Prime
Bodi ya Ligi inavyopaswa kuilinda Ligi Kuu Bara
LIGI Kuu England inatarajiwa kumalizika Mei 24 baada ya safari ndefu ya kuanzia Agosti 15, 2025 na itamalizika kwa kila timu kucheza mechi 38 kutokana na mashindano hayo kushirikisha timu 20.
Hadi sasa ni klabu mbili tu, Manchester City na Crystal Palace ndizo hazijacheza mechi 31 kama nyingine 18, maana yake ni hadi mwisho wa wiki iliyopita timu 18 zilikuwa zimeshacheza 31 na zimebakiza mechi saba tu kufunga msimu.
Hayo yanafanyika wakati klabu sita zilishiriki mashindano matatu ya barani Ulaya yanayoandaliwa na Chama cha Soka cha Ulaya (UEFA), yaani Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Europa Cup na Conference Cup. Klabu nne hushiriki Ligi ya Mabingwa, moja mbili huenda Europa, na moja hushiriki Conference.
Kuna uwezekano England ikatoa timu tano kwenye Ligi ya Mabingwa ijayo kutokana na klabu zake kufanya vizuri msimu huu unaoisha.
Pia hayo yanafanyika wakati timu ya taifa ya England inashiriki michuano ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) na ile ya Uefa, ambayo huandaa mashindano mawili; michuano ya kufuzu na fainali za Mataifa ya Ulaya, pamoja na Nations League, mashindano ambayo huchezwa kwa mtindo wa ligi.
Uahirishaji mechi za Ligi Kuu huwa wa nadra sana na hufanyika wakati kukiwa na jambo kubwa lisiloweza kuzuilika kama majanga makubwa.
Ushiriki wa klabu za England katika mashindano ya UEFA huwa hauathiri mechi za Ligi Kuu kwa kuwa wapangaji huzingatia sana kalenda ya UEFA na ile ya FIFA.
Timu zinazocheza Ligi ya Mabingwa Jumanne hupangiwa mechi zake za Ligi Kuu Ijumaa ya wiki inayoisha, wakati zinazocheza Jumatano hupangiwa mechi zake Jumamosi au Jumapili kwa ajili ya kuzipa muda wa kutosha wa kupumzika.
Huku ni misimu miwili tu tumetuma timu nne kwenye mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), yaani timu mbili zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Zaidi ya mashindano hayo mawili ya Afrika, msimu husimama pale kunapokuwa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi.
Leo hii, ligi iliyo na timu 16 ndio kwanza imeanza mzunguko wa pili baadhi ya timu zikiwa zimecheza mechi 17, nyingine 16, zipo zilizocheza 15 na zilizobaki zimecheza 14. Hakuna uwiano unaoonyesha kuna umakini katika kuhakikisha raundi moja inachezwa ndani ya siku tatu kama ile kamati maarufu inavyojiita; Kamati ya Saa 72.
Yaani ukizingatia siku hizo tatu, ingekuwa ni vigumu kwa timu kutofautiana sana kwa idadi ya mechi zilizochezwa. Hizo sita zilizocheza mechi 17, ziliharakishiwa nini hadi kufikia idadi hiyo? Na hizo zilizocheza 14 zilisubirishwa kwa sababu gani hasa? Na vipi hizo zilizocheza mechi 15 na hizo za 16?
Ni rahisi sana kwa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kujitokeza kuzungumzia sababu za timu moja kuchezeshwa mchakamchaka ili imalize viporo kwa sababu hoja ni ‘eti’ ilikuwa ikiahirishiwa mechi wakati inashiriki Afrika. Lakini si kitu rahisi ofisa wa TPLB kujitokeza na kuzungumzia tofauti hiyo ya timu sita kucheza mechi 17, timu moja kucheza mechi 14, nyingine moja kucheza mechi 15 na timu saba kucheza mechi 16.
Maana yake ni uhairishaji mechi hufanywa kiholela bila ya kujali athari zake. Ushiriki wa klabu zetu katika mashindano ya kimataifa hauwezi kuwa tatizo kwenye ligi yetu, labda tu kama hatuko makini kulishughilikia hilo. CAF hutoa ratiba mapema inayoonyesha mechi zake zitachezwa wakati gani ili kuzipa mamlaka za soka za wanachama wake uwezo wa kupanga ratiba zao vizuri na kuepusha uahirishaji ovyo wa mechi.
Ni muhimu TPLB ikaanza kuwa na wivu na mashindano yake kwa kuwa wagumu kukubali maombi ya klabu zetu kuahirishiwa mechi za ndani eti zijiandae vizuri kimataifa. Ni wakati sasa wa TPLB kuona thamani ya mashindano yake na kuyalinda ili yasipoteze mvuto na ladha.
Ikiwa TPLB itakuwa imeweka ugumu wa kuahirisha hovyo mechi, klabu zitajifunza na kujipanga vizuri kulingana na mahitaji ya wasimamizi na waendeshaji wa ligi. Ushiriki wa klabu zetu Afrika hauongezi thamani kwa TPLB bali unazijenga klabu na kupunguza thamani ya Ligi Kuu. Nadharia kubwa siku hizi duniani ni utengenezaji wa thamani.
Kitu kingine kinachosababisha mechi kuahirishwa hovyo ni maandalizi ya timu ya taifa. Tulipomaliza fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (AFCON), mara timu ikaondoka kwenda kuweka kambi Misri eti kujiandaa kwa mechi dhidi ya Morocco na Zambia.
Hayo mambo ya kambi ni ya kizamani sana. Timu ya taifa huundwa na wachezaji walio tayari kushindana, kiufundi, timamu kimwili na kisaikolojia. Timu za taifa huwekwa kambi za muda mrefu pale zinapoenda kushiriki mashindano ya vituoni (tournaments), lakini si mashindano ya ligi kama michuano ya kufuzu.
Kwa hiyo hiyo dhana ya kuwa timu itaandaliwa vizuri kwa kuweka kambi nje ya nchi kujiandaa kwa mchezo mmoja haipo katika soka la kisasa. Hata kanuni za FIFA zinaeleza ni siku ngapi mchezaji anatakiwa aruhusiwe na klabu yake kujiunga na timu ya taifa. Na siku hizo zinatofautiana kidogo katika suala la umbali, yaani safari ya kutoka bara moja hadi jingine.
Kwa hiyo, TPLB na klabu zikiwa shupavu hazitaruhusu kambi kama hizo za Taifa Stars kwa kuwa zinavuruga na kuchelewesha kumalizika kwa ligi, achilia mbali afya za wachezaji zinazoathiriwa na kutopata muda wa kutosha wa kupumzisha miili.
TPLB pia inabidi iwe shupavu kukabiliana na uyumbishwaji unaofanywa na klabu za Kariakoo. Tumeona ligi ya mwaka jana ilivyocheleweshwa hadi Juni kutokana na siasa za Simba na Yanga.
Tunaposema Bodi ya Ligi ni lazima iwe huru ili iendeshe mambo yake vizuri, ni katika masuala kama hayo. Kwamba Shirikisho la Soka (TFF) likitaka kambi ya wiki moja nje ya nchi, Ligi Kuu inasimama kwa kuwa hakuna uhuru wa kuigomea kwa kutumia kanuni za FIFA za klabu kuruhusu wachezaji wa timu ya taifa.
Bodi huru ya ligi inaweza kupambana hata pale shirikisho linapoandaa mechi za kirafiki nje ya kalenda ya FIFA kwa kuwa klabu zina wadhamini, mashabiki na wawekezaji wanaotaka waone timu zao zikicheza kwa kadri ya ratiba na mipango yao ya promosheni. Tunahitaji Bodi ya Ligi yenye wivu na mashindano yake na inayolinda thamani ya mashindano yake, inayowajali mashabiki wa soka na isiyotaka ligi yake ipoteze ladha.