Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

OKELLO: Silaha hatari ndani ya kikosi cha Yanga


NI wazi kiwango alichokionyesha kiungo mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello kwenye mechi za hivi karibuni kinaenda kuwapa chalenji mabeki wa Simba.


Ni mchezaji ambaye japo hana takwimu nzuri za kufunga lakini amekuwa na mchango mkubwa kwenye ubunifu wa mashambulizi na kasi yake ya kupeleka mipira mbele imekuwa ikileta madhara kwa wapinzani.


Katika mechi saba za hivi karibuni za Ligi Kuu Bara, Okello ameonyesha ubora wa hali ya juu, akicheza kwa kujiamini na uwezo wa kuusoma mchezo. Hii ndiyo silaha kubwa ambayo inaweza kubadilisha mchezo kama itatumika vizuri.

Kwanza Okello ana sifa ya kiungo anayependa kucheza kati ya mistari. Mara nyingi hujipenyeza kati ya viungo na mabeki wa timu pinzani, eneo ambalo ni hatari sana kwa mabeki kwa sababu linawafanya washindwe kuamua kwa haraka wamfuate au wabaki kwenye nafasi zao.

Katika dabi hii mabeki wa Simba kama Rushine De Reuck, Ismail Toure, Nickson Kibabage na Shomari Kapombe watakuwa na changamoto ya kufanya maamuzi ya haraka na kumdhibiti Okello kila anapopokea mipira katika maeneo hayo.

Pili, uwezo wa Okello katika kupiga pasi za mwisho ni jambo linaloweza kubadili matokeo ya mchezo. Akiwa na asisti sita katika mechi 13 za ligi, inaonyesha wazi kwamba yeye sio mfungaji tu bali ni mbunifu wa nafasi. Hapa ndipo hatari ilipo kwa Simba. Mabeki wanaweza kujikita kumzuia Okello kupiga mashuti, lakini hatari kubwa ipo kwenye pasi zake za ghafla zinazoweza kuwatoa kwenye nafasi na kuwaacha washambuliaji wa Yanga wakiwa uso kwa uso na kipa.

Katika mfumo wa Yanga 4-2-3-1, Okello hutumika kama kiungo anayezunguka karibu uwanja mzima wa mbele. Hii ina maana kwamba hata kama atadhibitiwa katikati, anaweza kuhamia pembeni au kushuka chini kuchukua mpira na kuanzisha mashambulizi. Hali hii inawalazimisha mabeki wa Simba kuwa na mawasiliano muda wote, jambo ambalo likikosekana linaweza kuigharimu timu hiyo.

Changamoto nyingine ambayo Okello anaweza kuleta ni uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali. Mabeki wa Simba wakimpa nafasi ya kumiliki mpira bila presha, wanaweza kujikuta wakikabiliwa na mashuti ya kushtukiza ambayo yanaweza kubadilisha mchezo. Kwa upande wa uamuzi, Okello si kiungo anayependa kukaa na mpira kwa muda mrefu huamua kwa haraka ama apige pasi, akokoe au apige shuti.

Uamuzi huo wa haraka unaifanya safu ya ulinzi ya timu pinzani kushindwa kujipanga vizuri. Dabi ya Kariakoo mara nyingi huwa na presha kubwa, lakini mchezaji mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa haraka kama Okello anaweza kuigeuza presha hiyo kuwa faida kwa timu.

Hata hivyo, Simba wana silaha za kukabiliana naye. Moja ya mbinu wanazoweza kutumia ni kumwekea ulinzi wa karibu kila anapokuwa na mpira. Lakini hili lina changamoto yake kumfungia Okello kunaweza kufungua nafasi kwa viungo wengine wa Yanga kama Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli. Pia viungo wa Simba watapaswa kukata mawasiliano kati ya Okello na washambuliaji wa Yanga. Hii ina maana viungo wa ulinzi wa Simba lazima wafanye kazi kubwa ya kuzuia pasi zisifikie maeneo hatari. Bila kufanya hivyo, hata kama mabeki watakuwa imara, watakuwa wanakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara.

Kitu kingine kinachomfanya Okello kuwa hatari ni uwezo wake wa kucheza katika mechi kubwa. Dabi ya Kariakoo si mechi ya kawaida ni mchezo wenye presha, ushindani mkubwa na mazingira yanayohitaji utulivu wa hali ya juu. Kwa kiwango anachoonyesha hivi sasa, anaonekana kuwa mchezaji anayeweza kubeba jukumu hilo na kuleta tofauti.

Dabi hii inaweza kuamuliwa na ubunifu wa katikati ya uwanja, na hapa kulingana na takwimu jina la Okello linapokuja kwa uzito mkubwa. Ikiwa Simba watashindwa kumdhibiti, basi watakuwa wamefungua mlango wa hatari kwa safu yao ya ulinzi. Lakini wakifanikiwa kumzuia, watakuwa wamepunguza kwa kiasi kikubwa makali ya Yanga.


WASIKIE WENYEWE

Akizungumzia kiwango chake, Okello anasema: “Kwanza nawashukuru wachezaji wenzangu kwa sapoti yao na naamini tukishirikiana kwa pamoja tutafanikisha malengo ya timu.”

Mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube anasema: “Ni mchezaji mzuri na niliwahi kusema siku akija kufunga kila mmoja ataona ubora wake kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kushambulia na kutusaidia.”