Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sio kufungia tu, pangeni ratiba kwa akili

ZENGWE Pict


Ni kawaida kila wiki kusikia uwanja fulani umefungiwa kutokana na kutokidhi viwango vya Leseni za Klabu vilivyowekwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).


Na ukisikia viwango utajua kuna mambo mengi kama yale ya kupandisha gharama kutoka Sh187 bilioni hadi Sh330 bilioni ili ulingane na viwango vya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika kama ilivyokuwa kule Arusha hadi ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inashtuka.


Kumbe la hasha! Wiki inayofuata tu unasikia taarifa nyingine, uwanja huo umefunguliwa baada ya kukidhi viwango hivyo vya leseni za klabu. Unashangaa hayo marekebisho yalihusu nini hasa hadi wiki moja au mbili zikatosha kukidhi viwango?

Mbona iliichukua serikali kufanya maamuzi magumu kuongeza bajeti ya takriban asilimia 80 kukidhi viwango vya CAF, wakati hawa wengine wanachukua wiki moja au mbili tena si kwa gharama kubwa.

ZENG 04

Kinachokuja kukushangaza wiki chache baadaye ni uwanja huo kufungwa tena ‘eti’ kwa sababu ileile ya kutokidhi viwango! Si kwamba adhabu hiyo itachukua muda mrefu, hapana. Itachukua siku chache tu kufunguliwa.

Ni kama vile waendeshaji wa ligi huwa wanataka kuiepusha mechi fulani ya timu pendwa isicheze kwenye uwanja mbovu na baada ya hapo uwanja hufunguliwa ili mambo yaende kama kawaida.

Au unaona huenda waendeshaji wanataka mechi fulani isichezwe mbali ili kuipa unafuu timu pendwa isiathiriwe na uchovu na mchezo huo ukishapita, uwanja unafunguliwa na kuendelea kutumika kama kawaida.

Au ni kama kuna timu ambayo wasimamizi wanataka ibanwe kwa kuchezea mechi yake kwenye uwanja mbovu ndio maana adhabu ya kufungiwa inakuwa ya muda mfupi ili ile mechi ya timu isiyopendwa icheze kwenye uwanja mbovu.

Kuna dhana nyingi zinazojitokeza kila wakati taarifa hizo za kutokidhi viwango vya Leseni za klabu zinapotolewa, hasa kutokana na taarifa hizo kutoeleza hasa tatizo ni nini hadi viwango vilivyokuwa vimefikiwa mwezi Januari vikapotea kabisa mwezi Februari na kufikiwa tena mwezi Machi.

ZENG 03

Mara nyingi tatizo la kutokidhi viwango huonekana kirahisi mechi inapochezwa kwenye uwanja wenye mfumo mbovu wa utoaji maji uwanjani nyakati za mvua.

Uwanja kama wa Sokoine wa mjini Mbeya hukumbwa na tatizo hilo la kutofikia viwango na kufungiwa kwa siku hizo chache hadi mvua inaposimama na ndiyo maana huonekana viwango hivyo vimefikiwa siku chache baadaye.

Mara chache tatizo la viwango huhusu vitu kama vyumba vya kubadilishia nguo au vya waamuzi na vyoo.

Tatizo la eneo la kuchezea ndio sugu kwa viwanja vingi, hasa ambavyo havijawekwa nyasi bandia. Maji hutuama sehemu nyingi za uwanja na hivyo kusababisha mpira kuonekana kama unachezwe kwenye mashamba ya mpunga.

ZENG 02

Huwa najiuliza wapangaji ratiba hutumia vitu gani kupanga mechi kiasi kwamba hawaangalii hata majira ya mwaka yanakwendaje au utabiri wa hali ya hewa kujua uwanja kama wa Sokoine utasumbua wakati wa mvua na hivyo kuepuka kuipangia timu mwenyeji mechi nyakati hizo.

Mara kadhaa fainali za Mataifa ya Afrika zimehamishwa kutoka Juni hadi Januari kutokana na waandaaji kujua kuwa nyakati hizo katika nchi fulani za ukanda fulani, huwa zina mvua kubwa zinazoweza kuathiri mashindano kwa kiasi kikubwa, ingawaje Morocco waliweza kukabiliana na hali hiyo kutokana na uwekezaji mkubwa kwenye viwanja vyao kulingana na majira hayo ya mwaka.

Kwa hiyo, badala ya kusubiri kutoa taarifa ya kufungia uwanja ‘eti’ kuonyesha waandaaji ni wakali katika suala la ubora wa viwanja, ni muhimu nao wakawa wakali katika kupanga ratiba kulingana na hali ya hewa au majira ya maeneo tofauti ya nchi.

ZENG 01

Viwanja vingi vya nchi yetu havitumiki kikamilifu nyakati za mvua na ili viweze kutumika kunahitajika uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kukausha maji kwa haraka ili mchezo usiathiriwe na mvua. Hili haliwezi kuchukua mwaka mmoja au miwili. Linahitaji wamiliki wafanye kazi ya ziada kupata fedha za kufanikisha hilo.

Kwa hiyo ni muhimu likaepukwa katika hatua ya upangaji ratiba na ikiwezekana timu ambazo zinatumia viwanja ambayo husumbua nyakati za mvua, zikaambiwa kabisa kuwa ifikapo Machi, mechi zake zitahamishiwa uwanja mwingine ili zijipange na kutaarifu mashabiki, wadhamini na wadau wengine kuwawezesha kupanga mipango yao mapema na si baada ya kuambiwa uwanja umefungiwa.

Uwanja wa nyumbani ni muhimu sana si kwa timu pekee, bali hata mashabiki na wakazi wengne wanaoweza kutumia fursa ya mechi kufanya shughuli a ujasiliamali. Hata wadhamini hujua eneo linalotumiwa na timu fulani lina soko la bidhaa gani kati ya bidhaa zao zote au bidhaa yao imetangazwa kwa kiasi gani.

Kuhamishahamisha mechi hakuna afya kwa mpira wa miguu zaidi ya kuugeuza kuwa “bora liende”. Ni muhimu sana kwa waendeshaji kuacha kiburi cha kuona kufungia ndio kitu pekee kinachoonyesha umakini wao katika suala la ubora wa uwanja, bali umakini wao pia unahitajika kuonyesha wanazijali timu, mashabiki wao, wadhamini na wadau wengine.