Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WANAUMEEE! Haya ndio majeshi ya Mapinduzi 2026

MAPINDUZI Pict

Muktasari:

  • Katika michuano ya msimu huu kuna jumla ya timu 10 zikiwamo tano za Tanzania Bara, Simba, Yanga, Azam FC, Singida Black Stars na TRA United pamoja na URA kutoka Uganda na klabu nne za Zanzibar, watetezi wa taji, Mlandege, Fufuni, KVZ na Muembe Makumbi.

MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi 2026 inaanza rasmi leo kwa kupigwa mechi mbili za Kundi A ikianza ile ya watetezi Mlandege dhidi ya Singida Black Stars saa 10:15 jioni kabla ya saa 2:30 usiku Azam FC itakwaruzana na URA ya Uganda.

Huu ni msimu wa 20 tangu michuano hiyo ilipoanza kwa mfumo wa sasa mwaka 2007, huku kwa miaka 18 imeshuhudiwa mechi zinazohusisha klabu mbalimbali kabla ya mwaka huu (2025) kutumiwa na timu za taifa zilizokuwa zikijiandaa na michuano ya CHAN 2024 iliyoandaliwa kati ya Tanzania, Kenya na Uganda na kushuhudiwa wenyeji Zanzibar Heroes ikibeba taji mbele ya Burkina Faso.

Katika michuano ya msimu huu kuna jumla ya timu 10 zikiwamo tano za Tanzania Bara, Simba, Yanga, Azam FC, Singida Black Stars na TRA United pamoja na URA kutoka Uganda na klabu nne za Zanzibar, watetezi wa taji, Mlandege, Fufuni, KVZ na Muembe Makumbi.

Hapa chini ni dondoo fupi za timu hizo 10 zitakazochuana kuwania zawadi ya Sh150 milioni na ile ya mshindi wa pili akijizolea Sh100 milioni mbali na zawadi nyingine za kila mechi na zile za jumla zinazohusisha Timu Bora, Mchezaji Bora na Kipa Bora zilizoboreshwa na waandaaji wa michuano hiyo inayoenda sambamba na Miaka 62 ya Siku ya Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964.

MAPI 07

MLANDEGE

Ndio watetezi wa taji hilo inalolishikilia kwa misimu miwili mfululizo kuanzia 2023 na 2024 ikiwa pia ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar, taji ililotwaa msimu uliopita ikiizidi akilia JKU iliyokuwa ikitetea taji.

Hii ni timu inayotarajiwa kuonyesha upinzani kutokana na aina ya kikosi ilichonacho kwa sasa ikiwa na baadhi ya nyota wa kigeni, ingawa itakuwa na kibarua kigumu cha kutetea taji hilo kwa msimu wa tatu ili kufikia rekodi inayoshikiliwa na Azam, timu pekee iliyowahi kutwa taji mara tatu mfululizo.

Nyota inayowategemea kuwabeba katika mbio hizo za kutetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo ni Suleiman Juma 'Kidawa', Mudathir Juma 'Muda Park', Aimar Hafidh 'Haaland', Mussa Hassan 'Mbappe' na wengine wanaoifanya timu hiyo kupewa nafasi ya kutetea ubingwa kama ikakaza buti.

MAPI 04

AZAM FC

Hii ndio timu iliyobeba mara nyingi ubingwa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi tangu 2007 ikifanya hivyo mara tano, 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.

Ni moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa huo kutokana na kuwa chini ya kocha mzoefu, Florent Ibnge ambaye ameifikisha Azam kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Azam inacheza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na katika Mapinduzi 2026 ipo Kundi A sambamba na Mlendege, URA na Singida Black Stars.

Ni timu yenye wachezaji wenye majina na wazoefu wa mechi za mashindano akiwamo Japhte Kitambala, Himid Mao, Nassor Saadun, kipa Aishi Manula na Issa Fofana, Yeison Fuentes na wengineo, japo itawakosa nyota watano waliopo Morocco katika michuano ya AFCON 2025.

MAPI 08
MAPI 08

SIMBA

Wekundu wa Msimbazi itakayokuwa chini ya kocha mkuu mpya, Steve Barker inapewa nafasi ya kufanya kweli katika michuano hiyo itakayoitumia kama sehemu ya kunoa makali kabla ya kurejea katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa makundi pamoja na Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

Simba inayoshikilia rekodi ya kucheza fainali 10 na kubeba ubingwa mara nne ikishika nafasi ya pili nyuma ya Azam yenye mataji matano, ipo Kundi B sambamba na Muembe Makumbi na Fufuni bna itawategemea nyota wote ambao hawajaenda katika michuano ya AFCON 2025 sambamba na wapya.

Mara ya mwisho kwa timu hiyo kubeba ubingwa ilikuwa mwaka 2022 na ilipoteza fainali ya mwisho ya 2024 mbele ya Mlandege, hivyo huenda msimu huu ikaja na moto kuliko awali ikitegemea wachezaji kama kina Hussein Abel, Rushine de Reuck, Jonathan Sowah, David Kameta 'Duchu', Mzamiru Yasin na wengine ambao baadhi walishaishiriki michuano hiyo misimu ya nyuma.

MAPI 03

YANGA

Wababe hao wa soka wa Tanzania Bara imeenda Mapinduzi ikiwa na kocha mpya Pedro Goncalves atakayeitumia michuano hiyo kujiweka tayari kabla ya kurejea kwa michuano ya CAF na Ligi Kuu Bara, pia kuwapima wachezaji wasiotumika kikosi cha kwanza ili kupitisha panga.

Mara ya mwisho kwa Yanga kubeba ubingwa ilikuwa mwaka 2021 ilipoitambia watani wao Simba kwa penalti na kufanya ifikishe mataji mawili likiwamo la 2007.

Ni kati ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa ikiwa Kundi C sambamba na TRA United na KVZ na itawategemea wachezaji wake wote ambao hawakuitwa timu za taifa zinazoshiriki AFCON 2025 akiwamo Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Frank Assinki, Kibwana Shomary, Abutwalib Mshery, Salum Abubakar na wengine ambao wana uzoefu mkubwa na michuano hiyo.

MAPI 01

SINGIDA BLACK STARS

Ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo, japo kuna baadhi ya wachezaji walikuwa na Singida Big Stars (sasa Fountain Gate), lakini ni moja ya timu nne za Tanzania Bara zilizopo hatua ya makundi ya michuano ya CAF ikiwa Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hii ambayo ilikuwa ikifahamika kama Ihefu kabla ya kununuliwa na kubadilishwa jina inapewa pia nafasi ya kufanya vizuri michuano ya Mapinduzi kutokana na kuwa na kikosi chenye wachezaji wenye majinma makubwa na uzoefu wa mechi za aina hiyo chini ya kocha David Ouma.

Kocha mkuu wa timu hiyo yupo AFCON sambamba na baadhi ya nyota kama Habib Idd 'Gego', Khalid Aucho na makipa mawili, Nickson Kibabage, Hussein Masalanga na Amas Obasogie, lakini bado haifanyi Singida kuchukuliwa poa kwani bado ina majembe ya maana na wazoefu wa michuano hiyo ya Mapinduzi kama Clatous Chama, Kelvin Kijiri, Gadiel Michael, Marouif Tchakei, Kennedy Juma, Elvis Rupia aliyekuwa Mfungaji Bora wa michuano ya mwaka 2024 na wengine waliocheza enzi wakiwa na Singida Bis Stars wanaotarajiwa kusumbua timu pinzani.

Kumbuka Singida BS pia ndio mabingwa wa Kombe la Kagame 2025 iliyotwaa katikati ya mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa kuizima Al Hilal ya Sudan.

MAPI 02

TRA UNITED

Inashiriki michuano hii kwa mara ya kwanza ikiwa mi miongoni mwa timu 10 na ipo visiwani chini ya kocha mzoefu, Etienne Ndayiragije sambamba na nyota wenye majina makubwa wanaotarajiwa kusumbua visiwani humo.

Wachezaji kama Adam Adam, Yassin Mustafa, Shaaban Idd Chilunda, Nassor Kapama, Reliants Lusajo, Abdulaziz Makame 'Bui' wenye uzoefu wa michuano hiyo pamoja na wengine wana kazi ya kuibeba timu hiyo iliyopangwa Kundi C sambamba na Yanga na KVZ.

Mseto wa wachezaji na kocha iliyenaye ni wazi wapinzani wa TRA (zamani Tabora United) itawapa kibarua kigumu wapinzani wa kundi hilo na michuano hiyo kwa ujumla ikizingatiwa timu hiyo imewahi kuitoa nishai Yanga katika Ligi Kuu kwa kuifunga kwa mabao 3-1.

MAPI 04

URA FC

Mabingwa hao wa zamani wa michuano hiyo ya Mapinduzi 2016 imerejea tena ikiwa kundi moja na Azam, Mlandege na Singida BS na inapewa nafasi ya kusumbua katika michuano hiyo kama ilivyowahi kufanya mara zote ilishiriki ikiwamo ilipopoteza fainali mbele ya Azam mwaka 2018.

Timu hiyo iliyo chini ya Kocha Alex Isabirye aliyeteuliwa mwezi mmoja uliopita kuchukua na nafasi ya David Obua amebeba matumaini na kurejea kilichofanywa na timu hiyo mwaka 2016 na 2018 kubeba ubingwa ikianza na kazi ya kuwabana wapinzani wao wa Kundi A.

Nyota tegemeo wa timu hiyo ni Fred Amaku, Joseoph Ssemujju, Ibrahim Wamannah, Justine Opiro na wengineo katika kuhakikisha inaondoka visiwani Zanzibar kwa mara nyingine na taji la Kombe la Mapinduzi kama ilivyokuwa 2016.

WAWAK 02

FUFUNI

Hii ni timu mpya iliyopanda Ligi Kuu Zanzibar msimu huu kutoka Pemba na kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo ikiwa imepangwa kundi moja sambamba na Simba na Muembe Makumbi. Haipewi nafasi kubwa ya kufanya maajabu kutokana na ugeni  katika mechi za kimataifa kama hizo, lakini inasifiwa kuwa na wachezaji wenye vipaji vya soka na kucheza soka la kitabuni, na ndio maana sio ajabu kwa sasa kuongoza msimamo wa ligi ya Zanzibar ikicheza mechi 15 na kuvuna pointi 30.

Hata hivyo, itakuwa na kazi ya ziada mbele ya wapinzani wa Kundi B ikiwamo Simba na Muembe Makumbi inayoshiriki pia fainali hizo za Mapinduzi kwa mara ya kwanza tangu ilipopanda Ligi Kuu Zanzibar msimu uliopita, ili kuitafuta nusu fainali na hatimaye fainali ya Mapinduzi 2026.

Timu hiyo ipo chini ya Kocha Suleiman Mohammed 'Mani Gamera' ambaye anawategemea nyota walioipandisha daraja na wengine waliosajiliwa msimu huu kufanya maajabu katika michuano hiyo ya 20 tangu mwaka 2007.

WAWAK 03

MUEMBE MAKUMBI

Ni moja ya timu nne za Zanzibar zilizobeba tumaini la visiwani hivyo katika michuano hiyo. Ni timu iliyopanda Ligi Kuu Zanzibar msimu uliopita na kuanza kwa kasi ikiongoza msimamo wa ligi kiasi cha kukaribia kutwaa ubingwa kama sio kuzembea mwishoni na kuzidiwa na Mlandege na kujikuta ikimaliza katika nafasi ya nne.

Inasifika kwa soka la ushindani na wachezaji wenye kutandaza soka kiufundi chini ya kocha mzoefu wa michuano hiyo, Sheha Khamis Rashid, ikipewa nafasi ya kusumbua kwa aina ya wachezaji ilionao, ingawa inapaswa kufanya kazi mbele ya Simba na Fufuni.

WAWAK 01

KVZ

Maafande hao waliomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Zanzibar msimu uliopita ikitofautiana na Mlandege kwa mabao ya kufunga na kufungwa ipo Kundi C na itakata utepe msimu huu wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Yanga kabla ya kumalizana na TRA United.

Ni timu inayosifika kwa kucheza soka la nguvu na la ushindani pia ni wazoefu wa michuano Kombe la Mapinduzi kwani misimu miwili ya 2023 na 2024 ambavyo Mlandege ilibeba ubingwa a kutetea ilishiriki na kutoa upinzani mkali ikiwamo kuzidindia Mlandege na Yanga na kutoka nao sare tofauti.

Ilitolewa robo fainali na Mlandege 2024 kwa penalti 3-2 baada ya muda wa kawaida kumalizika wa suluhu kitu kinachoonyesha msimu wake huu wa tatu mfululizo inaweza kufanya kitu kama benchi la ufundi n wachezaji wa timu hiyo wataamua kukomaa na kupambana mwanzo mwisho.

Nani atakayeibuka mbabe wa michuano ya msimu huu inayoanza leo Jumapili na kufikia tamati Januari 13 kwa kupigwa fainali, siku moja baada ya maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi ikirejea tukio tukufu lililofanyika Januari 12, 1964? Tusibiri tuone!