AFCON 2025: Gemu ya wakubwa!
Muktasari:
- Chini yao zinafuatia Gabon na Msumbiji, ambazo bado hazina pointi yoyote katika mashindano ya Afcon 2025 baada ya kucheza mechi moja.
RABAT, MOROCCO: MSIMAMO wa Kundi F kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) unasoma, Ivory Coast, ambao ni mabingwa watetezi wanashika namba moja, pointi tatu baada ya mechi moja, wakifuatiwa na Cameroon yenye pointi tatu pia baada ya mechi moja.
Chini yao zinafuatia Gabon na Msumbiji, ambazo bado hazina pointi yoyote katika mashindano ya Afcon 2025 baada ya kucheza mechi moja.
Msumbiji ilichapwa na Ivory Coast 1-0, shukrani kwa bao la Amad Diallo. Gabon yenyewe ilibondwa na Cameroom 1-0, bao la Etta Eyong. Na sasa zilizofungwa mechi za kwanza zinakutana zenyewe na zilizoshinda, zitakuwa na kasheshe la wenyewe kwa wenyewe katika mechi za pili za Kundi F. Mambo ni matamu.
Gabon inayoongozwa na straika la mabao, Pierre-Emerick Aubameyang itashuka uwanjani Stade Adrar kusaka ushindi wao wa kwanza kwenye Afcon 2025 kwa kumenyana na Msumbiji, huku rekodi zikionyesha kwamba kwenye mechi tatu zilizokutanisha timu hiyo mbili huko nyuma, Gabon imeshinda mara mbili ikiwamo kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia, wakati Msumbiji ilishinda mara moja, ambayo ilikuwa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia pia.
Lakini, safari hii timu hizo mbili zitachuana katika mechi muhimu kwa kila mmoja, wakisaka pointi ili kuwafanya kuwa hai katika msako wao wa kuwania nafasi ya kutinga mtoano wa mashindano hayo ya ubingwa wa Afrika.
Kasheshe zito litakuwa huko Stade de Marrakech, ambapo miamba miwili ya soka la Afrika, Ivory Coast na Cameroon itakapoonyeshana ubabe uwanjani.
Ivory Coast yenye mastaa kibao ndio mabingwa watetezi, lakini wanakabiliana na Simba Wasioshindika, ambao shughuli yao ndani ya uwanja sio ya mchezo. Patachimbika.
Mechi hiyo inakutanisha mastaa wawili wanaokipiga kwenye kikosi cha Man United, Amad, atakayekuwa upande wa Ivory Coast, wakati Bryan Mbeumo atakuwa upande wa Cameroon.
Kimbembe kingine cha mechi za pili za mashindano ya Afcon 2025 zitakuwa kwenye Kundi E, ambapo Equatorial Guinea itaonyeshana ubabe na Sudan, huku Algeria itakuwa na shughuli pevu na Burkina Faso.
Algeria na Burkina Faso zilishinda mechi zao za kwanza, hivyo zitachuana zenyewe katika kutafuta timu itakayotangulia kutinga hatua ya mtoano katika kundi hilo, wakati Sudan na Equatorial Guinea zitakutana zenyewe zinazosaka ushindi wa kwanza baada ya kupoteza katika mechi za kwanza. Mambo ni moto.