Zimbwe amuibua Aziz Ki, amtabiria makubwa Yanga
Muktasari:
- Tshabalala na Aziz KI walikuwa wakipambana uwanjani kwa misimu zaidi ya mitano kuanzia kiungo huyo akiwa ASEC Mimosas ya Ivory Coast kisha Yanga kipindi ambacho beki huyo akikipiga Simba.
WAKATI mwenyewe akifurahia maisha mapya Jangwani, beki Mohammed Hussein Zimbwe ‘Tshabalala’ amemuibua kiungo wa Wydad Casablanca ya Morocco, Stephanie Aziz aliyekiri kumkubali mwamba huyo wa zamani wa Kagera Sugar na Simba.
Tshabalala na Aziz KI walikuwa wakipambana uwanjani kwa misimu zaidi ya mitano kuanzia kiungo huyo akiwa ASEC Mimosas ya Ivory Coast kisha Yanga kipindi ambacho beki huyo akikipiga Simba.
Aziz Ki aliondoka Yanga wakati msimu uliopita ukienda ukingoni kwenda Wydad na Tshabalala alitua Yanga kupitia dirisha kubwa msimu huu alipomaliza mkataba Simba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz KI amesema alifurahishwa na Tshabalala kutua Yanga kwani ni beki aliyekuwa anamkubali.
Aziz KI amesema hana wasiwasi na Tshabalala kwa kuwa ni mchezaji aliyekamilika, mwenye kipaji kikubwa na uzoefu wa kutosha ambavyo vinambeba akiwa Yanga.
“Nimefurahi kumuona hapa Yanga. Unajua ukweli huyu ni beki bora hapa Tanzania. Anastahili kuchezea klabu kama hii, naamini atafanya vizuri sana,” amesema Aziz KI aliyepo nchini kwa sasa kwa mapumziko mafupi.
Kumbuka Aziz Ki amemuoa Hamisa Mabetto ambaye ni mwanamitindo na msanii maarufu nchini.
“Tshabalala wote mnafahamu. Licha ya upinzani wetu uwanjani hapo kabla ni beki mshindani. Ana kipaji kikubwa na uzoefu wa kutosha kabisa, nadhani ni usajili bora sana kufanyika na atafanya vizuri zaidi,” amesema Aziz Ki ambaye ni raia wa Burkina Faso.
Ameongeza kwamba amefurahishwa na namna mashabiki wa Yanga walivyompokea beki huyo kwani hatua hiyo imemjenga kirahisi Tshabalala na kuwa na mwanzo mzuri ndani ya timu hiyo.
“Ukiwa mchezaji halafu ukahama kutoka timu moja pinzani na kwenda nyingine lazima unakuwa na wasiwasi, lakini kama mashabiki au viongozi wa timu utakayohamia watakupokea vizuri inakupa nguvu,” amesema Aziz Ki na kuongeza:
“Hiki ndicho ambacho mashabiki wa Yanga wamefanya, walimpokea kwa furaha naye sasa anacheza kwa furaha, ana amani inayotokana na mapokezi ambayo uongozi ulimpa na mashabiki kwa ujumla, mimi nawajua mashabiki wa Yanga wana upendo mkubwa na wachezaji wao.”
Tangu atue Yanga hivi karibuni, Tshabalala ameonekana akipindua meza akianza kikosi cha kwanza akimweka nje Chadrack Boka anayeanzia benchi kwa sasa.
Takwimu zinaonyesha Tshabalala tangu atue Yanga amecheza dakika 555 katika mechi za kimataifa hadi za Ligi Kuu, huku akiwa na rekodi ya kukosa mechi moja tu dhidi ya Mbeya City ulioisha kwa suluhu.
Hadi sasa Yanga imecheza mechi sita katika Ligi Kuu Bara na kufikisha pointi 16, ikishinda tano na sare moja.