa nafasi ya kuchagua nahodha wa Arsenal ningempa Declan Rice. Mapafu ya mbwa ambaye anakupa kila kitu uwanjani. Na zaidi anakupa uongozi. Mwingine ambaye ningeweza kumpa unahodha ni Gabriel Magalhaes. Mbrazil mwenye roho ngumu, kiongozi na mpira upo mguuni.

Naitazama Manchester United. Nahodha wao ni Bruno Fernandes. Asikudanganye mtu. Bruno ndiye mchezaji muhimu zaidi Manchester United kwa sasa lakini sio kiongozi muhimu uwanjani. Bruno anaongoza kwa manung’uniko uwanjani.

PAZ 04

Bruno anawanung’unikia wachezaji wenzake. Anawanung’unikia waamuzi. Hataki ufafanuzi kutoka kwa mwamuzi. Huwa ananung’unika tu muda wote. Ananikumbusha unahodha wa Cristiano Ronaldo pale katika timu ya taifa ya Ureno.

Ronaldo anatumia muda mwingi kuwalalamikia wenzake badala ya kuwaongoza njia ya kupita. Anatumia muda mwingi kumlalamikia mwamuzi badala ya kuhitaji ufafanuzi. Sina shida sana na Ronaldo kwa sababu ni nahodha wa timu ya taifa. Siku hizi mchezaji staa zaidi katika kikosi cha timu ya taifa ndiye anakuwa nahodha.

Siongelei unahodha wa timu ya taifa ambao unatupatia manahodha wasiostahili. Naongelea Ligi Kuu England ambayo zamani ilikuwa inatupa manahodha wenye roho za chuma. Mchezaji anaweza asiwe staa kikosini lakini anaweza kuwa staa zaidi.

PAZ 03

Huu unahodha wa Bruno unanikumbusha namna ambavyo nyakati zimepotea. Zamani Manchester United walikuwa na Roy Keane. Mtu chuma. Keane alikuwa mtu anayeogopwa zaidi katika vyumba vya kubadilishia nguo Old Trafford baada ya Kocha Sir Alex Ferguson. Ungeweza kujua alikuwa mtu mgumu kiasi gani.

Nawatazama Chelsea. Nahodha wao ni Reece James. Sijui alipataje unahodha. Ni mmoja kati ya walinzi bora wa kulia duniani kama akikwepa majeraha. Ana akili nyingi ya mpira lakini nadhani alipata unahodha Chelsea kwa sababu ni mtoto wa nyumbani. Alikulia Stamford bridge.

Ni kama John Terry alivyoupata unahodha. Lakini subiri sasa. Terry na Reece ni mbingu na ardhi. Terry alikuwa nahodha haswa. Licha ya kwamba alikuwa mtoto wa nyumbani kama Reece lakini Terry alikuwa na sifa zote za unahodha. Chuma cha pua.

PAZ 02

Wachezaji wengi wa kigeni waliojazana Stamford Bridge wakati ule walikubaliana na uongozi wa Terry. Kina Michael Ballack. Mjerumani alikuwa chuma cha moto Ujerumani na nahodha wa Ujerumani lakini alipofika darajani alitulia.

Manchester City wana nahodha wao. Bernardo Silva. Simuoni kuwa nahodha. Jaribu kumlinganisha Silva na Patrick Vieira au Roy Keane. Silva fundi wa mpira lakini mlaini. Sioni kama anaweza kuita Kundi la wachezaji wa Manchester City akawatia moto.

Anaweza kuwaita wakatii kwa sababu ni mkongwe klabuni na ni fundi wa mpira lakini Silva ni Odegaard mwingine tu. Sio nahodha hasa kama wale manahodha kina Paul Ince ambao tuliwahi kuwajua na kuwapenda.

Virgil van Dijik anastahili kuwa nahodha wa Liverpool. Hakuna shida. Sio chuma cha pua sana lakini kwa wachezaji waliopo Liverpool anastahili kuwa nahodha. Kiongozi kutokea nyuma. Hana vurugu sana lakini anastahili kuwa nahodha.

PAZ 01

Kama angecheza kando ya Steven Gerrard asingeweza kuwa nahodha. Angeongozwa na sio kuongoza. Kama angecheza kando ya Paul asingeweza kuwa nahodha. Angeongozwa. Lakini kwa wachezaji wa sasa wa Liverpool anastahili kuwa nahodha. Hata katika utatu mtakatifu wa Sadio Mane, Roberto Firmino na Mo Salah bado VVD alistahili kuwa nahodha.

Kuna timu ambayo nadhani ina nahodha hasa. Aston Villa. Kuna mwanaume anaitwa John McGinn. Nahodha haswa. Roho ya Kiscotish. Anatoka Scotland. Wanaume wengi wa Scotland ni wababe na mafundi. Ni kama alivyo babu Sir Alex Ferguson.

McGinn anakupa kila kitu. Fundi. Ana roho ya paka. Kiongozi. Ananikumbusha manahodha wa zamani. Hauwezi kumlinganisha McGinn na Odegaard, Bruno, Reece wala VVD. Kama wewe ni mchezaji ukiangaliwa na McGinn unajua kweli una kiongozi. Kwangu mimi huyu ndiye nahodha bora ligi kuu ya Mfalme Charles.

Wapo wengine. Granit Xhaka ni nahodha hasa pale Sunderland. Bruno Guimaraes ni nahodha kweli kweli pale Newcastle lakini timu nyingi kubwa zimepoteza viongozi halisi katika ligi kuu ya mfalme.