Siri ya kunukia vizuri bila kuwakera wengine
Muktasari:
- Unatakiwa pia kujua harufu gani inafaa kwa sehemu unayokwenda, kwa sababu marashi ya sherehe si lazima yawe marashi ya ofisini, na yale yanayofaa kwenye chakula cha jioni yanaweza kuwa mazito ukiyapeleka kwenye safari ndefu.
Kuna watu wakiwa wanakuja, unawajua wamefika hata kabla hujawaona, si kwa sababu ya hatua zao, bali kwa sababu ya harufu ya marashi iliyowatangulia. Hata hivyo, hapa ndipo wengi hukosea; kunukia vizuri si kumwaga marashi mengi mwilini.
Unatakiwa pia kujua harufu gani inafaa kwa sehemu unayokwenda, kwa sababu marashi ya sherehe si lazima yawe marashi ya ofisini, na yale yanayofaa kwenye chakula cha jioni yanaweza kuwa mazito ukiyapeleka kwenye safari ndefu.
Marashi yana uwezo wa kuongeza mvuto, kukufanya ujisikie vizuri na hata kuacha kumbukumbu kwa watu unaokutana nao. Hata hivyo, kiasi na aina ya harufu ni muhimu. Mahali unapoenda, muda wa siku, hali ya hewa na watu unaokutana nao vinaweza kuamua aina ya marashi unayopaswa kutumia. Haya hapa maeneo mbalimbali na aina ya harufu zinazoweza kuendana nayo.
KAZINI
Kazini si sehemu ya kuonyesha una chupa mpya ya marashi. Kwa kuwa unakaa karibu na wafanyakazi wenzako kwa muda mrefu, chagua harufu nyepesi, safi na tulivu, kama harufu ya limau na matunda jamii hiyo, maua laini au harufu ya miti isiyokuwa nzito.
Marashi mepesi yanafaa zaidi kwa mazingira ya ofisini kwa sababu hayatawali chumba kizima. Usipulizie kupita kiasi kwa sababu harufu kali inaweza kuwafanya wengine wasijisikie vizuri, hasa kwenye ofisi ndogo au sehemu yenye kiyoyozi. Pulizia kiasi kwenye shingo na vifundo vya mikono ili harufu ibaki karibu na mwili.
SAFARINI
Safari ndefu inahitaji tahadhari zaidi kwa sababu unaweza kukaa karibu na watu ambao hawajui unapenda harufu gani. Ukiwa kwenye basi, ndege au gari, epuka marashi mazito yenye harufu kali sana.
Badala yake, chagua harufu ya ubaridi, usafi au matunda yenye ukakasi kidogo, kwa sababu huwa nyepesi na hailemei mazingira. Pulizia kiasi kabla ya kuanza safari. Kama safari ni ndefu, unaweza kuongeza baadaye badala ya kupulizia nyingi mara moja.
CHAKULA CHA JIONI
Unapoenda kula chakula cha jioni kwenye mgahawa au sehemu maalumu, unaweza kutumia marashi yenye harufu inayoonekana zaidi lakini bado yenye kiasi. Harufu za vanila, maua, matunda, miti au manukato yenye utulivu zinaweza kufaa.
Epuka kutumia marashi mengi kwa sababu chakula kina harufu yake. Harufu kali ya marashi ikichanganyika na harufu ya chakula inaweza kuwakwaza watu waliokaa karibu nawe. Lengo ni unukie vizuri unapokuwa karibu, si kufunika harufu ya chakula.
KWENYE SHEREHE
Sherehe ni moja ya sehemu ambazo unaweza kutumia marashi yenye harufu nzito kidogo kwa sababu kuna watu wengi na mara nyingi mazingira huwa na nafasi kubwa. Kwa harusi, sherehe za kuzaliwa au burudani za usiku, unaweza kuchagua marashi yenye harufu ya miti, vanila, manukato mazito au mchanganyiko.
Hata hivyo, kutumia marashi yenye harufu kali haimaanishi kumaliza nusu ya chupa. Pulizia kiasi kwenye shingo, nyuma ya masikio na sehemu za mapigo ya mwili. Harufu ikipulizwa kwa kiasi huweza kudumu na kuonekana vizuri bila kuwazidia wengine.
KWENYE MIADI YA WAWILI
Unapokwenda kukutana na mtu maalumu, chagua harufu inayovutia lakini isiyomchosha mtu aliye karibu nawe. Marashi yenye harufu ya vanila, matunda, miski au miti laini yanaweza kufaa kwa mazingira haya.
Pulizia kiasi kwenye shingo, nyuma ya masikio na vifundo vya mikono. Epuka kuchanganya aina nyingi za marashi kwa wakati mmoja kwa sababu harufu zinaweza kugongana na kutoa harufu isiyopendeza.
MTOKO WA UFUKWENI
Ufukweni kunahitaji harufu inayokupa hisia ya ubaridi na usafi. Kwa mazingira yenye joto, chagua marashi yenye harufu ya maji, limau na matunda jamii hiyo au harufu safi na nyepesi.
Epuka kutumia marashi yenye harufu nzito sana wakati wa mchana, kwa sababu joto linaweza kufanya harufu isikike kwa nguvu zaidi. Kiasi kidogo kwenye shingo na vifundo vya mikono kinaweza kutosha.
USHAURI
Kwa kifupi, marashi mazuri si yale yanayonukia zaidi, bali yale yanayolingana na mazingira. Kabla ya kupulizia, jiulize unaenda wapi, utakaa na watu kwa muda gani na hali ya hewa ikoje. Ukijua hilo, utaweza kuchagua harufu inayokufanya unukie vizuri bila kuwakwaza watu wanaokuzunguka.