Sunderland yaweka msimamo mgumu kwa Xhaka
Muktasari:
- Xhaka alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu waliowasaidia Sunderland kumaliza katika nafasi za kushiriki michuano ya Ulaya baada ya kurejea Ligi Kuu England msimu uliopita.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Sunderland, Regis Le Bris, ametoa msimamo wa mwisho kuhusu nahodha wake Granit Xhaka kwa kuieleza Chelsea isahau kabisa ndoto ya kumsajili kiungo huyo katika dirisha hili la usajili.
Xhaka alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu waliowasaidia Sunderland kumaliza katika nafasi za kushiriki michuano ya Ulaya baada ya kurejea Ligi Kuu England msimu uliopita.
Chelsea ilijaribu kumsajili, lakini Le Bris amesema hakuna nafasi ya nyota huyo kuondoka.
" Hapana, suala hilo limefungwa kabisa," alisema Le Bris alipoulizwa kuhusu mustakabali wa Xhaka.
"Amekuwa wazi kabisa kuhusu maisha yake ya baadaye. Anaipenda Sunderland, anataka kubaki Sunderland na anataka kujenga mustakabali wa klabu hii. Ni nahodha mzuri na kiongozi bora."
Mapema mwezi huu ilielezwa kuwa Chelsea iliwasilisha ofa ya Pauni 8 milioni kwa ajili ya Xhaka lakini Sunderland iliikataa mara moja na kuiona kuwa ni ya kudhalilisha.
Ingawa kiungo huyo mwenye miaka 33 alivutiwa na nafasi ya kufanya kazi tena chini ya Xabi Alonso, ambaye waliinuka pamoja Bayer Leverkusen, hatimaye aliamua kubaki Sunderland baada ya mazungumzo na viongozi wa klabu.
Mahusiano mazuri aliyonayo na mashabiki wa Sunderland pamoja na mapenzi yake kwa klabu hiyo pia yalichangia uamuzi wake wa kuendelea kubaki Stadium of Light.
Mwaka uliopita Sunderland ilisajili wachezaji 14 baada ya kupanda daraja kutoka Championship.
Lakini safari hii Le Bris amewaomba mashabiki wawe na subira.
Hadi sasa klabu hiyo imemsajili beki wa pembeni Thomas Meunier pekee, ambaye amejiunga nao akiwa mchezaji huru kutoka Lille.
Le Bris alisema:
"Dirisha hili litakuwa tulivu. Tunafanya kazi kubwa nyuma ya pazia na ni muhimu kubaki kimya, vinginevyo kutakuwa na vurugu."
"Tunafanya kazi tofauti na mwaka jana. Wakati ule tulihitaji kusajili wachezaji 14 wapya, lakini safari hii haitakuwa hivyo. Tutaona kitakachotokea."