Prime
Mastaa Simba waingilia kati presha ya Doumbia
WAKATI presha ikiwa juu kwa mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Doumbia ya kutokufunga mabao katika mechi za Ligi Kuu alizocheza, mastaa wenzake wa timu hiyo wameamua kuingilia kati suala hilo.
Rekodi zinaonyesha, msimu uliopita wa 2025/26 Doumbia mwenye umri wa miaka 19 akiwa na AS Korofina aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Mali akiwa na mabao 17, asisti tano, jambo ambalo wachezaji wenzake wa Simba wameamua kumlinda kwa kila hali wakisubiri muda ufike wa yeye kucheka na nyavu.
Staa huyo ameingia kwenye presha baada ya mashabiki kugawanyika, wengine wakiendelea kumuunga na mkono na wengine wakiamini kuwa Simba ilikosea kumsajili.
Beki wa kulia wa Simba Nathaniel Chilambo aliyejiunga na timu hiyo Julai 20, 2026, amesema Doumbia amekutana na presha kubwa, kama wachezaji wanajitahidi kumlinda kuhakikisha hawamtoi mchezoni kama ambavyo inaonekana presha kubwa kupitia mitandao ya kijamii.
“Kama mmefuatilia mechi za Simba hakuna mchezaji aliyeacha kumpa pasi Doumbia, hata akikosa mabao tunampa moyo ili atulie arejee mchezoni, kwani ni mfungaji mzuri na takwimu zake za timu aliyotokea zinaonyesha hilo,” amesema Chilambo na kuongeza;
“Doumbia akifungua akaunti ya mabao kila kitu kitabadilika, ila kwa sasa anakumbana na presha tofauti na timu alikotokea, ndiyo maana anapaswa kuizoea kwa haraka na sisi tukiendelea kumpa nguvu.”
Ukiachana na Chilambo, staa mwingine aliyemkingia kifua Doumbia ni kipa wa timu hiyo, Yakoub Suleiman ambaye alisajiliwa na Simba 2024/25 akitokea JKT Tanzania ambako alimaliza na cleansheets nane na uliyopita kabla hajaumia alikuwa na mbili, amesema ni kipindi cha mpito kwa mshambuliaji huyo lakini atakaa sawa.
“Mimi ni mfano halisi kwake, wakati najiunga na Simba nilikutana na presha kubwa, iliyonifanya nijiweke kando na mitandao ya kijamii ili nisifuatilie kila kitu kilichokuwa kinazungumzwa kuhusu mimi,” amesema Yakoub na kuongeza;
“Baada ya muda nilijifunza kuendana na presha, nikatulia na kufanya kazi kama kawaida, ndiyo maana nikipata muda wa kupiga stori na Doumbia huwa namwambia ajitahidi kutulia ni mshambuliaji mzuri, akianza kufunga upepo utabadilika.”
Kwa upande wa kiungo mshambuliaji Morice Abraham ambaye msimu huu amekuwa akitumika kwenye mechi nyingi za Simba amesema presha nyingine aliyokutana nayo Doumbia ni uwepo wa mawinga wanaofanya vizuri ambao ni Elie Mpanzu na Libasse Gueye na Anicet Oura, jambo ambalo linamfanya atumie nguvu kubwa na kujikuta anakosa mabao.
Gueye msimu uliopita alimaliza na mabao saba, 2026/27 hadi sasa ana bao moja, asisti tano, wakati Mpanzu alikuwa na mabao saba na kinara wa asisti 10 na sasa ana bao moja, jambo ambalo Morice amesisitiza linampa chalenji ya kupambana zaidi.
“Ni mshambuliaji mzuri ni suala la muda kukaa katika mfumo wa kucheka na nyavu, ndiyo maana kila mchezaji wa Simba anatamani kumuona Doumbia akifanya kitu kikubwa,” amesema.
Mbali na wachezaji wenzake kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Steve Barker amesema anatambua Doumbia ni mchezaji mzuri, ili kumjenga kisaikolojia asijione amepotea anampa nafasi ya kucheza mara kwa mara, anaamini akifunga atatulia: “Akianza kufunga atafunga sana, atakuwa amepata utulivu, natambua ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga ndiyo maana namtumia hata kama hajaanza kufunga mabao kwa sasa.”