Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi zinavyobamba Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Wakati ushindani ukizidi kuongezeka na kuvuta hisia za mashabiki na wadau wa soka, zipo rekodi mbalimbali ambazo zimetokea hadi sasa, kutoka katika timu zenyewe, makocha na wachezaji binafsi, kama ambavyo Mwanaspoti linavyozielezea.

MSIMU wa 2025-2026, wa Ligi Kuu Bara, unaendelea kushika kasi kwa sasa Tanzania na tunashuhudia upinzani ukizidi kuongezeka mechi baada ya mechi, huku kila timu ikipambana kwa ajili ya kujiwekea mazingira mazuri mwisho wa msimu huu.

Wakati ushindani ukizidi kuongezeka na kuvuta hisia za mashabiki na wadau wa soka, zipo rekodi mbalimbali ambazo zimetokea hadi sasa, kutoka katika timu zenyewe, makocha na wachezaji binafsi, kama ambavyo Mwanaspoti linavyozielezea.


YANGA YAFIKISHA MABAO 100

Ushindi wa bao 1-0, ilioupata Yanga, Machi 12, 2026, dhidi ya Tanzania Prisons, umeifanya timu hiyo kufikisha jumla ya mabao 100 ya Ligi Kuu, huku pia suluhu ya (0-0), dhidi ya Azam, Machi 15, 2026, imefikisha mechi 34, bila kupoteza.

Mechi hiyo iliyopigwa Machi 12, 2026, kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, bao hilo la ushindi la Yanga lilifungwa na mshambuliaji nyota, Laurindo Dilson Maria 'Depu', dakika ya 79, likiwa ni bao lake la sita msimu huu Ligi Kuu.

Mabao 100 iliyofikisha Yanga ni ya mechi 34 za Ligi Kuu bila ya kupoteza, tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 3-1, dhidi ya TRA United zamani Tabora United, pambano lililopigwa, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Novemba 7, 2024.

Hadi sasa timu hiyo imefikisha siku 493, bila ya kupoteza pambano lolote la Ligi Kuu, sawa na kucheza kwa kipindi cha mwaka mmoja, miezi minne na siku nane.

Katika mechi hizo 34, imeshinda 30 na sare nne tu na safu ya ushambuliaji imefunga mabao 100 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.

Mabao hayo 100, ni rekodi mpya kwa Yanga, kwani hata msimu wa 2021-2022, ambao kikosi hicho kilicheza mechi 49, bila ya kupoteza, kabla ya kutibuliwa katika pambano la 50, ilifunga mabao 84 na kuruhusu 20 na rekodi hiyo ilianzia tangu mara ya mwisho ilipochapwa na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC kwa bao 1-0, Aprili 25, 2021.


BAO LA MAPEMA ZAIDI LIGI KUU

Mshambuliaji wa Costal Union, Bakari Msimu aliandika rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi msimu huu la sekunde ya 58, katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, Februari 10, 2026.

Bao hilo ni kati ya mawili aliyofunga kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya, huku mengine yakifungwa na Shiza Kichuya na Cleophace Mkandala, huku kwa upande wa bao pekee la kufutia machozi kwa maafande wa Prisons likifungwa na George Mpole.

Rekodi ya pili ni ya kufunga mabao yake ya kwanza, huku ya tatu ni ya kuifungia timu hiyo bao la kwanza ugenini msimu huu.

Tangu msimu umeanza, bao hilo la sekunde ya 58, ndilo la mapema zaidi ikisubiriwa kuona atakayeivunja katika mechi zijazo.


FOUNTAIN YAANDIKA REKODI MBILI

Ushindi wa bao 1-0 iliyoupata Fountain Gate dhidi ya Mbeya City katika mechi iliyopigwa Machi 3, 2026, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya, umeifanya timu hiyo kuandika rekodi mbili mpya, baada ya mwenendo usioridhisha.

Rekodi ya kwanza ni ya kushinda mechi ya kwanza mwaka 2026, Ligi Kuu, huku ya pili pia kwa kikosi hicho kilichohamishia makazi yake jijini, Arusha, ni ya kupata ushindi wa kwanza ikiwa ugenini msimu huu.

Kikosi hicho mara ya mwisho kushinda katika Ligi Kuu kiliichapa Tanzania Prisons 1-0, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Novemba 26, 2025 na ilicheza mechi sita, ikichapwa nne na kutoka sare miwili.


JKT TZ NA REKODI MBOVU KWA YANGA

Kipigo cha mabao 5-0, ilichokipata JKT Tanzania, Februari 25, 2026, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam, katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, kimekifanya kikosi hicho cha maafande kuandika rekodi mbili mbovu.

Mabao ya Yanga, yalifungwa na Mohamed Hussein 'Tshabalala' dakika ya 7, Depu dakika ya 60, Mudathir Yahya dakika ya 63, Prince Dube dakika ya 85, huku Shekhan Khamis akipelekea maumivu kwa kupiga la tano dakika ya 89.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Rekodi hizo mbili ni ya kufungwa idadi kubwa ya mabao kama ilivyotokea msimu wa 2023-2024, ilipochapwa 5-0, Agosti 29, 2023, huku ya pili ni kufikisha miaka sita bila ya kufunga bao dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.

Katika msimu huo wa 2023-2024, Yanga ilishinda pia mabao 5-0, yaliyofungwa na Stephane Aziz KI, dakika ya 45+5, Kennedy Musonda dakika ya 54, Kouassi Yao dakika ya 64, huku Maxi Mpia Nzengeli, akifunga mawili kuanzia dakika ya 79 na 88.

Mara ya mwisho kwa JKT kufunga bao dhidi ya Yanga Ligi Kuu, ni sare ya 1-1, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma Juni 17, 2020.

Katika mechi hiyo, bao la JKT lilifungwa na Michael Aidan dakika ya 36, kisha, Patrick Sibomana akaisawazishia Yanga dakika ya 76, huku wachezaji wawili, Lamine Moro wa Yanga na Mwinyi Kazimoto wa JKT Tanzania wakionyeshwa kadi nyekundu.

Tangu Juni 17, 2020, JKT imekutana na Yanga katika mechi saba za Ligi Kuu Bara, imechapwa tano na sare mbili, huku kikosi hicho cha maafande kikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.


CHAMOU ANAIJULIA NAMUNGO FC

Beki wa kati wa TRA United, Chamou Karaboue ameendeleza rekodi bora Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kufikisha mabao mawili, ambayo yote ameyafunga dhidi ya 'Wauaji wa Kusini', Namungo, huku akichezea timu mbili tofauti.

Nyota huyo anayeichezea TRA United kwa mkopo akitokea Simba, alianza kufunga bao lake la kwanza akiwa na kikosi hicho cha Msimbazi, katika ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Namungo FC, Oktoba 1, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini, Dar es Salaam.

Chamou alifunga bao hilo dakika ya 43, huku mengine yakifungwa na beki, Rushine De Reuck, dakika ya 61 na mshambuliaji, Seleman Mwalimu 'Gomez' dakika ya 84.

Baada ya hapo, nyota huyo akajiunga na TRA United kwa mkopo Januari 2026 na aliifungia timu hiyo bao moja likiwa ni la pili kwake msimu huu wa Ligi Kuu, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya Namungo FC, Machi 11, 2026.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Black Rhino, Arusha, Chamou aliifungia TRA United bao la kwanza dakika ya 62, kwa kichwa safi, akiunganisha mpira wa 'frii-kiki', uliopigwa na beki wa kushoto wa zamani wa Simba, Valentin Nouma.

Bao la pili la TRA United katika mechi hiyo, lilifungwa na Mganda Joseph Akandwanaho, dakika ya 90, kwa umaridadi mzuri, baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Namungo, Mussa Malika, aliyekuwa amesogea mbele kidogo ya lango lake.


JKT TZ, COASTAL BAADA YA MIAKA 6

Sare ya bao 1-1, kati ya maafande wa JKT Tanzania dhidi ya kikosi cha Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa Februari 13, 2026, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, ni ya kwanza kwa timu hizo baada ya miaka sita tu.

Kabla ya mechi hiyo, mara ya mwisho kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1, ilikuwa ni Februari 4, 2020, wakati huo kikosi hicho cha JKT Tanzania kikiwa uwanja wa nyumbani, kama ilivyotokea pia kwenye pambano la Februari 13, 2026.

Katika mechi hiyo ya Februari 4, 2020, JKT ilitangulia kupata bao la kwanza lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Adam Adam dakika ya 50, huku Ayoub Lyanga akiifungia Coastal Union dakika ya 61, kwa mkwaju wa penalti.

Tangu Februari 4, 2020, mechi iliyojirudia ya sare ya bao 1-1 ni ya Februari 13, 2026 na JKT ilipata bao la dakika ya nne kwa penalti ya Valentino Mashaka, huku Shiza Kichuya aliyeichezea maafande akiisawazishia Coastal dakika ya 12.

Kuanzia mechi ya Februari 4, 2020, timu hizo zimekutana mara tisa katika Ligi Kuu Bara na JKT imeshinda mara nne, Coastal ikishinda mara tatu na sare mara mbili ambazo ni ya suluhu (0-0), Mei 25, 2024 na ya bao 1-1, Februari 13, 2026.


JOSIAH AWEKA REKODI MPYA

Suluhu ya (0-0), iliyoipata Dodoma Jiji dhidi ya Simba, Februari 25, 2026, imemfanya, Amani Josiah, kuandika rekodi mpya ya kocha wa kwanza kwa 'Walima Zabibu', kupata sare mbele ya kikosi cha Msimbazi, tangu kimepanda rasmi Ligi Kuu Bara.

  • New Content Item (1)
    New Content Item (1)

Tangu Dodoma Jiji icheze Ligi Kuu msimu wa 2020-2021, mechi na Simba ilikuwa ni ya 11 na kati ya hizo imepoteza 10 na kutoa sare moja, huku ikifunga mabao mawili na kuruhusu 22.

Kwa maana hiyo, Josiah aliyejiunga na timu hiyo Oktoba 16, 2025, anakuwa kocha wa kwanza kuandika rekodi mpya ya kupata sare katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba, kwani kabla ya hapo hakuna aliyeweza kufanya hivyo.

Josiah aliyezifundisha Tunduru Korosho, Biashara United 'Wanajeshi wa Mpakani', Geita Gold na maafande pia wa Tanzania Prisons, ameiongoza Dodoma katika mechi 14 na ameshinda nne, akitoka sare mitano na kuchapwa mitano.

Kwa jumla timu hiyo iliyoanza msimu huu na Kocha, Mrwanda Vincent Mashami, imecheza mechi 17 za Ligi Kuu na kati ya hizo imeshinda tano, sare sita na kupoteza sita, ikifunga mabao 14 na kuruhusu 18, ikiwa nafasi ya nane na pointi 21.