Carrick anasumbua vichwa Man United
Muktasari:
- Kocha huyo wa muda, aliyechukua nafasi ya Ruben Amorim aliyefutwa kazi, amekuwa na mwanzo bora katika kwenye ligi hiyo baada ya mechi tisa, akiandikisha rekodi bora kabisa katika historia ya Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: MICHAEL Carrick amejiandikisha jina lake katika vitabu vya historia vya Ligi Kuu England na kwa kufanya hivyo amewapa mabosi wa Manchester United presha kubwa juu ya kufanya uamuzi, apewe timu jumla au asipewe.
Kocha huyo wa muda, aliyechukua nafasi ya Ruben Amorim aliyefutwa kazi, amekuwa na mwanzo bora katika kwenye ligi hiyo baada ya mechi tisa, akiandikisha rekodi bora kabisa katika historia ya Ligi Kuu England.
Katika mechi hizo tisa, Carrick ameiwezesha Man United kuvuna pointi 23 kufuatia ushindi wa Jumapili dhidi ya Crystal Palace na hivyo kufikiria rekodi bora iliyokuwa ikishikiliwa na kocha Ange Postecoglou aliyokuwa ameweka akiwa na Tottenham Hotspur.
Uwepo wa Carrick kwenye kikosi cha Man United umekuwa na athari chanya na kuisaidia timu hiyo sasa kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikifukuzia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Ukiweka kando rekodi hiyo ya kihistoria kwenye Ligi Kuu England, Carrick mwenye umri wa miaka 44 pia ameshinda mechi tano mfululizo za ligi katika Uwanja wa Old Trafford, moja katika awamu yake ya kwanza kama kocha wa muda na nne katika awamu hii ya sasa, mafanikio yaliyowahi kufikiwa mara moja tu. Katika kipindi chake cha sasa, ameshinda mechi sita na kutoka sare moja kati ya saba, huku timu yake ikipata matokeo makubwa dhidi ya wapinzani wa ubingwa Arsenal na Manchester City katika mechi zilizofuatana.
Hali hiyo imezua mjadala kwa bodi ya Man United kuhusu mustakabali wa ukocha, wanapopima chaguo la kumteua meneja wa kudumu.
Matokeo ya Carrick yanamweka katikati ya kinyang’anyiro hicho.
Je, Man United wabaki naye na kuchukua tena njia ya kocha mwenye uzoefu mdogo au watafute chaguo jingine lenye uzoefu zaidi kutoka duniani kote? Ni mjadala utakaowagawa mashabiki, kutawala mazungumzo ya soka na pia kupewa nafasi kubwa na wachambuzi wa zamani na vyombo vya habari. Ndani ya kuta za Old Trafford, ilifichuliwa kuwa wachezaji wanataka Carrick apewe mkataba wa muda mrefu.
Vyanzo vinasema wachezaji kama Bruno Fernandes, Harry Maguire na Luke Shaw wamevutiwa na mbinu zake na uelewa wake wa soka la kimataifa. Lakini vipi kuhusu walioko nje ya chumba cha kubadilishia nguo? Wamesemaje kuhusu mustakabali wa Carrick?
Gary Neville: “Siko kinyume naye kuteuliwa. Namthamini sana na nadhani amefanya kazi ya ajabu hadi sasa. Lakini, nahisi Man United wanapaswa kwenda kwa kocha bora zaidi anayepatikana. Wamekuwa na makocha vijana na wasio na uzoefu mkubwa katika chaguo zao mbili za mwisho, na haikuishia vizuri. Ole Gunnar Solskjaer aliwahi kuja kama mchezaji wa zamani, akafanya kazi nzuri kwa miaka kadhaa, lakini mwishowe haikufanikiwa. Nadhani kuondoa hatari kadri inavyowezekana ni chaguo sahihi. Lakini hilo si jambo binafsi dhidi ya Michael ‘namkubali sana.’
Roy Keane alisema awali: “Sidhani kama ni uamuzi sahihi, lakini kila la heri. Kuwa kocha wa muda ni tofauti na kuwa meneja wa Man United anayepaswa kushinda mataji kwa miaka miwili, mitatu au mitano ijayo. Nadhani unaweza kupata kocha bora zaidi kuliko Carrick. Lakini anafanya kazi nzuri.”
Rio Ferdinand akijibu msimamo wa Keane: “Kuna hatari kwa yeyote atakayepewa kazi hiyo. Hata kama Carrick atamaliza msimu vizuri na kupewa kazi, bado kutakuwa na hatari. Kwa majina yote yanayotajwa, kila mmoja ana kiwango chake cha hatari.”
Dion Dublin: “Njia bora ya kujionyesha ni kupata pointi na kuendelea kufanya kazi yako. Michael Carrick ni mtu bora na mwenye tabia nzuri. Hapigi kelele, lakini anafikisha ujumbe wake.”
Msururu wa matokeo ya Carrick umemfanya kuwa kipenzi cha wabashiri kupewa kazi hiyo kwa kudumu. Majina kama Oliver Glasner, Roberto De Zerbi, Julian Nagelsmann, Gareth Southgate na Unai Emery pia wanatajwa katika masoko ya ubashiri.
Huenda Carrick hana jina kubwa au uzoefu mkubwa katika Ligi Kuu England au Ligi ya Mabingwa Ulaya kama kocha, lakini aliwahi kuifundisha Middlesbrough katika Championship kwa jumla ya mechi 136. Je, yeye ndiye mtu sahihi ambaye viongozi wa Man United wanapaswa na wataamua kumwamini?
Muda utaamua. Kwa sasa, anachoweza kufanya ni kuendelea kupata matokeo mazuri, kurejesha timu kwenye mashindano ya juu ya Ulaya na kuhakikisha klabu inanufaika kifedha.