Prime
Ofisi ya kipa lazima kiti akalie mgeni, tumepotea wapi?
MAJUZI nimefuatilia kwa makini michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika Zanzibar hivi karibuni. Nimefurahishwa na kiwango cha kipa Abutwalib Mshery wa Yanga. Imenifikirisha kitu.
Kama Mshery angekuwa anadaka katika lango la timu nyingine nchini isiyo Yanga, Simba au Azam, basi ni wazi angekuwepo Morocco na timu ya taifa. Nilimuona katika michuano ya Mapinduzi akiwa ametulia langoni na akiwa anakamata mpira bila ya hofu. Mpira ulikuwa unanata katika mikono yake kitu ambacho ni nadra kwa makipa wetu.
Miguuni pia alikuwa anajua kusambaza pasi nzuri kwa walinzi wake. Nadhani kila siku amekuwa akijifunza kutoka kwa kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra. Mshery atakuwa anafahamu kwamba Zubery Foba na Hussein Masalanga walipata nafasi ya kwenda Morocco kwa sababu wanacheza mara kwa mara katika timu zao.
Kuna matukio yametokea na yamenishangaza kidogo. Wakati Mshery akiendelea kusugua benchi kwa Diarra, ghafla Yanga imetangaza kumchukua Masalanga.
Siamini kama Yanga inaweza kumuachia Diarra kwa sasa hata kama atahitajika na timu kubwa. Wanamhitaji sana katika michuano ya CAF.
Ina maana Masalanga na Mshery wote wawili wanaenda kusugua katika benchi la Yanga. Hii itampa wakati mgumu kocha wa Taifa Stars, Manuel Gamondi, kuwajumuisha katika kikosi chake siku za usoni. Watu watahoji kwanini anawaita makipa wasiocheza katika klabu. Ni kama ambavyo watu wangehoji kama angeenda na Mshery kule Morocco.
Huwezi kuwalaumu hawa vijana kwa sababu wanaangalia maslahi yao. Wanajua wanaenda kukaa benchi, lakini wanapata fedha nyingi wakati wanasaini mikataba lakini wanalipwa mishahara mikubwa na bonasi nyingi kuliko kucheza timu kama Mashujaa. Hatujazijengea uwezo klabu nyingine kuwatunza wachezaji wake kama wakubwa wanavyofanya. Hili ndilo tatizo.
Jambo jingine ni nasoma mitandaoni kuwa Simba wanasaka kipa wa kigeni kwa sasa kwa sababu wanaamini kuwa kipa wao namba moja, Moussa Camara, hayupo tayari kurudi langoni kwa sasa na itamchukua muda mrefu kupona majeraha yake.
Kipa wa kigeni inaonekana kuwa kitu cha lazima ili tuhesabu kwamba lango la Simba lipo salama. Lazima mabosi wa Simba watakuwa katika msako mkali wa kipa wa kigeni kwa sababu hakuna mzawa ambaye anaweza kuaminika kukaa pale.
Hata kipa wetu namba moja wa timu ya taifa, Yakoub Suleiman, ambaye naye amepata majeraha haaminiki kukaa pale. Alichukuliwa na Simba katika dirisha kubwa la uhamisho ili aje kuwa msaidizi wa Camara na sio kuwa kipa namba moja.
Ina maana hata kama Yakoub angekuwa fiti bado angetafutwa kipa wa kigeni wa kuja kukaa langoni na yeye aendelee kuwa msaidizi. Tunajiuliza kwa nini katika ofisi hii ya kipa lazima kiti akalie mgeni? Kwanini tumefika hapa? Nafasi nyingine uwanjani wazawa huwa wanaaminika lakini hii ya kipa kwa sasa imekuwa kama sheria.
Kwanini tumefika hapa? Suala la kwanza tuangalie katika vipaji binafsi. Zamani tulikuwa na makipa wengi wenye vipaji binafsi. Kuanzia ile Afcon yetu ya kwanza kulikuwa na Athuman Mambosasa, Omary Mahadhi ‘Bin Jabir’ na Juma Pondamali.
Baadaye tuliendelea kuzalisha makipa warefu na wazuri. Kina Moses Mkandawire, Mohamed Mwameja, Riffat Said, Ally Bushiri, Steven Nemes, Joseph Fungo na wengineo kibao. Karibu kila timu ya Ligi Kuu ilikuwa na kipa mahiri na shujaa langoni.
Miaka ya karibuni hatuwezi kumuamini mzawa langoni. Baada ya kutokomea kwa zama za Juma Kaseja akabaki Aishi Manula pekee ambaye aliaminiwa katika lango la Simba.
Baada ya hapo hakuna mwingine ambaye tunaweza kumuamini. Kama vipaji ni tatizo, basi bado tuna tatizo jingine katika kuzalisha makipa. Nadhani kufundisha makipa utotoni au katika ujana wao kimekuwa kitu kigumu. Nadhani tunaichukulia poa hii idara na tumekazana zaidi katika kufundisha wachezaji wa ndani.
‘Goalkeeping area’ tunalichukulia poa eneo hilo. Sidhani kama ni eneo ambalo tunawekeza kwa wataalamu wanaoweza kufundisha ukipa watoto wetu. Kinachotokea sasa hivi ni kwamba mchezaji akiwa kipa wa zamani basi anafundisha watoto kudaka hata kama hana utaalamu wa kufundisha.
Sio lazima kila kipa wa zamani awe kocha wa makipa. Lazima wasomee kufundisha watoto. Mbaya zaidi ni kwamba hata mbinu zenyewe langoni zimekuwa zikibadilika mara kwa mara. Chukulia tu mfano namna ambavyo mpira wenyewe umebadilishwa na kina Pep Guardiola wanaotaka kipa atumie miguu yake vizuri.
Suala la kufundisha makipa tusilichukulie poa kwa sababu hata kwa wenzetu kuna makipa wengi ambao hawakuzaliwa na vipaji, lakini wamefundishwa kufika hapo walipo. Unapoonekana unarefuka kuliko wenzako unafundishwa kuwa kipa.
Kuna kanuni nyingi ambazo unaona makipa wanazitumia kwa sababu wamefundishwa. Sio kwamba wanatumia vipaji, wanafundishwa tu kwamba mpira ukipigwa hivi unapaswa kuucheza vile. Unafundishwa namna ya kujipanga langoni na mengineyo. Ni kanuni za lazima. Sidhani kama sisi tunafanya vya kutosha kwa vijana wetu.
Matokeo yake sasa hivi hatuzalishi makipa hodari. Hii ofisi tumeikabidhi kwa wageni. Ni kama ambavyo tumekabidhi ofisi ya benchi la ufundi kwa wageni. Siamini kama wakubwa watarudi tena kuwaamini makocha wazawa katika klabu zao.
Hawa kina Suleiman Matola, Juma Mgunda na wengineo watakuwa wanapewa ofisi hizi kwa muda tu kama makocha wa muda wakati tukisubiri kupata makocha kutoka nje. Zamani tuliwaamini wazawa lakini taratibu tukaanza kuhisi kwamba wazawa huwa hawatoshi katika nafasi zao.