Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walilofanya CAF kwa Senegal, tuweke hisia pembeni, tuangalie ukweli

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza, unahisi huenda ni ile siku ya wajinga duniani (April Fool’s Day), kwa sababu taarifa yenyewe inaonekana ya kushangaza na isiyo ya kawaida.

GHAFLA unapata taarifa Morocco ndio mabingwa wa AFCON 2025, toleo la 35 lililofanyika kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini kwao.

Kwa mara ya kwanza, unahisi huenda ni ile siku ya wajinga duniani (April Fool’s Day), kwa sababu taarifa yenyewe inaonekana ya kushangaza na isiyo ya kawaida.

Lakini baada ya kuchunguza kwa makini, unashtuka kugundua hii si masihara bali ni habari ya kweli kabisa, inayothibitishwa na vyanzo vinavyoaminika na hata kuwa gumzo kubwa duniani.

Mjadala unaibuka kila kona ya dunia, huku watu wakitoa maoni yao kwa hisia kali. Wengi wanaonyesha kusikitishwa, wengine wanakejeli vyombo vinavyosimamia soka Afrika, wakidai kuna ubabaishaji mkubwa. Lakini tukisimama na kujiuliza kwa utulivu, je, kweli tatizo ni ubabaishaji, au ni namna tunavyoshindwa kuelewa na kuheshimu kanuni tulizojiwekea?

Kwa mtazamo wangu, sehemu kubwa ya watu wanaotoa maoni wanaongozwa zaidi na hisia kuliko uhalisia wa mambo.

Wengi wanaamini kila kitu kinapaswa kufuata mifumo ile ile iliyozoeleka Ulaya au maeneo mengine, kana kwamba Afrika haina uwezo wa kusimamia na kuboresha mifumo yake.

Huu ni mtazamo ambao kwa kiasi kikubwa unaweza kuitwa utumwa wa fikra hali ya kuamini kilicho nje ndio sahihi zaidi kuliko kile tulichonacho au tunachoweza kukiboresha.

Tukija kwenye tukio lenyewe, hoja kubwa ipo kwenye uamuzi uliochukuliwa dhidi ya timu ya taifa ya Senegal. Kwa mujibu wa taarifa, Senegal waligomea mchezo na kutoka uwanjani kabla ya muda wa kawaida wa mchezo kumalizika. Hapa ndipo kanuni za mashindano zinapoingia.

Kanuni ya 82 ya mashindano hayo inaeleza wazi timu yoyote itakayoondoka uwanjani kabla ya mchezo kumalizika bila ruhusa ya mwamuzi, itapoteza mchezo na kuondolewa kwenye mashindano. Kanuni ya 84 inaenda mbali zaidi kwa kusisitiza timu hiyo itapoteza mchezo kwa mabao 3-0 na itaondolewa rasmi kwenye mashindano.

Sasa swali la msingi ni hili: Je, Senegal waliondoka uwanjani kabla ya mchezo kumalizika? Kama jibu ni ndiyo, basi ni wazi walikiuka kanuni zilizowekwa. Na kama kanuni zilikiukwa, je, tunatarajia nini kutoka kwa kamati inayosimamia mashindano hayo? Je, isiwe ni wajibu wao kuzisimamia na kuzitekeleza bila kujali hisia za watu?

Wapo wanaosema matokeo ya dakika tisini hayapaswi kubadilishwa baada ya mchezo. Kauli hii ni maarufu sana katika soka, lakini ukweli ni haitekelezwi kwa kila tukio. Kuna matukio mengi matokeo hubadilishwa mezani kutokana na uvunjifu wa kanuni. Mfano mzuri ni pale timu inapomchezesha mchezaji asiye na sifa hata kama imeshinda uwanjani, inaweza kupokonywa ushindi huo.

Kwa hiyo, kwa nini tukio hili lionekane la ajabu sana? Je, ni kwa sababu limetokea Afrika? Au ni kwa sababu watu wengi hawapendi kuona kanuni zikisimamiwa kwa ukali?

Ni muhimu pia kujiuliza, si sisi ndio mara nyingi tunasisitiza vyombo vyetu vya ndani kama TFF na Bodi ya Ligi kuwa makini katika kusimamia kanuni? Tunaposhuhudia uvunjifu wa sheria, huwa tunadai hatua kali zichukuliwe. Sasa inapofanyika hivyo kwenye ngazi ya juu zaidi, kwa nini tunaanza kulalamika?

Kamati iliyochukua uamuzi huu imechagua kusimamia kanuni badala ya kupendwa na umma. Huu ni uamuzi mgumu, lakini ni wa kisheria. Wamekumbusha taasisi yoyote iliyoundwa kusimamia mashindano ina wajibu wa kuhakikisha sheria zinafuatwa.

Kuna mifano mingi duniani na timu zimewahi kupokonywa ubingwa hata baada ya misimu kadhaa kupita, pale inapobainika kulikuwa na uvunjifu wa sheria. Hii inaonyesha sheria hazina muda wa mwisho wa kutekelezwa pale zinapokiukwa.

Wengine wanaweza kumlaumu mwamuzi, wakisema alipaswa kuchukua hatua mapema. Ni kweli mwamuzi ana wajibu mkubwa, lakini hata kama alikosea, hilo halifanyi kosa lililofanywa na timu kuwa sahihi. Makosa mawili hayafanyi jambo kuwa sahihi.

Kwa hiyo, badala ya kuangalia suala hili kwa hisia, ni vyema tukaliangalia kwa jicho la kisheria na kiutawala. Je, kanuni zilikiukwa? Kama ndiyo, basi hatua zilizochukuliwa zina msingi.

Kwa mtazamo wangu, uamuzi huu unapaswa kuwa fundisho kwa timu zote na wadau wa soka, kanuni si mapambo, zipo kwa ajili ya kufuatwa. Pia unapaswa kuwa mfano kwa kamati nyingine kwamba mamlaka waliyopewa ni kwa ajili ya kusimamia haki na utaratibu, si kufurahisha watu.

Tuweke hisia pembeni, tuangalie ukweli. Soka si tu mchezo wa uwanjani, bali pia ni mchezo wa sheria na kanuni. Na pale kanuni zinapovunjwa, lazima zisimamiwe bila kujali nani anaumia au nani anafurahia.