Ushabiki wa Simba, Yanga hadi Kigali
Muktasari:
- Ushindi huo umeipa Rayon Sports pointi tatu katika mbio za kutinga nusu fainali huku ukiwa umeongeza furaha kwa mashabiki wake ambao kwa sasa wanajivunia mwanzo mzuri kuliko wapinzani wao, APR.
UKIWA Tanzania huwezi kuzungumzia ushindani wa soka bila kutaja Simba na Yanga, hali hiyo ndiyo inayoonekana pia nchini Rwanda kati ya vigogo APR na Rayon Sports, jambo lililojidhihirisha juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.
Rayon Sports iliifunga KVZ ya Zanzibar mabao 2-0 katika mchezo wa Kundi C wa Kombe la CECAFA Kagame 2026, ushindi uliowapa mashabiki wake nafasi ya kuwakejeli wapinzani wao APR, walioanza mashindano kwa kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Gor Mahia ya Kenya.
Katika kipindi cha kwanza, KVZ ilisimama imara na kufanikiwa kuzima mashambulizi ya Rayon Sports, hali iliyofanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana licha ya presha kubwa kutoka kwa wenyeji.
Mambo yalibadilika kipindi cha pili baada ya Rayon kuongeza kasi ya mashambulizi, dakika ya 69 walipata penalti iliyofungwa na Junior Kameni na kuamsha shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki waliofurika Amahoro.
Rayon haikuishia hapo. Iliendelea kulitawala lango la KVZ kabla ya Daniel Muhoza kufunga bao la pili dakika ya 82 na kuhitimisha matumaini ya wageni hao kurejea mchezoni.
Baada ya filimbi ya mwisho, mashabiki wa Rayon waliinuka kwa nyimbo na vijembe dhidi ya APR, wakikumbushia kipigo kizito walichopokea kutoka kwa Gor Mahia katika mchezo wao wa kwanza.
Mandhari hayo yalionyesha wazi kuwa ushindani kati ya APR na Rayon Sports una sura inayofanana sana na ule wa Simba na Yanga ambapo mafanikio ya upande mmoja huwa chanzo cha kejeli kwa mpinzani wake.
Ushindi huo umeipa Rayon Sports pointi tatu katika mbio za kutinga nusu fainali huku ukiwa umeongeza furaha kwa mashabiki wake ambao kwa sasa wanajivunia mwanzo mzuri kuliko wapinzani wao, APR.
‘Viking Clap’ yapigwa uwanja wa Amahoro
Wakati mashabiki wa Norway wakifahamika duniani kwa mtindo wao wa kushangilia wa ‘Viking Clap’, mashabiki wa Rayon Sports ya Rwanda nao wameonyesha utamaduni wao katika michuano ya CECAFA Kagame 2026 kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.
Kabla ya mchezo wa Kundi C dhidi ya KVZ ya Zanzibar kuanza, maelfu ya mashabiki wa Rayon Sports waliinua shamrashamra kwa kusubiri ngoma ipigwe mara mbili, kisha kupiga makofi kwa mpangilio huku wakipaza sauti “Huu...!” kwa pamoja, hali iliyotikisa uwanja mzima na kuvutia hata mashabiki wa timu pinzani.
Ushangiliaji huo uliendelea kwa dakika kadhaa kabla ya mechi na kuonyesha umoja wa mashabiki wa Rayon Sports, huku ukiwa sehemu ya burudani iliyoongeza hamasa kwa wachezaji na kuifanya Amahoro kuwa na mazingira ya kipekee.