Zimamoto, Polisi hazishikiki Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, Zimamoto na Polisi hazijaonja ladha ya kipigo baada ya kila moja kushuka dimbani mara sita.
ZIMAMOTO na Polisi, zimeonekana kuwa na makali zaidi katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada ya kuwa timu pekee hadi sasa ambazo hazijapoteza mechi.
Kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, Zimamoto na Polisi hazijaonja ladha ya kipigo baada ya kila moja kushuka dimbani mara sita.
Zimamoto katika mechi hizo sita, imeshinda tano dhidi ya Muembe Makumbi, Chipukizi, Mafunzo, Wembe na KMKM huku sare ikiwa moja dhidi ya Polisi ikikaa kileleni mwa msimamo kwa pointi 16.
Polisi licha ya kutopoteza, lakini inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 12, ikishinda mechi tatu dhidi ya KVZ, Fufuni, Mlandege na sare tatu dhidi ya Mwenge, Mafunzo na Zimamoto.
Uhamiaji ambayo awali nayo ilikuwa haijapoteza na kukaa kileleni kitendo cha kupoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya JKU iliwatibulia na sasa inakamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 15, ikishinda mechi tano na kupoteza moja.
Wakati Zimamoto na Polisi zikiwa hazijapoteza, Fufuni na Mafunzo ndizo pekee hazijaonja ladha ya ushindi baada ya kucheza mechi sita kila moja.
Fufuni ndio ina hali mbaya zaidi kwani matokeo hayo yanaiweka mkiani mwa msimamo ikiwa na pointi mbili, ikitoka sare mechi mbili na kupoteza nne, huku ikiwa ndiyo iliyoruhusu mabao mengi zaidi ambayo ni kumi, ikifunga matatu.
Mafunzo ambayo nayo haijashinda mechi yoyote, inakamata nafasi ya 13 ikiwa na pointi nne kutokana na sare nne ilizopata, ikipoteza mechi mbili.