Prime
Mambo sita yanayomkabili Folz Yanga
LEO Jumatano, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wanatarajia kuanza kuzichanga karata kutetea taji hilo kwa kuikaribisha Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kwenye mchezo huo, Yanga inaingia ikiwa na rekodi tamu dhidi ya mpinzani wake huyo ikiwa na kumbukumbu ya kumfunga nyumbani na ugenini msimu uliopita jumla ya mabao saba, mzunguko wa kwanza ikishinda 4-0 na mzunguko wa pili 3-0.
Wakati rekodi ikionekana hivyo, ni mtihani kwa kocha mpya wa Yanga, Romain Folz ambaye amejiunga na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu na kukutana na rekodi tamu za watangulizi wake.
Folz hadi sasa akiwa na Yanga, amecheza mechi tano za kirafiki na mbili za mashindano. Upande wa mashindano, alianza na Ngao ya Jamii akiibuka na ushindi mbele ya Simba wa bao 1-0, nyingine ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika akishinda mabao 3-0 dhidi ya Wiliete.
Mwanaspoti linakuletea rekodi nyingine anazotakiwa kuzifikia Folz dhidi ya mtangulizi wake Miguel Gamondi ambaye anainoa Singida Black Stars kwa sasa.
Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 ambapo uongozi wa klabu hiyo ilipomtangaza hakuwa na rekodi yoyote tamu na hasa ugeni wake wa kufundisha soka ukanda wa Afrika Mashariki.
Lakini mwamba huyo aliwathibitisha mashabiki kwamba mabosi wa Yanga hawakukosea kumpa kibarua hicho, kwani ndani ya muda mfupi alifanya maajabu sita yaliyomfanya ajitofautishe na makocha waliopita ndani ya timu hiyo tangu ilipocheza mara ya kwanza makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1998.
MECHI ZA LIGI
Folz akitarajia kuanza kibarua chake kwenye mechi za ligi leo Jumatano kwa kuikaribisha Pamba Jiji, ana kibarua kikubwa kuvunja rekodi za Gamondi ambaye sasa anainoa Singida Black Stars.
Gamondi tangu alipoteuliwa Yanga, aliiongoza timu hiyo kucheza mechi 40 za Ligi Kuu Bara zikiwamo 30 za msimu wa 2023-2024 na 10 za msimu wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hiyo ameshinda 35, sare mmoja na kupoteza minne.
Katika michezo hiyo 40, Yanga chini ya Gamondi ilifunga mabao 87 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14, akikusanya pointi 108.
Msimu uliopita ambapo Gamondi aliiongoza Yanga katika mechi 10 za ligi kabla ya kuondoka, alifanya vizuri zaidi mechi nane za kwanza akishinda zote bila ya kuruhusu bao.
Kwa Folz, huu ni mtihani mkubwa unaomkabili ambapo inaonekana ameanza vizuri kwani katika mechi mbili za kimashindano alizocheza, hajaruhusu bao akishinda zote.
KUIVUSHA MAKUNDI
Folz ambaye ameanza vizuri ugenini kwenye mechi ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wiliete, ana kibarua kikubwa kufikia rekodi za Gamondi ambaye aliipeleka timu hiyo makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25 kufuatia kufanya hivyo mara ya mwisho 1998 wakati huo ikinolewa na kocha wa muda, Tito Mwaluvanda aliyempokea Mwingereza Steve McLennan.
Mwaluvanda alipewa timu hiyo akiwa hana umaarufu wowote na aliyekuwa Mwenyekiti, Rashid Ngozoma Matunda ambapo kikosi hicho kiliangukia kundi la kifo na ASEC Mimosas (Ivory Coast), Manning Rangers (Afrika Kusini) na Raja Casablanca ya Morocco.
Kwa wakati huo, mechi ya kwanza tu Yanga ilichapwa mabao 6-0 na Raja Casablanca, ikachapwa 3-0 na ASEC Mimosas kwenye Uwanja wa Uhuru kisha ikaenda Afrika Kusini kupambana na Manning Rangers na kuambulia kichapo kingine cha mabao 4-0.
Baada ya hapo ikapoteza ugenini 2-1 dhidi ya ASEC Mimosas, 1-1 na Manning kisha sare ya mabao 3-3 na Raja Casabalanca kwenye Uwanja wa Uhuru na kumaliza michezo sita ya hatua ya makundi ikiwa imefunga mabao matano tu na kuruhusu 19.
Gamondi aliyewahi kufundisha timu mbalimbali amefika hatua hiyo ya makundi baada ya miaka hiyo 25 kufuatia kuifunga Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo kwani awali ilikuwa haijawahi kushinda.
Yanga ilikuwa haijawahi kuifunga Al Merrikh katika mechi za CAF ila chini ya Gamondi timu hiyo ya Sudan ilipoteza mabao 2-0 ya Kennedy Musonda na Clement Mzize ikiwa uwanja wa nyumbani Rwanda kisha marudiano jijini Dar es Salaam kuchapwa 1-0.
Maajabu yake ni kwamba ameipokea timu na moja kwa moja kuipeleka makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kitu ambacho hakijawahi kufanywa hata na Nasreddine Nabi, kwani kocha huyo aliyepo kwa sasa FAR Rabat ya Morocco katika miaka miwili na nusu aliyokuwapo Yanga, alikwama mara mbili aking’oka hatua ya awali mbele ya Rivers United ya Nigeria, kisha ikaatolewa raundi ya kwanza na Al Hilal ya Sudan.
ROBO FAINALI
Ushindi wa mabao 4-0, ilioupata Yanga dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, ilimfanya Gamondi kuandika rekodi mpya baada ya 2023-2024 kuivusha robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo tangu michuano hiyo ilipobdilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika mwaka 1997.
Kwa mara ya kwanza Yanga iliwahi kucheza hatua ya robo fainali enzi hizo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970 na kucheza makundi 1998 ila tangu hapo haikuwa na maajabu hadi msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pia iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 na 2018 huku ikifika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika 1995.
KUMPIGA MWARABU 4-0
Haijawahi kutokea kwa timu yoyote ya Tanzania kupata ushindi mnono kwa klabu kutoka Afrika Kaskazini maarufu Waarabu, lakini chini ya Gamondi, Yanga imefanya kweli kwa kuifunga Belouizdad.
Sio kumfunga Mwarabu tu, lakini ushindi ulioenda na soka tamu na la kusisimua lililowaduwaza Waalgeria ambao kwenye mechi ya kwanza nyumbani kwao, walishinda mabao 3-0, licha ya kupigiwa mpira mwingi vilevile.
Ushindi huo uliifanya Yanga kuvuka robo fainali na kocha huyo Muargentina akiipiku rekodi ya Simba.
Simba ilikuwa ikishikilia rekodi ya kuipiga timu ya Afrika Kaskazini kwa mabao mengi, ilipoifumua JS Saoura ya Algerias kwa mabao 3-0 katika michuano hiyo msimu wa 2018-2019 kwa mabao ya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere aliyefunga mawili na kuifanya kumaliza nafasi ya pili katika kundi D ikiwa na pointi tisa nyuma ya vinara Al Ahly.
KUMPIGA SIMBA MKONO
Kama kuna tukio lililomheshimisha Gamondi mbele ya mashabiki wa klabu hiyo na kuwatetemesha wale wa Msimbazi ni kipigo cha 5-1 ilichopewa Simba kwenye Ligi Kuu Bara, kwa upande wa Folz ameanza na shangwe baada ya kutwaa Ngao ya Jamii mbele ya mtani wake Simba licha ya ushindi mwembamba wa bao 1-0.
Simba ilikuwa haijawahi kufungwa 5-1 na Yanga ikiwa ni idadi kubwa ya mabao tangu ilipolazwa 5-0 mwaka 1968, kipigo ambacho Simba ilikilipa kwa kishindo mwaka 1977 kwa kuifumua Yanga 6-0 kisha kupigilia msumari mwingine wa mabao 5-0 mwaka 2012. Vipigo hivyo viliifanya Yanga inyanyasike mbele ya Simba kwani kila walichokuwa wakikifanya walikejeliwa kwamba wameshindwa kulipa kisasi cha 6-0 cha zaidi ya miaka 40, lakini ujio wa Gamondi na miujiuza yake uwamerejeshea jeuri Yanga baada ya mechi hiyo ya Dabi ya Novemba 5, 2024.
Kipigo hicho kikubwa kwa Yanga dhidi ya Simba kilifuatia na kusitishiwa mkataba kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, aliyekuwa akionekana anaijulia sana Yanga kwani ameshaitungua kwenye mechi tofauti ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii, lakini mambo yamebadilika.
VIPIGO VIKALI
Achana na yote hayo, kocha Gamondi ameandika pia ajabu lingine la kutoa dozi nono karibu kwenye michuano yote ambayo timu hiyo imeshiriki chini ya Muargentina huyo.
Yanga ilitoa dozi ya tano tano kwa wapinzani wake kwenye michuano minne tofauti ikiwamo Ligi Kuu Bara, Kombe la Mapinduzi, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho (FA).
Gamondi alianza kwa kuifumua Asas ya Djibouti kwenye mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa kwa mabao 5-1, lakini kuna watu walimpuuza wakisema amewaotea vibonde, lakini akaja kwenye Ligi Kuu akaifumua JKT Tanzania kwa mabao 5-0 kabla ya kuifumua KMC kwa idadi kama hiyo ndipo akaifumua Simba kwa 5-1. Moto wa Gamondi uliendelea kwenye mechi za Kombe la Mapinduzi kwa kuifumua Jamhuri mabao 5-1, huku kwenye Kombe la FA, Yanga ilishinda 5-1 dhidi ya Hausung ya Njombe, kisha kuifumua Polisi Tanzania kwa mabao 5-0 na kutinga hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo.
Rekodi inaonyesha hakuna kocha yeyote nchini aliyewahi kupata matokeo ya kupiga wapinzani 5G, hapo ni mbali na zile mabao 4-1 iliyoipiga Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu Bara kisha kuifumua Belouizdad 4-0 kuonyesha kwamba Yanga ya Gamondi ukikaa vibaya unapigwa nyingi na huwezi fanya lolote.