Prime
Barker: Kuna shida Simba
UKIONA mtu mzima analia ujue kuna jambo. Ndicho unachoweza kusema baada ya kocha mkuu wa Simba, Steve Barker kulalamikia ugumu wa ratiba wa mechi za Ligi Kuu Bara ulivyokiathiri kikosi chake na kuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la majeraha kwa wachezaji.
Simba yenye pointi 57, wapo nafasi ya pili katika mbio za ubingwa na watani zao Yanga (pointi 60) na sasa ushindani umekuwa mkali hakuna anayetakiwa kupoteza mchezo kwani kufungwa au sare ni wazi itakuwa mwisho wake katika mbio hizo.
Ndani ya siku 66, Simba iliyo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 58, imecheza mechi 16 ikiwemo tatu za Kombe la CRDB, hivyo imekuwa na wastani wa kucheza mechi moja ndani ya siku nne.
Kocha huyo alisema hali ya uchovu imekuwa kubwa kwa wachezaji kutokana na kucheza mechi nyingi muda mfupi huku baadhi yao wakilazimika kucheza wakiwa na majeraha madogo ili kuhakikisha timu inaendelea kupata matokeo.
Kocha huyo alisema baadhi ya nyota wamekuwa wakipambana na majeraha ya aina tofauti huku wengine wakikosekana kabisa katika mechi muhimu za mwisho wa msimu. Katika mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji, Simba ilimkosa beki Rushine De Reuck huku Clatous Chama akitoka uwanjani anachechemea wakati Seleman Mwalimu akicheza akiwa hayupo fiti kwa asilimia 100. Pia, beki David Kameta ‘Duchu’ alipata tatizo wakati wa maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo huo.
“Wachezaji wengi wana majeraha madogo na uchovu mkubwa. Duchu alipata tatizo wakati wa mazoezi ya mwisho, Chama alikuwa anacheza akiwa na maumivu kidogo, Mwalimu pia alikuwa na majeraha madogo huku Rushine akiwa hayupo kabisa,” aliongeza Barker.
Barker sasa anaamini mapumziko ya wiki mbili zijazo yatakuwa msaada mkubwa kwa kikosi chake kurejea katika hali bora kabla ya kuanza mechi tano za mwisho za ligi pamoja na hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.
“Ni muda muhimu kwa wachezaji kupumzika, kurejea katika hali nzuri na kujiandaa kwa hatua za mwisho za msimu. Bado tuna mechi kubwa mbele yetu,” alisema Barker.
Katika mechi tano zilizosalia msimu huu kwa Simba itacheza mechi tatu nyumbani na mbili ugenini.
Simba watalejea uwanjani Juni 14 dhidi ya Pamba Jiji (nyumbani), siku nne baadaye Juni 18, watakuwa ugenini kuivaa Mbeya City, kabla ya kuifuata Mtibwa Sugar mkoani Morogoro (Juni 24), watarejea Dar es Salaam, (Juni 27) kuivaa Singida Black Stars na mechi ya mwisho watacheza nyumbani dhidi KMC (Juni 30) huku wakiwa na mechi moja ya nusu fainali ya Kombe la CRDB dhidi ya Coastal Union (Juni 20) itakayochezwa Arusha.
Kwa mujibu wa ratiba ya mechi hizo, Simba itakuwa na wastani wa kucheza mechi moja kila baada ya siku tatu mara baada ya kumalizika kwa kalenda ya FIFA.