Mambo manne yanayomsubiri kocha mpya Simba Queens
Muktasari:
- Hata hivyo, msimu uliopita umewaacha na maswali baada ya kushindwa kutetea taji la Ligi Kuu ya Wanawake Bara ubingwa ukienda kwa JKT Queens walionyakua kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
SIMBA Queens ni moja ya timu kubwa na zenye historia katika soka la wanawake nchini Tanzania na Afrika Mashariki na Kati ikiweka rekodi mbalimbali ikiwamo kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake mwaka 2022.
Hata hivyo, msimu uliopita umewaacha na maswali baada ya kushindwa kutetea taji la Ligi Kuu ya Wanawake Bara ubingwa ukienda kwa JKT Queens walionyakua kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Tukio hilo lilisababisha mabadiliko ya benchi la ufundi na wachezaji Simba ambayo yalimuondoa kocha Yussif Basigi, raia wa Ghana na kumpa mkataba Elieneza Nicolaus aliyetumikia timu za taifa za wanaume kama kocha wa viungo na atasaidiana na Mussa Mgosi.
Basigi aliondolewa kikosini hapo baada ya kushindwa kutimiza malengo ya timu ya kuutetea ubingwa huo akijikuta wakipoteza mataji mawili ya Ngao ya Jamii na ligi ambayo yote yalinyakuliwa na JKT.
Mwanaspoti limekuchambulia mambo matano yanayomsubiri kocha huyo ambayo ni kurejesha heshima ya Simba Queens, kuleta ubora wa kiuchezaji na kuhakikisha timu inakuwa na mwelekeo wa mafanikio ya muda mrefu.
1. KUREJESHA UBINGWA
Changamoto ya kwanza na kubwa zaidi inayomkabili kocha mpya ni shinikizo la kurejesha taji la Ngao ya Jamii na Ligi Kuu ya Wanawake.
Ligi ya Wanawake Tanzania kwa sasa imeanza kuwa na mvuto wa aina yake hasa linapokuja suala la dabi ya wanawake. Mashabiki wanaitazama kama ile ya wanaume kunyanyua makombe na kushinda kila mechi ili kuwapa furaha.
Kocha mpya anakabiliwa na hali ambayo kila mechi itachukuliwa kama mtihani wa uwezo wake, anapaswa kufanya kazi ya kuongeza nidhamu ya timu kuboresha mbinu za kiuchezaji na kuhakikisha wachezaji wanakuwa na morali ya juu.
Aidha, anapaswa kubuni mikakati ya kuwashinda wapinzani wakuu kama JKT Queens, Yanga Princess, Fountain Gate Princess na timu nyingine zinazoonyesha ushindani kwenye ligi hiyo.
Kosa dogo linaweza kumgharimu nafasi yake mapema jambo linaloonyesha shinikizo kubwa alilonalo. Kimsingi kocha mpya hana muda wa kujenga timu bali anapaswa kuonyesha matokeo ya haraka.
2. KIMATAIFA
Msimu uliopita timu hiyo iliishia hatua ya nusu fainali kwenye mashindano ya CECAFA yaliyofanyika Ethiopia baada ya kutandikwa mabao 3-2 na Kenya Police mwaka 2024 lakini kabla ya hapo mwaka 2022 ilifika hadi hatua ya nusu fainali ya Caf.
Sasa changamoto nyingine kubwa ni kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwenye anga za kimataifa -- Ligi ya Mabingwa Afrika na CECAFA imekuwa jukwaa kubwa la kuonyesha ubora wa Wana Lunyasi hao.
Timu hiyo ilishiriki michuano hiyo na kupata uzoefu, lakini bado haijafikia mafanikio makubwa ya kutwaa ubingwa au angalau kufika hatua za juu kwa misimu mfululizo.
Kocha mpya anapaswa kuweka mikakati ya kushindana na timu kubwa za Afrika kama Mamelodi Sundowns Ladies (Afrika Kusini), AS FAR Rabat (Morocco), na wawakilishi wengine wa kanda mbalimbali.
3. KUREKEBISHA SAFU YA USHAMBULIAJI
Moja ya changamoto kubwa zilizomwangusha Basigi msimu uliopita ni upungufu kwenye eneo la ushambuliaji katika mechi muhimu dhidi ya Yanga Princess ambapo Simba hao wa kike walipoteza kwa bao 1-0 na Mashujaa wakitoka sare ya 2-2.
Msimu uliopita timu hiyo ilifunga mabao 57 dhidi ya 70 waliyoweka kambani JKT kwenye mechi 18 za Ligi.
Simba Queens ilionekana kutengeneza nafasi nyingi lakini ikashindwa kuzitumia. Katika mechi kadhaa dhidi ya wapinzani wakubwa, timu ilionekana kukosa mbinu mbadala za kuvunja ukuta wa mabeki wa wapinzani.
Kocha mpya anakabiliwa na jukumu la kufufua ubunifu na ufanisi katika eneo la mbele. Anapaswa kuhakikisha kwamba washambuliaji wanapata msaada wa kutosha kutoka kwa viungo wabunifu.
Na msimu huu timu hiyo imeongeza washambuliaji watano ambao ni Cynthia Musungu (Besiktas), Zawadi Usanase (AS Kigali), Nandede Zainah (Kampala Queens), Umutesiwase Magnifique (APR Rwanda) na Fadhila Adhiambo (Ulinzi Starlets) wanaoungana na Jentrix Shikangwa na Aisha Mnunka waliokuwapo muda mrefu.
Kilichobaki kwa kocha kufanya marekebisho ya kiufundi, kuimarisha mazoezi ya kumalizia mipira na hata kuleta falsafa mpya ya uchezaji inayozingatia kushambulia kwa kasi na nidhamu ya pasi za mwisho.
4. KUTENGENEZA KIZAZI KIPYA
Kwenye usajili wa msimu huu kuna mchanganyiko wa nyota wapya wachanga waliosajiliwa kutokea akademi mbalimbali akiwamo Elizabeth Nashon (Ceasiaa Queens), Neema Mtunzi (Hanang), Elizabeth Joseph (Alliance Girls), Zuhura Waziri (Ceasiaa Queens) na Asha Omary aliyetokea Yanga Princess.
Moja ya mipango ya timu hiyo msimu huu ni kuwekeza na kukuza vipaji vya mabinti wadogo ambao waliwasajili ili kuweza kupata uzoefu wa timu kubwa na kuwa tegemeo kwenye kikosi hicho baadae na timu ya taifa.
“Kwa hiyo tulioona hatutaendelea nao tukawaacha baadhi na kuongeza wengine wenye ubora zaidi ili watusaidie msimu ujao na usajili uliofanywa ni wa muda mrefu kwa kuwa tuliongeza na vijana wadogo ambao wakipata uzoefu wanaweza kuwa na manufaa kwa baadaye na timu ya taifa.”
Kwa hivyo viongozi wa timu hiyo wameona kuna haja ya kusajili vijana wadogo hivyo matamanio yao ni kuona matunda ya uwekezaji wa muda mrefu hivyo kocha mpya akifanikiwa kuchanganya wachezaji wazoefu na vijana chipukizi, ataijengea Simba kwenye msingi wa mafanikio ya baadaye.
5. MSIKIE MWENYEWE
Akizungumza baada ya kutambulisha malengo yake na timu, Elieneza alisema: “Tuna timu nzuri na wachezaji wanataka mafanikio na kuna kitu wanatafuta na tumeandaa mbinu nyingi na vitu vingi tulivyofundisha wanaonekana kuvishika vizuri, malengo ni kufanya vizuri na kuonyesha mpira mzuri,” anasema na kuongeza:
“Kama kocha, malengo yangu ni kufanya vizuri na kurejesha heshima ya Simba. Nimekaa na wachezaji pia tumeongea nao tunachotakiwa kufanya, naamini msimu huu utakuwa mzuri kwetu.”