Vita mpya ya ufungaji bora Championship
Muktasari:
- Katika vita hiyo hadi sasa, nyota wa Transit Camp, Hamdan Sarhani ndiye anayeongoza akiwa amekifungia kikosi hicho cha maafande mabao tisa, akifuatiwa kwa ukaribu na mshambuliaji wa KMC FC, Ramadhan Hashim Kalanje aliyefunga mabao manane.
WAKATI Ligi ya Championship ikiwa raundi ya nane hadi sasa, tayari vita mpya ya ufungaji bora imeanza mapema, baada ya washambuliaji wa timu mbalimbali kuchuana vikali, jambo linaloonyesha kila mmoja anajitengenezea mazingira yake mazuri.
Katika vita hiyo hadi sasa, nyota wa Transit Camp, Hamdan Sarhani ndiye anayeongoza akiwa amekifungia kikosi hicho cha maafande mabao tisa, akifuatiwa kwa ukaribu na mshambuliaji wa KMC FC, Ramadhan Hashim Kalanje aliyefunga mabao manane.
Aliyekuwa mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Coastal Union anayecheza kwa sasa Kigamboni United zamani B19 FC, Abdulkarim Segeja, anafuatia akiifungia timu hiyo mabao sita, huku kwa upande wa Abiud Mtambuka wa Mbeya Kwanza akifunga matano.
Nyota wa Mbuni FC ya jijini, Arusha, Ezekiel Zonobi amefunga mabao manne, ambayo ni sawa na Calvin Kayongo wa Bigman FC ya mjini, Tanga, huku Adam Uledi wa KMC FC na Oscar Paul wa maafande wa Tanzania Prisons wakiwa na matatu kila mmoja.
Wachezaji wengine waliofunga mabao matatu ni Zuberi Malila na Pascas Wagana wanaocheza Rhino Rangers, Gilbert Boniface (Songea United), Mussa Mpina (Mbuni FC), Ibrahim Mtonga na Ibrahim Joseph Kilali wanaoichezea KenGold ya jijini, Mbeya.