Baleba afuzu vipimo, kusaini Man United
Muktasari:
- Manchester United inatarajiwa kutangaza rasmi usajili huo wakati wowote leo baada ya kufikia makubaliano ya kumsajili kiungo huyo raia wa Cameroon kwa jumla ya pauni 70milioni.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa Brighton, Carlos Baleba amefaulu vipimo vya afya na kusaini mkataba wa miaka mitano na Manchester United, ukiwa na kipengele cha kuongeza muda hadi mwaka 2032.
Manchester United inatarajiwa kutangaza rasmi usajili huo wakati wowote leo baada ya kufikia makubaliano ya kumsajili kiungo huyo raia wa Cameroon kwa jumla ya pauni 70milioni.
United italipa pauni65 milioni kama ada ya msingi, huku pauni milioni tano zikilipwa kama bonasi kulingana na vigezo vilivyowekwa kwenye mkataba.
Baleba, 22, alitumia muda wa mwisho wa wiki jijini Manchester na alifika katika kituo cha mazoezi cha Carrington Jumapili kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili.
UNITED YAMTAZAMA BALDE
Wakati huo huo, Manchester United inaendelea kumfuatilia beki wa kushoto wa Barcelona, Alejandro Balde, ikiwa sehemu ya mipango ya kuongeza chaguo katika nafasi hiyo.
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, alizungumzia mustakabali wa Balde baada ya timu yake kuichapa Elche mabao 5-0 ugenini Jumapili usiku, huku beki huyo wa Hispania akiwa hajawekwa kwenye kikosi.
“Nimezungumza na Balde asubuhi hii na nikamwambia kwamba kwa maoni yangu hayupo hapa kwa asilimia 100. Anapaswa kuweka mambo yake sawa kwanza, kisha tutazungumza,” alisema Flick.
UNITED YAONGEZA VIUNGO
United tayari imesajili viungo wawili wa kati, Andrey Santos kutoka Chelsea na Youri Tielemans kutoka Aston Villa, kwa jumla ya pauni85 milioni.
Wachezaji hao wote walianza mchezo wa kwanza wa Manchester United katika msimu mpya wa Ligi Kuu England, ambapo timu hiyo ilipokea kipigo cha kushtukiza cha mabao 2-0 kutoka kwa Hull Jumamosi.
Kwa upande mwingine, mchezaji wa akademi ya Manchester United, Jacob Devaney, ameondoka Old Trafford na kujiunga na Hibernian kwa mkopo wa msimu mmoja.
Mkataba huo una kipengele kinachoiwezesha Hibernian kumsajili moja kwa moja mchezaji huyo baada ya kumalizika kwa kipindi cha mkopo.