Susan ajipanga kuwashangaza wanaume African Rally Championship
Muktasari:
- Susan Muwonge kutoka nchini Uganda, amekuwa kivutio kwenye mashindano hayo yaliyozinduliwa leo Oktoba 2, 2026 na kilele chake ni Oktoba 4, 2026 kwenye shamba la miti la TFS, amesema amefurahi kuwa mshiriki na tayari ameshajiandaa kushindana na madereva wanaume.
MWANAMKE pekee Afrika anayeshiriki mashindano ya African Rally Championship 2026, Susan Muwonge, amesema amejiandaa kikamilifu kuingia kwenye ushindani na madereva wa kiume na kuhakikisha anapata ushindi.
Akizungumza leo Oktoba 2, 2026 katika mkutano na waandishi wa habari, Susan ambaye amekuwa kivutio kwenye mashindano hayo amesema amefurahi kuwa mshiriki na tayari ameshajiandaa kwani ameshaisoma njia vizuri.
Susan amesema ushiriki wake kama mwanamke pekee ambaye ni dereva, inampa faraja na kuona mashindano hayo sio tu yanawahusu wanaume pekee bali hata wanawake wanayo nafasi ya kushiriki.
"Nafurahi kuwa mwanamke pekee kwenye mashindano haya, najiamini na nina ujasiri wa kutosha kwenye kushiriki," amesema Susan.
Kwa upande wake mmoja wa madereva wanaoshiriki mashindano hayo kutoka Tanzania, Kartik Valambia, amesena amejiandaa kushinda na sio kushiriki, na kwamba amepanga kumrithisha mtoto wake mchezo huo wa kuendesha magari.
Hata hivyo, Kartik amesikitishwa na kukosekana kwa wanawake wa Tanzania katika mashindano hayo akiamini kwamba wapo wengi wenye uwezo wa kushiriki mchezo huo isipokuwa ni kukosa kujiamini.
Naye dereva Karam Patel amesema mchezo huo alianza kuupenda akiwa na miaka 20 na kuanza kushiriki kwenye mashindano mbalimbali ambapo kwa sasa ana uwezo mkubwa wa kushindana na madereva wa mataifa mengine.
Gari analotumia Susan Muwonge kutoka nchini Uganda ambaye ni mwanamke pekee anayeshiriki mashindano ya magari African Rally Championship yanayofanyika mkoani Morogoro katika shamba la miti la TFS lililopo Makunganya wilaya ya Mvomero.
"Huu mchezo alicheza babu yangu, baba yangu, baba yangu mdogo na wajomba zangu, hivyo upo kwenye damu na naupenda, nimeshashiriki mashindano mbalimbali," amesema Patel.
Akizindua mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Mkwawa Group of Company, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema uwepo wa mashindano hayo yanayofanyika katika shamba la miti la TFS mkoani Morogoro yana faida ya kiuchumi kwa kuwa yamekusanya wageni kutoka nchi mbalimbali.
"Kupitia mashindano haya watu wa Manispaa ya Morogoro watafanya biashara za kila aina, nyumba za wageni zitapata wateja, wasafirishaji watapata abiria, hivyo watu watapata kipato," amesema Kilakala.
Hata hivyo, amewataka wananchi wa Manispaa ya Morogoro kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo huku akisisitiza kuchua tahadhari za kiusalama kwa kufuata maelekezo watakayopewa na watu wa usalama wakiwemo askari na waandaaji wa mashindano hayo.
Mmoja wa mashabiki wa mchezo wa magari, Aziz Msuya, amesema mchezo huo una burudani ikiwemo umahiri wa madereva katika kukata kona kali na namna magari hayo yanavyoweza kukimbia kwenye vikwazo mbalimbali kama vile milima na mabonde.
"Niwashukuru waandaaji wa mashindano haya makubwa kwa uamuzi wao wa kuyaleta hapa Morogoro, kwani mbali ya kuleta burudani lakini pia ni sehemu ya kuongeza mapato na kudumisha mahusiano mema na nchi nyingine zinazoshiriki mashindano haya," amesema Msuya.