Marcus karibu kutua FC Barcelona
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa England mwenye umri wa miaka 28 kwa sasa yupo kwenye mazungumzo ya hatua za mwisho na Barcelona, baada ya kuieleza klabu hiyo kuwa anataka kubaki Hispania baada ya mkopo wake kutoka Man United kumalizika.
BARCELONA, HISPANIA: MARCUS Rashford yupo karibu kukubaliana na masharti ya kujiunga na Barcelona kwa mkataba wa kudumu msimu ujao wa majira ya joto, lakini mazungumzo kati ya klabu hizo bado hayajakamilika.
Mshambuliaji huyo wa England mwenye umri wa miaka 28 kwa sasa yupo kwenye mazungumzo ya hatua za mwisho na Barcelona, baada ya kuieleza klabu hiyo kuwa anataka kubaki Hispania baada ya mkopo wake kutoka Man United kumalizika.
Hata hivyo, mazungumzo kati ya klabu hizo yamekwama kwa muda, huku mikutano zaidi ikitarajiwa kufanyika, ambapo United unakomalia kulipwa Euro 30 milioni, ilhali Barcelona inataka punguzo.
Vyanzo vya United vimesisitiza kuwa Barcelona lazima walipe kiasi hicho cha fedha kama ada iliyowekwa kwenye kipengele cha kumnunua Rashford ikiwa inataka kumsajili moja kwa moja.
United wanaamini bei hiyo ni nafuu ikilinganishwa na thamani yake halisi sokoni, na msimamo huo tayari umeelezwa moja kwa moja kwa mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, Deco. Tayari kumekuwa na mikutano kadhaa kati ya klabu hizo tangu Januari, ambapo Barcelona walijaribu kujadili upya bei na mfumo wa malipo.
Inaripotiwa kuwa Deco pia amependekeza mkopo wa pili wa msimu mzima, ambao ungeipa Barcelona muda zaidi kulipa ada hiyo huku Manchester United wakipata thamani kamili ya mkataba. Rashford anaendelea kufanya vizuri, ambapo katika kipindi chake cha sasa amefunga mabao 10 na kutoa asisti 13 katika mechi 38.
Ubora wake pia unampa nafasi ya kuitwa katika kikosi cha England kinachotarajiwa kushiriki Kombe la Dunia chini ya kocha Thomas Tuchel.
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick ameeleza kwa viongozi wa klabu hiyo kuwa kumchukua Rashford ni moja ya vipaumbele vyake vikuu. Barcelona pia wanatazama machaguo mengine licha ya hilo, ambapo wanafuatilia washambuliaji iwapo makubaliano na United hayatafikia muafaka.
Miongoni mwa majina yanayotajwa ni Pedro Neto wa Chelsea, Abde Ezzalzouli wa Real Betis na Jan Virgili wa Real Mallorca. Majina mengine yanayotajwa ni pamoja na Savinho wa Manchester City, Said El Mala wa FC Koln na Eliesse Ben Seghir wa AS Monaco.
Kwa upande wao, Manchester United wanataka kuondokana kabisa na mshahara wa Rashford kwenye orodha ya mishahara ya klabu, na haionekani kuwa kocha mpya ataweza kubadili msimamo huo. Mchezaji huyo analipwa Pauni 315,000 kwa wiki Old Trafford. Rashford aliarifiwa majira ya joto yaliyopita kuwa hana nafasi siku za baadaye katika kikosi cha United.
Kwa sasa bado ana zaidi ya miaka miwili katika mkataba wake, na itahitajika mabadiliko makubwa ya uamuzi wa klabu ikiwa atalazimika kurejea United iwapo Barcelona hawatamsajili moja kwa moja.