Man United mpya; Carrick aibadili gia angani
Muktasari:
- Tangu Carrick achukue mikoba Januari mwaka huu, Man United imeshinda mechi saba kati ya 10 zilizopita, tofauti na kipindi cha Ruben Amorim na katika mechi 11 za mwisho kabla hajaondoka mashetani hao wekundu walishinda mechi tatu tu.
MANCHESTER United ipo kwenye njia nzuri ya kurejea Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya mabadiliko makubwa waliyoonyesha chini ya kocha wa muda Michael Carrick.
Tangu Carrick achukue mikoba Januari mwaka huu, Man United imeshinda mechi saba kati ya 10 zilizopita, tofauti na kipindi cha Ruben Amorim na katika mechi 11 za mwisho kabla hajaondoka mashetani hao wekundu walishinda mechi tatu tu.
Hapa chini ni uchambuzi wa kina juu ya mambo ambayo Carrick anaonekana kuyabadilisha kiufundi yanayoonekana kuchangia kiwango bora kinachoonyeshwa na timu hiyo wa sasa.
MASHAMBULIZI YA KUSHTUKIZA
Carrick ameanzisha mfumo wa kujilinda kisha kushambulia kwa kushtukiza na timu huwaruhusu wapinzani kushambulia kiasi cha kuwachosha kabla ya kuwageukia na kurudusha mashambulizi kwa kasi.
Mfumo huu ulitumika kuwafunga Arsenal na Manchester City.
Ingawa kwa sasa timu inatumia mabeki wanne, wakati mwingine mfumo huonekana kama 5-2-1-2. Hii huwapa nafasi ya kushambulia kwa kushtukiza, huku Bruno Fernandes akiwa ndio mhimili wa mashambulizi ya aina hiyo.
PASI NYUMA YA SAFU YA ULINZI
Kwa kutumia kasi ya washambuliaji kama Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko, Man United hucheza mipira mirefu nyuma ya mabeki.
Hata kama pasi hazijafika, mbinu hii huwavuta mabeki nyuma na kufungua nafasi katikati.
Katika mchezo dhidi ya Aston Villa ya Unai Emery, mbinu hii ilisaidia kuunda nafasi nyingi zaidi za mashambulizi.
KUMPA NAFASI KOBBIE MAINOO
Kiungo Kobbie Mainoo amerejea kwenye ubora wake baada ya Carrick kumpa kuchukua mikoba na kumpa nafasi ya kucheza.
Akiwa pamoja na Casemiro, Mainoo kwa sasa anaonekana kuwa huru zaidi, anaonekana kupanda na kushuka tofauti na ilivyokuwa kwa Ruben Amorim ambaye alihitaji staa huyo acheze enei moja tu jambo lililomfanya ashindwe kuonyesha kiwango bora mwisho akakosa nafasi katika kikosi cha kwanza.
MASHAMBULIZI YA PEMBENI
Kurudi kwa Luke Shaw katika nafasi yake ya kawaida ya beki wa kushoto kumebadilisha namna timu inavyoshambulia.
Carrick amempa uhuru wa kuingia ndani au kushambulia pembeni kulingana na hali ya mchezo.
Hii imekuwa tofauti na ilivyokuwa kwa Amorim ambaye hakumpa uhuru sana Shaw na muda mwingi alitaka atimize majukumu yake mama ya kukaba na akawa hapandishi mashambulizi.
Carrick anamtumia Shaw na kumpa uhuru ambao pia anaupata akiwa na timu ya taifa chini ya Thomas Tuchel.
BRUNO NDIO MASTA WA MCHEZO
Bruno Fernandes sasa ana uhuru mkubwa zaidi wa kushambulia badala ya kucheza katikati sana.
Staa huyu ambaye kwa sasa anaiwinda rekodi ya pasi za mabao 20 kwa msimu mmoja katika Ligi Kuu England inayoshikiliwa na Thierry Henry, Bruno ndio moyo wa Man United kwa sasa.
Carrick amempa majukumu ya kutengeneza zaidi mashambulizi na kuhakikisha timu inamiliki mpira.
Vilevile, Bruno huhakikisha timu pinzani haipati muda mwingi wa kuandaa mashambulizi kwa kufanya kazi yakuwa beki wa kwanza akisaidiana na Casemiro na Mainoo.
Vilevile Bruno ndio amekuwa injini ya timu linapokuja suala la mashambulizi ya kushtukiza ambapo kwa asilimia kuwa yeye ndio hutoa pasi za mwisho.
MECHI ZIJAZO
Mashetani hawa wekundu ambao kwa sasa wapo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu England, wanatarajiwa kurudi dimbani Jumatatu na itakutana na Leeds United katika dimba la Old Trafford kuanzia saa 4:00 usiku.
Mbali ya mechi hiyo, April 18 pia itakutana na Chelsea katika dimba la Stamford Bridge kabla kurudi Old Trafford kuvaana na Brentford na baadae kuikaribisha Liverpool.
Mechi hizi zinaonekana kuwa muhimu sana kwa mashetani hawa wekundu kwenye harakati zao za kuwania nafasi ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu ujao.