Prime
Tuzo za BMT haziwezi kumuona Fred Minziro
Muktasari:
- Hili ni jukumu kubwa ambalo likifanywa kwa usahihi na kwa kuzingatia vigezo bora, huchochea sana wanamichezo na vyama kufanya jitihada za kweli ili mwishoni mwa mwaka waenziwe kwa kadri inavyostahili.
MOJAWAPO wa madhumuni ya kuanzishwa kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ni kuenzi wanamichezo wanaofanya vizuri katika maeneo yao kila mwaka ili kuchochea maendeleo ya mchezo husika.
Hili ni jukumu kubwa ambalo likifanywa kwa usahihi na kwa kuzingatia vigezo bora, huchochea sana wanamichezo na vyama kufanya jitihada za kweli ili mwishoni mwa mwaka waenziwe kwa kadri inavyostahili.
Lakini, jukumu hili likifanywa kwa kulipua thamani ya tuzo zinazotolewa mwishoni mwa msimu kuenzi jitihada za wanamichezo na vyama vya michezo hupungua na ishara zake huwa ni kutoshiriki kwa wadau wakubwa kwa kuwa wanachukulia kama ni tuzo zinazotolewa ama kuridhisha kila mtu au kupendelea watu ama taasisi fulani au kushusha watu wanaojiona kuwa wamefanikiwa sana.
Ndio maana taasisi kubwa zinazotoa tuzo ulimwenguni hujiwekea vigezo imara na makini kuhakikisha kuwa vinatengeneza thamani kwa tuzo zinazotoa na hivyo kutengeneza kuaminika kwa wadau wa michezo.
Kuna taasisi zinazotoa tuzo kwa kuangalia takwimu, tuzo ambazo huwa hazina ubishi na hazina chochote cha kushangaza au kustua kwa sababu takwimu ziko tayari mezani. Lakini zipo taasisi zinazotoa tuzo au kuwathaminisha wachezaji na taasisi zao kwa kuingia ndani zaidi kuangalia mambo ya msingi ya mchezo husika.
Kwa mfano, shirika la utangazaji la Sky Sport hufanya uchambuzi wake wa wachezaji bora kwa kuangalia rekodi zaidi ya zile za majukumu ya kawaida.
Mfano, kazi ya kiungo mshambuliaji huwa ni kutengeneza nafasi kwa wamaliziaji. Hivyo inapotokea kwenye mechi ametengeneza au kutoa pasi za mwisho kwa mabao mawili au matatu, hilo huchukuliwa kuwa ni jukumu la kawaida kwake kwa kuwa ndiyo kazi yake.
Lakini kiungo huyohuyo wa ushambuliaji anapokwenda mbali zaidi kwa kutoa pasi za mwisho na kufunga huchukuliwa kuwa amefanya kazi zaidi ya majukumu yake ya kawaida na hivyo pointi zake katika kutafuta viungo bora huwa nyingi.
Hali kadhalika beki wa kati ambaye ameiongoza safu yake ya ulinzi kutoruhusu bao na papohapo kutoa pasi ya bao au kufunga kabisa huyo huchukuliwa kuwa amefanya kazi zaidi ya majukumu yake ya kawaida na hivyo kustahili kuwa beki bora miongoni mwa mabeki wengi ambao waliongoza safu zao kutoruhusu mabao.
Hali kadhalika, kazi ya makipa huwa ni kuhakikisha nyavu zao haziguswi hovyo, Hivyo hilo ni jukumu lake la msingi ambalo haliwezi kusababisha awe kipa bora. Lakini pale anapokwenda mbali zaidi na kuwezesha ngome yake iwe na idadi kubwa ya wachezaji pale inapomiliki mpira golini kwake au kupiga pasi inayoweza kusababisha bao (key pass) au pasi ya mwisho (assist), basi hujinyakulia pointi nyingi katika kinyang’anyiro cha kipa bora.
Na mshambuliaji huwa ni hivyo. Kazi yake ni kufunga na hivyo anapofunga bao moja au mawili tena ya kusogezea mpira nyavuni huwa ametekeleza majukumu yake ya kawaida. Sifa huja pale anapofanya jitihada zisizo za kawaida kama kufunga bao katika mazingira magumu, kuhusika katika kuanzisha mashambulizi au kuhusika katika kulinda ngome huyo hujinyakulia pointi nyingi katika kulinganisha na wenzake.
Michezo iko mingi kama riadha ambayo juhudi binafsi ndio kitu muhimu. Hali kadhalika ngumi, mpira wa pete, wavu na wa kikapu. Lakini yote huwa na vigezo tofauti vya kuwapata wachezaji bora, kuanzia kwenye takwimu kama mpira wa kikapu na netiboli hadi juhudi binafsi.
Kuna wakati kocha wa klabu ya ligi ya pili kwa ukubwa nchini England alishinda tuzo ya kocha bora. Si kwa sababu aliiongoza timu yake kupanda daraja, la hasha, bali aliiongoza timu hiyo kutoshuka daraja katika mazingira magumu ya hali ya kifedha na mambo mengine.
Haya ndio mambo ambayo makocha kama Fred Felix Minziro hukutana nayo. Hupewa timu ikiwa katika mazingira magumu ya kubaki Ligi Kuu na hali ya kifedha ikiwa ileile waliyokuwa nayo makocha wengine, lakini huhakikisha timu yake haishuki daraja. Na hajafanya hivyo mara moja!
Makocha kama hawa hawawezi kufikiriwa kwenye tuzo za BMT kwa kuwa kigezo kikubwa ni kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Minziro anaweza kuonekaje kwenye tuzo za BMT kama majukumu aliyopewa yalikuwa ni kuhakikisha timu haishuki daraja katika mazingira ya usajili uleule na fedha zilezile?
Kuna wachezaji ambao wanafan ikiwa kufunga idadi nzuri ya mabao wakiwa katika vikosi ambavyo vinaelekea kushuka daraja na juhudi zao haziwezeshi timu zao kubakia daraja la juu, hawa nao tutasema hawastahili tuzo kwa sababu timu zao zilishuka daraja? Kuna wachezaji ambao wametekeleza majukumu yao ya kawaida ya kutoa pasi za mwisho, lakini walifanya hivyo katika mazingira ambayo wachezaji wenzao walifanya kazi kubwa zaidi ya kulinda timu na kuvuruga mipango ya timu pinzani, inakuwaje tunapowapa tuzo hao walionufaika na juhudi za wengine?
Utoaji tuzo huanzia katika kutengeneza vigezo vya kuzawadia washindi. Na si lazima vigezo vifanane kote duniani, la hasha. Bali vigezo vitengenezwe kwa kuzingatia malengo ya kukuza michezo badala ya kuenzi matokeo ambayo hayajulikani yamepatikanaje. Ni muhimu BMT ikaanza kutengeneza vigezo ambavyo vitachochea ushindani na kusaidia kukuza vipaji vya wanamichezo wetu, makocha, viongozi na wadau wengine wote ili jumuiya ijue kuwa washindi walienziwa kwa hoja zipi na baadaye wajifunze kutoka kwao.