Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shalulile rasmi atua Yanga

Muktasari:

  • Shalulile anajiunga na mabingwa hao wa Tanzania baada ya kuhitimisha safari yake ya miaka sita ndani ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

KLABU ya Yanga, imepata nguvu mpya katika safu yake ya ushambuliaji baada ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Namibia, Peter Shalulile.

Shalulile anajiunga na mabingwa hao wa Tanzania baada ya kuhitimisha safari yake ya miaka sita ndani ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Mshambuliaji huyo anatua Jangwani akiwa na rekodi ya kuvutia baada ya kufunga mabao 136 katika mashindano yote akiwa na Sundowns, huku akiisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mbalimbali ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), African Football League na ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini mara tano.

Mbali na mafanikio hayo, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33, aliifungia Sundowns mabao 20 katika Ligi ya Mabingwa Afrika na alibaki na tofauti ya mabao nane pekee kufikisha mabao 100 katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini, jambo linalodhihirisha ubora wake mbele ya lango.

Usajili huo unamrejesha Shalulile kufanya kazi tena na kocha Manqoba Mngqithi, ambaye kwa sasa anaiongoza Yanga. Wawili hao waliwahi kushirikiana kwa mafanikio makubwa ndani ya Mamelodi Sundowns, ambapo Mngqithi alikuwa sehemu muhimu ya benchi la ufundi lililomlea na kumfanya Shalulile kuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi barani Afrika.

Kuungana tena kwa nyota huyo na Mngqithi kunatajwa kuwa moja ya sababu zilizomshawishi kuchagua Yanga, huku kocha huyo akiamini uzoefu, uwezo wa kufunga na uelewa wa mfumo wake wa mchezo vitakuwa silaha muhimu katika harakati za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa usajili huo, Yanga inaongeza mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa, jambo linaloongeza matarajio ya mashabiki kuona safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ikiwa na makali zaidi msimu ujao.

Kabla ya Shalulile, Yanga ilitambulisha nyota watatu wa kimataifa ambao ni mshambuliaji Cheikh Ibrahima Toure raia wa Ufaransa mwenye asili ya Senegal aliyetokea Al Jabalain FC ya Saudia, winga Housseine Zakouani ambaye ni raia wa Comoro aliyezaliwa Ufaransa akitokea Al Zulfi ya Saudi Arabia na wingina mwingine Mzambia, Albert Kangwanda kutoka Red Arrows ya kwao.

Utambulisho wa wachezaji hao, unafanya Yanga hadi sasa kuwaweka hadharani nyota wapya kumu wakiwemo wazawa sita ambao ni Juma Issa Abushiri kutoka Fountain Gate, Hussein Mihambo (Mashujaa), Abdulnasir Muhamed (Mashujaa), Mohamed Mussa (Mashujaa), Erick Mwijage (Mashujaa) na Suleiman Mbarouk maarufu Mpemba D aliyekuwa JKU.