Hiki hapa kinachoitesa Azam FC, kocha afunguka
Muktasari:
- Azam katika mechi ya raundi ya 21, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam ikifikisha pointi 43 kabla ya jana kucheza dhidi ya TRA United.
KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge amedai mbio za Ligi Kuu Bara zimekuwa ngumu zaidi katika hatua za mwisho na kilichowagharimu katika baadhi ya mechi za hivi karibuni ni kushindwa kutumia vizuri nafasi wanazotengeneza.
Azam katika mechi ya raundi ya 21, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam ikifikisha pointi 43 kabla ya jana kucheza dhidi ya TRA United.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge amesema changamoto kubwa kwa kikosi chake si kutengeneza nafasi, bali ni kushindwa kuzitumia ipasavyo wanapozipata kwa kufunga mabao, jambo ambalo anaendelea kulifanyia kazi.
“Ligi ni ngumu sana hasa hizi mechi za mwisho za kumalizia msimu, lakini tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia,” amesema Ibenge.
Kocha huyo ameongeza, wakati wakijiandaa na michezo yao ya ugenini, suala la umakini mbele ya lango ni moja ya maeneo wanayopaswa kulifanyia kazi kwa haraka ili kuendelea kupata matokeo chanya.
“Tunapokwenda ugenini lazima tufanyie kazi hilo, tunahitaji ushindi ili kuendelea kuzikimbiza Simba na Yanga, unajua unapocheza na timu pinzani kwake anakuwa na nafasi ya kushinda kutokana na uzoefu hasa wa viwanja,” amesema.
Mbali na hilo, Ibenge pia ameizungumzia safu yake ya ulinzi akisisitiza umuhimu wa kupunguza makosa yanayoweza kuwagharimu, licha ya kuwapongeza baadhi ya wachezaji kwa kujituma.
“Tunapaswa kupunguza makosa kwenye ulinzi. Nimempongeza Foba (Zuber) kwa juhudi zake, lakini penalti ile ingeweza kutugharimu kwa kuruhusu bao la kusawazisha. Makosa kama hayo hayatakiwi kuendelea,” amesema Ibenge.