Prime
Mourinho mwalimu wa nidhamu, Bernabeu darasa la viburi
ALIKUWA amekaribia kabisa kuelekea kwao Setubal. Ndio, ni kilomita 47 tu kutoka Lisbon Kwenda kitongoji cha Setubal. Nyakati zilionekana zimempita. Aliondoka kwao akiwa na nywele nyeusi mwaka 2004, amerudi majuzi tu akiwa na nywele nyeupe. Jose Mourinho.
Lakini ghafla simu yake imeita. Mpigaji wa simu amepiga kutoka Hispania. Nchi Jirani. Jina lake limetokea kama Fiorentino Perez. Bilionea. Tajiri. Mtu na pesa zake. Anahitaji huduma zake. Wakati watu wote tukidhania kwamba nyakati za Mourinho zimepita, ghafla Perez amempigia simu Jose.
Huyu huyu Jose ambaye msimu huu ulioisha ameiongoza Benfica kucheza msimu mzima bila ya kufungwa lakini akaambulia nafasi ya tatu. Umewahi kuona wapi maajabu haya? Huyu huyu ambaye alifukuzwa na rais wa Fenerbahce ambaye alikuwa analalamika kwamba timu yake ilikuwa inacheza mpira mbovu chini ya Mourinho.
Ndiyo, Jose alionekana amepitwa na wakati. Baada ya kuwapa Porto ubingwa wa Ulaya, akaenda zake Chelsea akawapa mataji ya ligi kuu. Akaenda zake Inter Milan akawapa ubingwa wa Ulaya. Akaenda zake Real Madrid akawapa ubingwa wa La liga. Kuanzia hapo akarudi Chelsea, akafundisha Manchester United, akaenda Tottenham Hotspurs, Roma, Fenerbahce kisha akarudi nyumbani.
Kuanzia ujio wake wa mara ya pili pale Chelsea na timu zilizofuata, Jose alionekana kuwa sio yule ambaye tulimzoea. Kila alikopita alionekana kuishiwa na maarifa. Kuna kwingine ambako alidhalilika.
Hata hii ligi ya wakulima ya Ureno ameishia kushika nafasi ya tatu. Katika umri wa miaka 63, Jose alionekana anakaribia kutua katika kikosi chochote cha timu ya taifa, hasa taifa lake la Ureno, ili ale pensheni. Lakini ghafla Perez amenyanyua simu yake na kupiga namba za Jose. Anampatia mkataba wa miaka miwili.
Siku hizi kuna lugha ya mpira inaitwa ‘project’. Kwamba kocha anakabidhiwa mradi maalumu kwa ajili ya kutengeneza kikosi anachokitaka kwa ajili ya mafanikio ya muda mrefu. Kwa Perez na Mourinho lugha hii haipaswi kutumika.
Real Madrid imemtupa Xabi Alonso kwa sababu mfumo wao wa kupata mafanikio hautaki mambo haya. Mambo ya kumpa kocha mkataba wa muda mrefu ili aanze kukisuka kikosi taratibu. Wanataka kununua mastaa ili wapate mafanikio ya haraka.
Tayari pale Santiago Bernabeu wachezaji mastaa wao. Akina Vinicius Junior. Akina Kylian Mbappe. Akina Jude Billingham. Akina Eduardo Camavinga. Wapo wengi katika maeneo mengi. Perez nadhani anahitaji kocha wa Kwenda kuwatia nidhamu wale vijana ambao wana majina makubwa na mishahara mikubwa.
Baada ya ‘project’ ya Alonso kufeli nadhani ameamua Kwenda kwa Jose Mourinho. Kocha mkubwa ambaye anaweza kutuliza viburi vya mastaa katika vyumba vya kubadilishia nguo. Chini ya Alonso akina Vinicius hawakuwa na adabu.
Chini ya Alonso akina Vinicius walikuwa hawaogopi hata kamera na wangeweza kumbwatukia kocha kile wanachojikisia. Nadhani ndio maana Perez ameona kuna umuhimu wa kumpeleka ‘mwalimu wa nidhamu’ wa kukomesha viburi vyao.
Na anapoweza kukomesha hivi viburi huwa anaibuka kuwa mshindi uwanjani. Mourinho amewahi kuwamiliki wachezaji wakubwa zaidi ya hawa akina Vinicius ambao hawana adabu. Amewahi kuwa kocha wa Cristiano Ronaldo. Amewahi kuwa kocha wa Didier Drogba. Amewahi kuwa kocha wa Samuel Etoo.
Amewahi kutwaa mataji ya ligi ya mabingwa wa Ulaya ambayo akina Mbappe hawajawahi kutwaa. Na sasa anakwenda kukomesha viburi vyao na watafuata maagizo yake. perez sio mgeni katika hili.
Aliwahi kumfanya Zinedine Zidane awe kocha wa akina Cristiano Ronaldo. Wangemwambia nini Zidane ambaye ameshinda kila kitu katika mpira? Amewahi kushinda hata kombe la dunia ambalo Cristiano na wenzake ale Madrid hawajawahi kushinda.
Tatizo moja litamkabili Jose. Achilia mbali uwezo wake wa kukomesha viburi vya wachezaji anakabiliwa na changamoto ya kuonyesha ubora wake uwanjani. Ubora ambao kwa kiasi kikubwa inaonekana umefifia. Hili litatia shaka katika uwepo wake Santiago Bernabeu.
Hapa karibuni timu zake zimeshindwa kuonyesha uwezo wa kupaki Basi. Na kama utatafuta mfano wa namna ambavyo sio tu wanashindwa kupaki Basi na vile vile wanashindwa kutafuta ushindi ni namna ambavyo wamemaliza msimu huu kule Ureno wakiwa hawajapoteza pambano lolote lakini wameishia nafasi ya tatu.
Na sasa anarudi zake Real Madrid. Tusubiri kuona ni namna gani anaweza kuwanyoosha kina Mbappe. Ni jambo jema kwa La liga kwa sababu wamepata bidhaa adimu sokoni. Kwa maana ya jina wamempata mtu ambaye anaenda kuisisimua ligi yao ndani na nje ya uwanja.
Mourinho atawapatia La liga vichwa vya habari kuanzia katika mikutano yake na waandishi wa habari. Atatupatia vichwa vya habari kwa namna ambavyo atawaadabisha akina Vinicius hadharani.
Atatupatia vichwa vya habari kwa namna ambavyo atakuwa akipewa kadi nyekundu na waamuzi na pia kufungiwa na watu wa La liga kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Nataka nisikie namna ambavyo atakuwa anatoa maneno ya shombo kwa Lamine Yamal. Nataka nione pia akirudisha yale masekeseke ya El Clasico kama alivyokuwa anafanya wakati ule alipokuwa akikutana na hasimu wake, Pep Guardiola. Moto ulikuwa unawaka sana.
Sidhani kama Madrid watakaa na Mourinho kwa muda mrefu lakini itakuwa habari ya kusisimua kwa muda wote ambao atakuwa England. Na kama atarudi kucheza dhidi ya timu za England katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya itakuwa habari ya kusisimua zaidi. ‘The Special One’ hawezi kuwepo sehemu na dunia ikatulia.