Yanga, Azam kusaka pointi tatu muhimu Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Yanga itakuwa KMC Complex kuanzia saa 12:30 baada ya kurudi njia ya ushindi ilipoichapa Singida BS kwa mabao 3-0, itaikaribisha Namungo ambayo imekosa matokeo mazuri ya ushindi kwenye mechi 13 zilizopita.
KUNA mechi mbili za muendelezo wa Ligi Kuu Bara leo ambapo dakika 90 za kwanza zitawahusu bingwa mtetezi Yanga atakayekuwa nyumbani akiikaribisha Namungo ya Lindi wakati Azam FC nayo ikiwa mwenyeji wa vibonde KMC.
Yanga itakuwa KMC Complex kuanzia saa 12:30 baada ya kurudi njia ya ushindi ilipoichapa Singida BS kwa mabao 3-0, itaikaribisha Namungo ambayo imekosa matokeo mazuri ya ushindi kwenye mechi 13 zilizopita.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo na hesabu kali ikijua kwamba kama itaangusha pointi itakuwa imezidi kuitengenezea njia Simba baada ya vijana hao wa Msimbazi kucheza jana jioni na Dodoma Jiji.
Wasiwasi pekee kwa Yanga ni juu ya kiungo wake Pacome Zouzoua ambaye alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Singida ambapo vilikuwa vinasubiriwa vipimo kujua ukubwa wa jeraha lake, ingawa inaelezwa kwamba hayakuwa majeraha makubwa.
Hata hivyo, kiungo Allan Okello ambaye yupo kwenye kiwango bora yupo sawa kuendelea kuongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga kufunga pamoja na kutengeneza mabao ambapo raia huyo wa Uganda ameshafunga mabao tisa akiwa na asisti saba ikiwa na maana kuwa amehusika kwenye mabao 16.
Yanga yenye pointi 57 kwenye ligi rekodi zinaibeba zaidi mbele ya Namungo ambapo timu hizo zimekutana kwenye michezo 12, mabingwa hao wakishinda saba, na sare tano huku wageni wakiwa hawajawahi kushinda hata mchezo mmoja.
Kwenye mechi hizo 12 Yanga imefunga jumla ya mabao 20 wakati Namungo ikifunga mabao saba pekee.
Kocha wa muda wa Yanga Abdihamid Moalin, akizungumzia mchezo huo jana amesema kila kitu kuhusu maandalizi yao kimekwenda vizuri ambapo hawataki kufanya makosa ya kurudia kuangusha pointi wkati wanautafuta ubingwa.
“Kila mmoja anajua kilichotokea kwenye mechi yetu dhidi ya Dodoma Jiji, unazungumzia takwimu, haikuwa timu ambayo imewahi kutufunga (Dodoma), lakini ikafanikiwa kufanya hivyo, tumejifunza, tunaiheshimu Namungo ina kocha mzuri na wachezaji wazuri, tunachotaka ni kuendelea kushinda,” amesema Moalin.
Namungo ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo na pointi 25 kama itapoteza mchezo dhidi ya Yanga kisha Coastal Union iliyokuwa inacheza jana nyumbani dhidi ya Mashujaa ikishinda basi itashuka mpaka nafasi ya 13 ikiingia eneo la hatari kwenye msimamo.
“Mechi hii ni muhimu sana kwetu kutokana na nafasi tuliyopo kwenye msimamo lakini hata wapinzani wetu nao ni mechi muhimu kutokana na nafasi waliyonayo, itakuwa mechi yenye ushindani, maandalizi yetu yamekamilika tayari kwa mchezo huo,” amesema Mgunda.
Mchezo mwingie wa pili utaanza kuanzia saa 3:00 usiku ambapo Azam FC itaikaribisha KMC ambayo inazidi kutengeneza uhakika wa kucheza ligi ya Championship kwa msimu ujao, ikiwa mkiani na pointi tisa baada ya michezo 24.
Azam ipo moto ambapo kuanzia ilipochapwa mabao 4-1 ugenini na TRA United haijapoteza mechi yoyote ikishinda nne bila kuruhusu wavu wake kuguswa.
Timu hizo zimekutana kwenye jumla ya michezo 13 lakini rekodi zikaibeba zaidi Azam iliyoshinda michezo tisa huku KMC ikishinda tatu zikitoa sare moja.
KMC itakuwa na kibarua cha kuzuia moto wa kiungo wa Azam FC Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyepo kwenye kiwango bora akifunga mabao 12, akiwa ndio kinara wa ufungaji kwenye ligi lakini pia akiwa na asisti nane.