Prime
Mzize ashtua Yanga, mtaalamu aanika faili zima
LIGI Kuu Bara imesimama hadi Januari 21 mwakani, pia michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga inashiriki ikiwa Kundi B nayo imesimama hadi mwakani, huku mabosi wa klabu hiyo wakikuna vichwa kuhusu straika na mfungaji bora wa klabu hiyo, Clement Mzize aliye majeruhi.
Wakati Yanga ikijiandaa kuvuka Bahari ya Hindi kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoanza rasmi Jumapili hii, faili la afya ya Mzize limewekwa hadharani na Yanga iliyokuwa ikimpigia hesabu kurudi mapema uwanjani mambo sivyo.
Hii ni kutokana na ripoti ya mtaalamu anayeshughulikia ili kumrejesha uwanjani baada ya upasuaji kufichua, mshambuliaji huyo hawezi kuonekana akiitumikia Yanga hadi apone kabisa na hilo linatarajiwa kuwa Februari mwakani, timu hiyo ikiwa imeshacheza mechi mbili za CAF dhidi ya Al Ahly.
Yanga itacheza na Al Ahly katika mechi hizo mfululizo zitakazopigwa kati ya Januari 23 na 30 kisha kuifuata FAR Rabat ya Morocco Februari 6 na kumalizia dhidi ya JS Kabylie ya Algeria visiwani Zanzibar Februari 13, hali inayotoa picha huenda Mzize akazikosa mechi zote hizo.
Ipo hivi. Mzize aliyeumia katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola iliyopigwa Septemba 19 mwaka huu na Yanga kushinda mabao 3-0 kabla ya kufanyiwa upasuaji Novemba.
Ilielezwa awali jeraha hilo lingemweka nje ya uwanjani kwa muda wa wiki kati ya 8-10 na licha ya sasa kuonekana akijifua kwa mazoezi na wenzake, lakini ukweli ni jamaa atakuwa nje kwa muda mrefu hadi Februari.
Daktari wa viungo wa Yanga, Youssef Ammar aliliambia Mwanaspoti, kihesabu huenda Mzize atarejea uwanjani mapema Februari kutokana na hali yake kwa sasa kuendelea kuimarika.
Youssef alisema mshambuliaji huyo kwa sasa ameanza mazoezi akiwa chini yake na anamtazama kwa ukaribu kabla ya kumpeleka kwa kocha wa viungo wa klabu hiyo na mambo yakiwa mazuri atarudi uwanjani.
“Ni kweli Mzize sasa yupo chini yangu kwa ajili ya kumtazamia nafurahi anaendelea vizuri na mara baada ya kukamilisha programu yangu atatakiwa kuwa chini ya kocha wa viungo, hivyo nafikiri anahitaji muda zaidi kukaa sawa,” alisema Ammar na kuongeza;
“Hatutamruhusu kurudi haraka katika mechi za ushindani kutokana na mahitaji ya benchi la ufundi, tunachokifanya ni kuhakikisha mchezaji anarudi katika hali ya ubora ili aendeleze kasi yake aliyomaliza nayo msimu uliopita.”
Youssef alisema hana uhakika siku gani hasa Mzize atarejea uwanjani, lakini anafikiri ni katika miezi miwili ijayo, huku akiahidi atarudi akiwa na moto ule ule wa zamani uliomfanya amalize msimu uliopita akiwa kinara wa mabao wa klabu akifunga 14 katika Ligi Kuu Bara.
“Daktari na uongozi unataka kuona Mzize anarudi kwa kuzingatia mahitaji na ripoti ya daktari izingatiwe asiharakishwe ili tu timu inufaike naye na baadae wakamrudisha katika changamoto ya majeraha,” alisema Ammar na kuongeza;
“Kutokana na hilo ni mambo mengi yanafanyika kwa utaratibu lengo ni kuona mchezaji huyo anarejea akiwa katika hali ya utimamu na ubora kama alionao misimu miwili nyuma na hilo linawezekana kama yeye pia atazingatia maelekezo anayopewa madaktari wanaomtazama.”
Kutokana na ripoti hiyo, ni wazi Kocha Pedro Goncalves atalazimika kuendelea kujipanga kivyake kwa kuwatumia washambuliaji alionao ili kupata matokeo mazuri katika mechi zilizopo mbele yao, zikiwamo za Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Mapinduzi 2026 inayoanza Jumapili.
Yanga inaenda Mapinduzi ambako itaanza mechi zake kwa kuvaana na KVZ Janurai 4 kabla Januari 6 kumalizana na TRA United ikimtegemea Andy Boyeli, Celestin Ecua na Offen Chikola kwa eneo la ushambuliaji kwa vile Price Dube yupo AFCON 2025.
Inaelezwa tayari kocha Pedro ameshatoa pendekezo la kutafutiwa straika mpya kwa ajili ya kuwahi mechi zilizosalia za CAF ikiwa ipo nafasi ya pili kwa sasa katika Kundi B ikuvuna pointi nne baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya FAR Rabat kisha kutoka suluhu na JS Kabylie ugenini.