Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dabi hii! Lazima kieleweke ‘goma’ litapigwa sana hapa


ILE Dabi ya Kariakoo katika duru la pili la Ligi Kuu Bara, inapigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, ambapo Simba itakuwa mwenyeji wa Yanga.


Timu hizo zinakutana katika dakika 90 zenye presha kubwa, kila moja ikiwa na hesabu zake tofauti lakini zote zikilenga ubingwa.


Simba, ikiwa nyumbani, inalazimika kushinda ili kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Yanga kwani hivi sasa tofauti yao ni tano. Yanga inaongoza ligi kwa pointi 47, inafuatia Simba yenye 42.

Kushindwa kufanya hivyo kutamaanisha kuipa nafasi kubwa Yanga kuelekea kutetea ubingwa wa ligi hiyo.

Iwapo mchezo huo Simba itaambulia sare au kipigo, itakuwa pigo kwao ambayo inataka kukatisha ukame wa kutwaa taji la ligi, mara ya mwisho ilibeba msimu wa 2020-2021.

Simba inaingia kwenye dabi hiyo ikiwa na morali ya juu baada ya kushinda Fainali ya Kombe la Muungano Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.

Baada ya ushindi huo, wachezaji waliocheza fainali walirejeshwa haraka Dar es Salaam kwa ndege ili kupata mapumziko, huku wengine wakirejea na boti.

Hofu kubwa kwa Simba ni hali ya majeraha ya winga Anicet Oura aliyepata tatizo la misuli ya paja kwenye fainali hiyo na kutolewa dakika ya 26, ingawa juhudi zilikuwa zinafanyika awe fiti kwa mchezo wa leo huku taarifa zikibainisha hakuumia sana.

Pia, beki Ismael Toure alimaliza mechi hiyo akiwa na maumivu, lakini taarifa zinaeleza kuwa yuko tayari kwa mchezo huo.

Kwa upande wa Yanga, baada ya kupoteza fainali ya Muungano, ilibaki visiwani Zanzibar kwa maandalizi kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa siri.

Yanga inahitaji ushindi kurejesha imani kwa mashabiki wake na kuonyesha kuwa imejirekebisha baada ya kupoteza taji hilo.

Ingawa imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Simba kwa kushinda mara sita mfululizo kabla ya kusimamishwa kwa sare na kipigo.

Yanga inahitaji ushindi au sare ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa tano mfululizo. Mabingwa hao watetezi bado hawajapoteza mechi yoyote ya ligi msimu huu, huku Simba ikiwa imepoteza mmoja.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alifanya mazungumzo binafsi na baadhi ya wachezaji wake ili kuwaandaa kisaikolojia kabla ya mchezo huo.

Mechi hii Yanga itawakosa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kutokana na majeraha pamoja na kiungo Mudathir Yahya anayetumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu na Bodi ya Ligi Tanzania.

Hata hivyo, Chadrack Boka anatarajiwa kuendelea upande wa kushoto, huku Duke Abuya akitarajiwa kuanza eneo la kiungo wa kati baada ya kutokea benchi katika fainali ya Muungano.


BARKER NA HATMA YA PEDRO

Dakika 90 za dabi hii, zinaweza kubadili kila kitu Yanga kuanzia mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara hadi hatma ya kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves.

Awali, Pedro ambaye hajapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-2026, aliwekwa kikaangoni takribani miezi miwili iliyopita baada ya Yanga kutoka sare tatu mfululizo dhidi ya Azam FC (0-0), TRA United (0-0) na Mtibwa Sugar (1-1).

Matokeo hayo yaliibua taharuki kubwa ndani ya uongozi na mashabiki wa klabu hiyo, yakilazimisha kukaa kikao kizito cha kufanya tathimini ya mwenendo wa timu hiyo.

Katika kikao hicho, hatua ya haraka ilichukuliwa kuimarisha benchi la ufundi kwa kumrudisha Abdihamid Moallin, ikiwa ni awamu yake ya pili ndani ya Yanga.

Uamuzi huo ulionekana kuwa na matokeo chanya kwa muda mfupi, kwani timu ilirejea kwenye makali yake kwa kushinda mechi sita mfululizo, zikiwemo za Kombe la FA na Kombe la Muungano.

Hata hivyo, katikati ya wiki hii Yanga ilipoteza Kombe la kwanza msimu huu kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Simba katika fainali ya Kombe la Muungano, kipigo hicho kilichotokea kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kinatajwa kurudisha presha kwa kocha huyo raia wa Ureno. Sasa, dabi hii inachukuliwa kama mtihani halisi kwa Pedro.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa matokeo ya mchezo huo yanaweza kuamua hatma yake, ushindi unaweza kumnusuru lakini kichapo kinaweza kumuweka katika wakati mgumu zaidi ndani ya klabu hiyo.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 47 huku Simba ikifuatia na pointi 42. Hii ina maana kuwa ushindi kwa Yanga utaongeza pengo hadi pointi nane, hatua itakayoiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutetea ubingwa.

Lakini kama Simba itashinda, tofauti itapungua hadi pointi mbili na kurejesha ushindani mkali wa ubingwa.

Kwa upande wa Simba chini ya Steve Barker, dabi hii ni zaidi ya mchezo wa kawaida. Mbali na kuhitaji kuendeleza morali ya ushindi walioupata Jumatano, pia wanahitaji kuvunja rekodi mbaya dhidi ya Yanga.

Katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu Bara, Simba haijashinda hata moja dhidi ya Yanga, imechapwa nne mfulizo huku mchezo mmoja ukiisha kwa sare. Takwimu hizi zinaongeza uzito wa dabi hii na kuifanya kuwa vita ya heshima pamoja na matokeo.

Rekodi hiyo pia inaipa Yanga kujiamini zaidi lakini wakati huohuo inaongeza presha kwao kulinda ubora huo. Kwa Simba, huu ni mchezo wa kulipiza kisasi na kurejesha hadhi yao mbele ya watani wao wa jadi.

Katika mazingira haya, mchezo wa leo unageuka kuwa na sura mbili kwa upande mmoja ni pambano la ubingwa na kwa upande mwingine ni vita ya makocha wawili wenye malengo tofauti.

Barker anahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya ubingwa na kuvunja mwiko, wakati Pedro anahitaji matokeo chanya ili kuendelea kujikita kileleni mwa Ligi hiyo pamoja na kulinda kibarua chake.


WAMOROCCO KUAMUA

OFISA Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda alisema kuchagua waamuzi kutoka Morocco ili kuchezesha Dabi ya Kariakoo kati ya Simba dhidi ya Yanga, si pendekezo la klabu, bali ni muongozo wa kanuni za ligi.

Kauli ya Boimanda imekuja baada ya TPLB kuwatangaza waamuzi wa mechi hiyo akisema: “Waamuzi hawakuja kwa pendekezo la klabu, bali kanuni inaruhusu, kamati inapoona kuna umuhimu wa kutoa waamuzi kutoka ndani itafanya hivyo, kama itateuwa kutoka nje pia inaruhusiwa.”

Waamuzi waliochaguliwa kuchezesha mechi hiyo ni Hamza El Fareq (mwamuzi wa kati), Lahsen Agaou (mwamuzi msaidizi namba moja), Hamza Massiri (mwamuzi msaidizi namba mbili) na Mustapha Kechaf (mwamuzi wa nne wa mezani) ambao wote ni raia wa Morocco.

Kanuni ya 39 ya Ligi Kuu toleo la 2025 inayozungumzia waamuzi, imefafanua jambo hilo.

Kanuni hiyo ya 39 kifungu cha 7.1, inasema: “Kamati ya Waamuzi ya TFF inaweza kupanga mwamuzi/waamuzi kutoka nje ya Tanzania kwenye Michezo ya Ligi Kuu.”

Hii itakuwa mara ya pili kwa Dabi ya Kariakoo ndani ya Ligi Kuu Bara kuamuliwa na waamuzi kutoka nje, ambapo msimu uliopita mchezo wa mwisho baina ya timu hizo uliochezwa Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, uliamuliwa na waamuzi kutoka Misri na Yanga kushinda 2-0.

Mwamuzi wa kati alikuwa Amin Mohamed Amin Omar, huku Mahmoud Ahmed Abo El Regal akiwa mwamuzi msaidizi namba moja na Samir Gamal Saad Mohamed ni mwamuzi msaidizi namba mbili, Ahmed Mahrous alikuwa mwamuzi wa nne wa mezani, hawa wote kutoka Misri, huku mtathimini waamuzi akiwa Alli Mohamed wa Somalia.

Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kuingia uwanjani, Boimanda alisema: “Mageti yatafunguliwa kuanzia saa 7 mchana, mashabiki wale wenye tiketi ndio wataruhusiwa kuingia, vinywaji havitaruhusiwa kesho.”


WASIKIE MAKOCHA

Akiuzngumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Steve Barker, alisema: “Ili kushinda mechi ya kesho tunapaswa kufunga magoli na sio rahisi, tumekuwa na muendelezo mzuri hiyo inafanya mechi hiyo kuwa ngumu kutokana na ubora wa Yanga kwenye eneo la ulinzi.

“Kila mchezaji yuko sawa na wanashauku ya kutosha japo kushinda mechi dhidi ya Yanga ni ngumu na tunaelewa tukishinda kesho itakuwa tumepunguza gepu la pointi kubaki mbili dhidi ya Yanga, naamini itakuwa mechi ngumu kwa timu zote mbili.”

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema: “Ni mashindano tofauti, tunajiamini vya kutosha na tunaamini tunaweza kucheza vizuri kesho (leo), tunaenda kucheza mechi na moja ya timu ngumu Tanzania na Afrika.”