Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shilingi ilivyosimama Kariakoo Derby

MACHO ya mashabiki wa soka kwa sasa nchini, yanaelekezwa Mei 3, 2026, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, jijini Dar es Salaam, wakati watani wa jadi Simba na Yanga watakapokutana katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu.

Timu hizo zinakutana zikiwa zimepita siku nne tangu zilipokutana Aprili 29, 2026, Zanzibar, katika fainali ya Kombe la Muungano, lililoshuhudiwa Simba ikitwaa taji hilo la saba kwake tangu mwaka 1982, baada ya kushinda bao 1-0.

Bao pekee la Simba lilifungwa na nyota wa kikosi hicho, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, dakika ya 120+4, kwa mkwaju wa penalti, iliyotokana na kiungo, Clatous Chota Chama ‘Triple C kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari na nyota wa Yanga, Edmund John.

Mechi hiyo ya ‘Kariakoo Derby’ ilishindwa kuamuliwa mbabe kwa dakika 90, baada ya kushindwa kutambiana na kutoka suluhu kisha kuongezwa dakika 30 za nyongeza, zilizoinufaisha Simba na kuivua Yanga ubingwa iliyotwaa mwaka 2025.

Yanga iliingia na kumbukumbu nzuri baada ya kutwaa taji hilo la Kombe la Muungano mwaka 2025, baada ya kuifunga JKU FC bao 1-0 lililofungwa na Maxi Nzengeli,katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, Mei 1, 2025.

Timu hizo zinakutana tena Mei 3, 2026 ikiwa ni raundi ya pili ya Ligi Kuu baada ya mzunguko wa kwanza zilipokutana Machi 1, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, kushindwa kutambiana na kutoka pia suluhu (0-0). 

Sasa wakati timu hizo zikitarajia tena kukutana katika mechi hiyo ya raundi ya pili, rekodi zinaonyesha zinaibeba zaidi Yanga inapocheza mwezi Mei, huku kwa upande wa Simba ikibebwa siku ya Jumapili, jambo linaloonyesha shilingi imesimama.


REKODI ZA MWEZI MEI

Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 1965, timu hizo zimekutana mara saba katika mechi za Ligi Kuu Bara zilizochezwa kwa mwezi Mei, ambapo kati ya hizo Yanga ni mbabe zaidi, baada ya kushinda tatu, ikitoka sare mbili, huku Simba ikishinda miwili.

Mechi ya kwanza kwa timu hizo kukutana Mei tangu 1965, ilipigwa Jumapili ya Mei 19, 1985, ambapo zilitoka sare ya bao 1-1, Yanga ikifunga kupitia kwa Omar Hussein dakika ya sita, kisha Mohammed Bob Chopa, akaisawazishia Simba dakika ya 30.

Katika tatu ilizoshinda Yanga ni ya Mei 18, 1991, iliposhinda bao 1-0, lililofungwa dakika ya saba na Said Sued ‘Scud’, huku ya pili ni ushindi wa mabao 3-1, Mei 1, 1999, ikiwa ni mechi ya 62, kwa timu hizo kukutana katika Ligi tangu 1965.

Katika mechi hiyo ya Mei 1, 1999, mabao ya Yanga yalifungwa na Idd Moshi dakika ya 59, Kalimangonga Ongala dakika ya 64 na Salvatory Edward dakika ya 70, huku lile la kufuatia machozi kwa Simba likifungwa na nyota, Juma Amir, dakika ya 12.

Mechi ya tatu kwa Yanga kushinda dhidi ya Simba katika Ligi Kuu, ni iliyopigwa Jumamosi ya Mei 18, 2013, ambapo kikosi hicho kilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Didier Kavumbagu dakika ya 5 na Hamis Kiiza, maarufu ‘Diego’ dakika ya 62. 

 Kwa upande wa mechi mbili za Simba ilizoshinda ni ya bao 1-0 la Mavumbi Omari dakika ya sita, Mei 26, 1990 na ile ya ushindi pia mzuri wa mabao 5-0, Mei 6, 2012 yaliyofungwa na Mganda Emmanuel Okwi aliyefunga mawili dakika ya 1 na 65.

Mabao mengine katika mechi hiyo iliyoteka hisia kubwa za mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi yalifungwa na Patrick Mafisango dakika ya 58, Juma Kaseja dakika ya 69 na Felix Sunzu dakika ya 74, ambapo nyota hao walifunga kwa penalti.

Mechi mbili za sare ni za bao 1-1, Mei 19, 1985, Yanga ikitangulia kufunga kupitia kwa Omar Hussein dakika ya 6 kisha Mohammed Bob Chopa akaisawazishia Simba dakika ya 30 na ile pia iliyoisha kwa suluhu ya (0-0), iliyopigwa Mei 21, 1989.

Katika mechi saba ambazo timu hizo zimekutana mwezi Mei katika Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965, yamefungwa jumla ya mabao 15, ambapo Simba inaongoza kwa kufunga mengi zaidi, ikifanya hivyo, mara nane, huku kwa upande ya Yanga ikifunga saba.


REKODI YA JUMAPILI

Mechi ya Mei 3, 2026, itakuwa ni ya 38, kwa timu hizo kucheza siku ya Jumapili tangu rasmi mwaka 1965, ambapo kati ya 37 iliyopita, Simba imeshinda tisa, Yanga ikishinda saba, huku 21, iliyobakia ikimalizika kwa sare kwa maana hakuna mbabe.

Katika mechi 37 za Kariakoo Derby kati ya miamba hiyo ya soka hapa nchini iliyochezwa siku ya Jumapili yamefungwa mabao 68 tangu 1965 ambapo Simba inaongoza kwa kufunga mengi zaidi ikiwa na 36, huku Yanga ikifunga 32.

Hata hivyo, Yanga ndio timu ya kwanza kushinda mechi ya ‘Kariakoo Derby’ iliyopigwa Jumapili baada ya kuifunga Simba bao 1-0 lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho kwa wakati huo, Leonard Chitete, pambano lililopigwa Juni 18, 1972.

Katika mechi 37, Simba ndio timu pekee iliyokuwa mwenyeji mara nyingi zaidi (21) huku Yanga ikiwa mara (16), ambapo mara ya kwanza kukutana katika Ligi Kuu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ilikuwa ni Oktoba 26, 2008.

Mechi hiyo ambayo ni ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, iliyopigwa Oktoba 26, 2008, Yanga iliifunga Simba kwa bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Ben Mwalala, dakika ya 15.


SIKU 542 KWA YANGA

Moja ya jambo linalosubiriwa kwa hamu, ni kuona endapo Simba itaivunja rekodi ya Yanga ya kucheza bila ya kupoteza mechi ya Ligi Kuu Bara, tangu mabingwa hao watetezi mara ya mwisho walipochapwa na TRA United kwa mabao 3-1, Novemba 7, 2024.

Tangu mara ya mwisho Yanga ilipochapwa na Tabora United (sasa TRA United) mabao 3-1, Novemba 7, 2024 imefikisha mechi 39 za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza ambapo kati ya hizo imeshinda 33 na kutoka sare sita iliyobakia. Katika mechi hizo 39, safu ya ushambuliaji ya Yanga imefunga mabao 113 na kuruhusu tisa, ambapo Mei 3, 2026 inatimiza siku 542 za kucheza bila kupoteza ambazo ni sawa na mwaka mmoja, miezi mitano na siku 26 au miezi 17 na siku 26.

SIMBA KUVUNJA UTEJA?

Baada ya Simba kuifunga Yanga bao 1-0, Aprili 29, 2026 na kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano, swali kwa sasa ni itaweza kuvunja uteja au itaendeleza rekodi mbovu ya kutoshinda katika Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho Aprili 16, 2023.

Mara ya mwisho kwa Simba kuifunga Yanga katika Ligi Kuu ilikuwa ni ushindi wa mabao 2-0, Aprili 16, 2023 yaliyofungwa na waliokuwa nyota wa kikosi hicho Henock Inonga Baka ‘Varane’ aliyefunga dakika ya 2 tu na Kibu Denis katika dakika ya 32.

Mechi hiyo iliyokuwa ya 110 ya Ligi Kuu Bara kwa timu hizo kukutana tangu mwaka 1965 ilikuwa ya mwisho kwa kikosi hicho cha Simba kuifunga Yanga, kwani baada ya hapo, imeshindwa kutamba na kushuhudia ikichapwa mara nne na kutoka sare moja.