Simba Queens ina rekodi nzuri kwa Yanga
Muktasari:
- Timu hiyo msimu huu imekusanya pointi 10 dhidi ya vigogo Yanga Princess na iliifunga jumla ya mabao 4-1 nyumbani na ugenini na kubeba pointi sita kisha ikachukua pointi nne dhidi ya mabingwa watetezi JKT Queens.
USHINDI wa mabao 2-1 ilioupata Simba Queens dhidi ya JKT Queens juzi katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, umeendelea kuthibitisha ubabe wa timu hiyo kwenye moja ya dabi kubwa zaidi ya soka la wanawake nchini huku ukiiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake(WPL) msimu huu.
Timu hiyo msimu huu imekusanya pointi 10 dhidi ya vigogo Yanga Princess na iliifunga jumla ya mabao 4-1 nyumbani na ugenini na kubeba pointi sita kisha ikachukua pointi nne dhidi ya mabingwa watetezi JKT Queens.
Mbali na pointi tatu zilizoifanya kufikisha pointi 52 kileleni mwa msimamo, takwimu zinaonyesha timu hiyo imekuwa na rekodi nzuri inapokutana na JKT Queens, hasa kwenye Uwanja wa Isamuhyo ambao umeonekana kuwa uwanja rafiki kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Tangu mwaka 2019, timu hizo zimekutana mara sita katika uwanja huo na Simba Queens haijawahi kupoteza mechi hata moja. Katika mechi hizo sita, Simba imeshinda tano huku sare moja pekee mwaka 2023.
Rekodi hiyo ilianza Desemba 8, 2019 kwa Simba Queens kushinda bao 1-0 kabla ya Februari 28, 2021 kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao 4-0. Mei 17, 2022 ilishinda tena 1-0, Machi 9, 2023 wakatoka sare ya 1-1, huku Mei 7, 2025 dabi hiyo ikitoa mvua ya mabao baada ya Simba kushinda 4-3 na juzi Mei 23 ikishinda kwa mabao 2-1.
Kwa jumla, timu hizo zimekutana mara 20 tangu mwaka 2017 na Simba Queens imeshinda mara tisa dhidi ya nane za JKT Queens huku mechi tatu zikimalizika kwa sare.
Takwimu bado zinaibeba Simba hadi na kwenye mabao timu hiyo ikionekana kuwa na safu bora ya ushambuliaji, ikifunga mabao 30 kwenye mechi hizo 20 walizokutana huku JKT ikifunga 25.
Takwimu pia zinaonyesha katika mechi walizokutana Simba iliwahi kuwafunga wanajeshi hao wa kike kipigo kikubwa cha mabao 7-0, Februari 2022 kipigo ambacho kimebaki kuwa historia na hakijavunjwa hadi sasa.
Katika upande wa wafungaji, mshambuliaji wa zamani wa Simba Queens, Opah Clement ambaye kwa sasa anakipiga SD Eibar ndiye kinara wa mabao kwenye dabi hiyo akiwa amefunga mabao matano, akifuatiwa na Jentrix Shikangwa mwenye manne. Kwa upande wa JKT Queens, Asha Mwalala ndiye anayeshikilia rekodi ya mabao mengi zaidi dhidi ya Simba Queens akiwa amefunga mara tatu.
Ikumbukwe timu zote mbili zimebeba ubingwa mara nne kila mmoja tangu Ligi ya Wanawake ianze kuchezwa mwaka 2016 na Mlandizi Queens iliandika historia ya kuwa bingwa wa kwanza.
NJIA ILICHONGWA KWA YANGA
Kama Simba itachukua ubingwa msimu huu basi mafanikio yao makubwa yamechangiwa na Yanga Princess ambayo imekubali kichapo ikiwa nyumbani na ugenini.
Haijabahatisha kutokana na muendelezo mzuri na Simba kwenye ligi tangu msimu umeanza na kwenye mechi 18 ikitoka sare moja na kushinda mechi 17.
Hata hivyo, huu siyo msimu wa kwanza kwa wananchi hao wa kike kushindwa kufurukuta mbele ya Mnyama ambaye amekuwa na kiwango bora kila akikutana na mtani wake.
Takwimu zinaonyesha tangu mwaka 2019 timu hizo zimekutana mara 19 katika mashindano mbalimbali, huku Simba Queens ikishinda mara 13, Yanga Princess ikishinda mara tatu na sare tatu.
Kwenye mechi za ligi wamekutana mara 15 Simba ikishinda mara 11 ikipoteza mechi mbili na kutoka sare mbili.
Mbali na rekodi hiyo, Simba pia imekuwa na uimara mkubwa wa safu ya ulinzi. Msimu huu timu hiyo ilikuwa imeruhusu mabao manne pekee katika mechi 18 za ligi, rekodi iliyoifanya kuwa timu yenye ulinzi bora zaidi WPL.
Mshambuliaji Jentrix Shikangwa anashikilia rekodi ya kuwafunga Yanga mara nyingi akiweka kambani mabao 11 tangu alipojiunga na Simba msimu wa 2022/23, Yanga aliifunga mara saba sawa na Opah Clement huku kinara akiwa Mwanahamisi Omary anayekipiga Tausi FC mwenye mabao 10. Kwa JKT ameifunga mabao manne.
Simba Queens pia inabeba historia ya ushindi mkubwa zaidi kwenye dabi hiyo baada ya kuichapa Yanga Princess mabao 5-1 mwaka 2020.
Ingawa Yanga Princess imeonyesha maendeleo makubwa misimu ya hivi karibuni na kuendelea kuwa mshindani wa karibu kwenye mbio za ubingwa, takwimu zinaonyesha Simba Queens bado inaonekana kuwa na uzoefu mkubwa zaidi wa mechi za dabi na uwezo wa kupata matokeo katika michezo mikubwa.
MSIKIE KOCHA
Kaimu kocha mkuu wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi' amesema "Hadi sasa malengo ya timu yamefikia asilimia kubwa tuna imani tutafanya vizuri kwenye mechi zilizosalia na ndipo ilipo fokasi yetu kwa sasa."