Unambeza Carrick? Msikie anachosema
Muktasari:
- Keane alizungumzia uteuzi wa Carrick, Januari mwaka huu baada ya kutangazwa kuwa kocha wa mpito hadi mwisho wa msimu. Kiungo huyo wa zamani mashuhuri, mwenye miaka 54, aliita klabu hiyo “sarakasi” na kumtaja Carrick kama aliyeshindwa, kabla ya mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England tangu achukue nafasi ya kocha aliyekosolewa sana, Ruben Amorim, katika dabi dhidi ya wapinzani wao Manchester City.
MANCHESTER, ENGLAND: MICHAEL Carrick ameamua kuvunja ukimya na kujibu vikali maoni yaliyotolewa na wachambuzi wa soka kumhusu, akiwemo nyota wa zamani wa Manchester United, Roy Keane.
Keane alizungumzia uteuzi wa Carrick, Januari mwaka huu baada ya kutangazwa kuwa kocha wa mpito hadi mwisho wa msimu. Kiungo huyo wa zamani mashuhuri, mwenye miaka 54, aliita klabu hiyo “sarakasi” na kumtaja Carrick kama aliyeshindwa, kabla ya mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England tangu achukue nafasi ya kocha aliyekosolewa sana, Ruben Amorim, katika dabi dhidi ya wapinzani wao Manchester City.
Keane alisema: “Ninachojali zaidi ni uteuzi na benchi la ufundi waliokuja na kocha. Angalia Michael Carrick, bila kujali jukumu lake lilikuwa nini kule Middlesbrough, nina uhakika lilikuwa kuipandisha daraja. Hakufanikisha hilo. Hivyo unaweza kusema alishindwa huko. Lakini, haimaanishi kwamba yeye ni kocha mbaya. Kwa hakika, ilikuwa kazi ngumu.
“Kila wiki tunazungumzia Manchester United kama klabu bora kuliko zote, lakini kwa sasa sioni hilo hata kwa uteuzi huu na benchi lake la ufundi. Ni fursa kubwa kwa Carrick. Lakini. bila shaka nina wasiwasi na nilisema hivyo pia kwa kocha wa awali. Inaonekana kama sarakasi kwa sasa.”
Carrick alishinda dabi ya Manchester katika mechi yake ya kwanza, kabla ya kuifunga timu nyingine inayowania ubingwa, Arsenal wiki iliyofuata. Kwa kweli, bado hajapoteza katika mechi tano za ligi tangu achukue usukani, huku doa lake pekee likiwa sare ya 1-1 dhidi ya West Ham United mapema mwezi huu. Sasa mzaliwa huyo wa Wallsend, Carrick, mwenye miaka 44, amezungumzia ukosoaji na uchunguzi kutoka kwa wachezaji wa zamani na jinsi unavyomgusa yeye na wachezaji wake.
Carrick aliiambia BBC Sport: “Hainisumbui hata kidogo. Kwa kweli, hainisumbui. Sitagombana na mtu yeyote kuhusu hilo. Nadhani ni suala la heshima zaidi ya kitu kingine chochote na natoa na kupokea hilo. Nafikiri kwa wachezaji vijana kwa ujumla ni jambo tunalopaswa kuwasaidia nalo na kuwalinda. Dunia ni tofauti sasa na ilivyokuwa wakati mimi nilipoanza, lakini tutafanya hivyo na tunawatunza.”
Carrick atapata nafasi nyingine ya kuwathibitishia wakosoaji wake Jumatatu hii wakati Man United itakapokipiga na Everton. Mwanzo wake mzuri umeibua maswali iwapo mkataba wake wa nusu msimu unaweza kuongezwa na kuwa wa kudumu.
Carrick alisema: “Kwangu mimi, hii ni nafasi ya juu kabisa. Ninaifurahia sana, napenda ninachofanya. Nina bahati.”
MECHI ZIJAZO ZA MAN UNITED
-Februari 23 vs Everton (ugenini)
-Machi 1 vs Crystal Palace (nyumbani)
-Machi 4 vs Newcastle (ugenini)
-Machi 15 vs Aston Villa (nyumbani)
-Machi 20 vs Bournemouth (ugenini)