Kocha Mafunzo atimkia Raskazone
Muktasari:
- Kocha huyo aliliambia Mwanaspoti sababu ya kusitisha mkataba na timu hiyo ni baada ya viongozi kusajili wachezaji 10 bila kumshirikisha.
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Mafunzo, Salum Haji Salum amejiunga rasmi na Raskazone iliyopanda daraja msimu huu wa Ligi Kuu Zanzibar.
Kocha huyo aliliambia Mwanaspoti sababu ya kusitisha mkataba na timu hiyo ni baada ya viongozi kusajili wachezaji 10 bila kumshirikisha.
Hivyo, amesema hakupendezwa na hicho na ndio sababu ya kufanya uamuzi wa kuwa mbali na timu ili lisije kutokea jengine zaidi ya hilo.
Amesema kwa sasa yupo Raskazone na ameshaamalizana nao tayari na ameshaanza kuinoa timu hiyo kwa ajili ya msimu mpya.
"Kwa sasa nimejiunga na Raskazone na sababu kubwa ambayo ilinifanya kuachana Mafunzo ni baada ya kusajili wachezaji 10 bila kunishirikisha," amesema
Alieleza timu hiyo inafanya mazoezi kwenye uwanja uliopo Kiembe Samaki na anaamini msimu wa 2026-2027 utakuwa bora zaidi upande wao na inaendelea kukamilisha usajili na kurekebisha maeneo ambayo hayapo vizuri kwani msimu huu utakuwa mgumu zaidi kwa timu zote.
Amesema kama ilivyomaliza Ligi Daraja la kwanza kwa kufanya vizuri, itaendelea vivyo hivyo kwa Ligi Kuu Zanzibar na inaendelea na mazoezi, hivyo mashabiki watarajie mazuri kutoka kwake.