Prime
Mambo magumu… Simba wanapochapwa na fimbo yao wenyewe
MOJAWAPO ya raha za mpira ni utani unaozaliwa kila uchao na kuwapa mashabiki cha kuongea kila wakati.
Safari hii mada kubwa ya kuongelea ni mateso wanayopitia wakali wa Bunju, Simba SC baada ya matokeo mabaya yanayowaandama.
Vipigo mara mbili mfululizo kutoka kwa Azam FC na vile viwili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika vimewafunga midomo mashabiki wao na kuwaacha wenzao watambe hadi kugalagala.
Mbaya zaidi wanaotamba hawaishii tu kuzungumzia matokeo, wameenda mbali na kuwatafutia Simba SC jina lenye maudhi ambalo hadi mashabiki wao wanalikubali kwa uchungu mkubwa. Jina hilo ni WAGAWA UTAMU SC ambalo sasa limekuwa maarufu na kuvuma kila sehemu.
LIMETOKEA WAPI?
Jina hilo lililetwa na Ahmed Ally, meneja wa Habari wa Simba tangu msimu uliopita alipokuwa akitupa ‘jiwe gizani’ kupitia mashindano ya CAF hatua ya makundi.
Simba waliokuwa kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika walianza vizuri kwa kulitawala kundi na kushinda mechi mbili kati ya tatu za kwanza, wakipoteza moja; Simba 1-0 Bravo, Constantine 2-1 Simba na Simba 2-1 CS Sfaxien
Watani wao wa jadi, Yanga, walianza vibaya kwa kufungwa mechi mbili za kwanza na kupata sare moja; Al Hilal 2-0, Yanga, MC Alger 2-0 Yanga na TP Mazembe 1-1 Yanga. Hapo ndipo palipomuibua Ahmed Ally na kuja na jina la WAGAWA UTAMU.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ahmed alisema wao wanaendelea vizuri kwenye kundi lakini kwa kawaida kwenye mashindano ya Afrika hatua ya makundi lazima kuwe na timu ambayo kazi yake ni KUGAWA UTAMU kwa wenzao.
Yaani ni sawa na kusema KIBONDE WA KUNDI, akitolea mfano CS Sfaxien katika kundi ambao walikuwa wameshapoteza mechi zote hadi wakati huo. Akasema hata katika makundi mengi timu za hivyo zipo, zinagawa tu utamu na mnazijua...hapo sasa ndipo alipowalenga Yanga.
Kwa kweli Yanga waligawa sana utamu katika kundi lao, matokeo yaliyowagharimu kuvuka hatua ya makundi.
LIMERUDI KWAO
Kuna ule msemo wa Kiingereza wa TASTING YOUR MEDICINE yaani kuionja dawa yako mwenyewe. Simba sasa wanaonja dawa yao wenyewe...lile jina limegeukiwa wao.
Mambo yalianzia kwenye mashindano ya CAF tangu hatua za awali kufuzu makundi hadi makundi yenyewe.
Simba haikuwa na matokeo mazuri, kwani haijashinda hata mchezo mmoja nyumbani lakini mbaya zaidi ilifungwa michezo yote miwili ya kwanza; Petro Atletico 1-0 Simba na Stade Malien 2-1 Simba.
Matokeo hayo yakawakumbusha kitu waandishi na kwenye moja ya mahojiano wakamuuliza Ahmed sasa hivi wao wamegeuka kuwa WAGAWA UTAMU wa kundi kama alivyosema msimu uliopita? Hii ilikuwa kuelekea mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC iliyokuja kufanyika Desemba 7, 2025.
Ahmed akajibu ili timu ipate sifa ya kuitwa WAGAWA UTAMU ni sharti ipoteze michezo mitatu mfululizo, sio miwili. Mungu si Athuman, Simba ikafungwa 2-0 na Azam FC, michezo mitatu mfululizo ikatimia...hapo sasa jina la WAGAWA UTAMU likapata mashiko. Kila sehemu ikawa WAGAWA UTAMU tu hadi mashabiki wakakereka sana.
Yakaja mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026 na Simba ikafika nusu fainali na kukutana na Azam FC walewale waliowafunga 2-0 katika ligi. Matarajio yalikuwa Simba washinde ili walivue jina la WAGAWA UTAMU, lakini wakafungwa tena. Hapo sasa hata mashabiki nguvu ziliwaishia na hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kulipokea jina la WAGAWA UTAMU SC.
Mashabiki maarufu wa Simba kama GB 64 wamelipokea na kukiri kwamba hawana jinsi yoyote ya kulikataa kwani wanastahili. Kwa kifupi hivi sasa watu wanawachapa Simba kwa fimbo waliyoichonga wenyewe.
Jina walilolianzisha wao wenyewe kuwakera wenzao linawageukia wao wenyewe na kuwa la kwao. Na yawezekana jina hilo likawakaa kwa muda mrefu kwani ukiangalia ratiba ilivyo na kwa namna timu inavyocheza huoni kama wataliepuka.
Mechi ijayo katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni dhidi ya Taraj SC ya Tunisia ambayo nje ya nchi yao inafahamika zaidi kama Esperance. Taraj ni neno la Kiarabu lenye maana ya TARAJIO (matarajio) au TUMAINI (matumaini) kwa Kiswahili.
Kiswahili kina uhusiano mkubwa sana na Kiarabu na maneno yake mengi yana asili ya Kiarabu.
Mojawapo wa maneno hayo ni matarajio, ambalo asili yake ni neno la Kiarabu la TARAJ ambalo ni jina la wapinzani wao wa Simba. Na kwa Kifaransa neno hilo linatafsirika kama Esperance na ndilo jina maarufu nje ya Tunisia. Sasa matarajio ni kuona Simba anabadilisha upepo na kuwafanya wapinzani wao waponzwe na jina.
Isipokuwa hivyo, basi Simba ndio watakaoteseka kwani jina la WAGAWA UTAMU litaendelea kutamalaki na kuwanyima raha mashabiki wao.