Man United yalalamikia ratiba Ligi Kuu England
Muktasari:
- Tofauti na baadhi ya wapinzani wao, Man United kwa sasa ianazingatia mashindano ya Ligi Kuu England pekee msimu huu, lakini upangaji wa ratiba umewaacha wakiwa hawajaridhika kabisa.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United inaripotiwa kuwasilisha malalamiko Ligi Kuu England pamoja na kituo cha televisheni cha Sky Sports baada ya kukerwa na ratiba mpya ya mechi iliyotangazwa hivi karibuni.
Tofauti na baadhi ya wapinzani wao, Man United kwa sasa ianazingatia mashindano ya Ligi Kuu England pekee msimu huu, lakini upangaji wa ratiba umewaacha wakiwa hawajaridhika kabisa.
Kikosi hicho cha Kocha Michael Carrick kimepangiwa kucheza mechi tatu mwezi Aprili saa 2:00 usiku. Mechi hizo ni dhidi ya Leeds United na Brentford katika Uwanja wa Old Trafford siku za Jumatatu, huku pia wakisafiri kwenda London kucheza na Chelsea, Jumamosi saa hiyo.
Hii ina maana kuwa kati ya mechi 34 za ligi ambazo tayari zimepangwa hadi sasa, 14 kati yake zimeanza saa 2:00 usiku.
Muda huo hauwafurahishi sana mashabiki, hasa kwa safari ya kwenda Stamford Bridge, Aprili 18, pia kuna mambo mengine yanayoiudhi klabu hiyo ya Old Trafford. Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, maafisa wa Man United wamekasirishwa sana na uamuzi huo wa ligi pamoja na watangazaji wa televisheni. Inasemekana wanaelewa Man United ni timu inayovutia watazamaji wa televisheni, lakini bado wameamua kuwasilisha malalamiko kwa Ligi Kuu England na Sky Sports.
Ratiba hiyo imeathiriwa pia na ukweli Man United haishiriki mashindano mengine msimu huu. Ilitolewa kwenye Kombe la Ligi, Agosti mwaka na Grimsby Town na pia ilitolewa katika Kombe la FA hatua ya raundi ya tatu na Brighton, Januari mwaka huu.
Kutokana na kutoshiriki mashindano ya Ulaya pia, mechi zao huwa rahisi kubadilishwa au kupangwa upya na Ligi Kuu ili kukidhi ratiba za matangazo ya televisheni. Pia Man United ina mapumziko marefu kati ya baadhi ya mechi zao. Kuna pengo la siku 24 kati ya mechi yao dhidi ya Bournemouth, Machi 20 (pia saa 2 usiku) na mechi inayofuata dhidi ya Leeds United, Aprili 13. Baada ya mechi ya Newcastle, Man United itapumzika kwa siku 11 kabla ya kukabili Aston Villa uwanjani Old Trafford, Machi 15.