Mtihani wa Polisi kwa KVZ Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- KVZ itakutana na Polisi kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja, Jumamosi ya Agosti 29 kuanzia saa 10:00 jioni, huku KMKM ikikabiliana na Kipanga Uwanja wa Mao A, Unguja, siku hiyo hiyo na muda huo.
LIGI Kuu Zanzibar msimu wa 2026-2027 inatarajiwa kuanza Agosti 29, 2026 kwa bingwa mtetezi KVZ kuanza safari ya kutetea taji dhidi ya Polisi, wakati mabingwa wa Kombe la FA, KMKM, watafungua kampeni yao dhidi ya Kipanga.
KVZ itakutana na Polisi kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja, Jumamosi ya Agosti 29 kuanzia saa 10:00 jioni, huku KMKM ikikabiliana na Kipanga Uwanja wa Mao A, Unguja, siku hiyo hiyo na muda huo.
Polisi ina mtihani wa kuanza msimu kwa kucheza dhidi ya bingwa mtetezi, huku yenyewe msimu uliopita ikimaliza nafasi ya 11 ikikusanya pointi 40 baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 12, sare tano na kupoteza 13.
Kwa KMKM, mechi yake dhidi ya Kipanga, zinakutana timu ambazo msimu uliopita zilipishana nafasi moja, huku zote zikiwa na pointi 44. Tofauti ya mabao ndiyo iliiweka KMKM nafasi ya saba, huku Kipanga ikiwa ya nane.
Katika raundi ya kwanza, jumla ya mechi nane imepangwa kuchezwa katika siku tatu, huku mechi nyingine itakayopigwa Agosti 29, FSC itaikaribisha Raskazone Uwanja wa Gombani, Pemba.
Michezo mingine ya raundi hiyo itakayopigwa Agosti 30, ni JKU vs Mlandege (Uwanja wa Mao A), Zimamoto vs Mafunzo (Pangatupu) na Mwenge vs Muembe Makumbi (Gombani), kisha Agosti 31 ni Black Sailor vs Chipukizi (Mao A) na Uhamiaji vs Wembe (Mao B).
Mbali na ushindani wa timu, msimu huu unaanza ukiwa na ongezeko la viwanja vinavyotumika kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu Zanzibar.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, viwanja viwili vipya vimeongezwa ukilinganisha na msimu uliopita ambapo viwanja vitatu vilitumika ambavyo ni Mao A na Mao B vilivyopo Unguja na Gombani kisiwani Pemba. Viwanja vilivyoongezwa ni Pangatupu na Kinyikani, vyote vikiwa Unguja.
Msimu mpya unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku KVZ ikiwa na jukumu la kutetea taji lake na KMKM ikilenga kuendeleza kasi baada ya kutwaa Kombe la FA.