Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Barcelona yasua sua dili la Marcus Rashford

FUNUNU Pict

Muktasari:

  • Inaelezwa Barca inatakiwa kulipa takribani Euro 30 milioni ili kubadilisha mkataba wa Rashford kuwa wa moja kwa moja lakini kiasi hicho kinaonekana kuwa kikubwa kwao.

BARCELONA inaripotiwa bado haijafanya uamuzi wa kumsainisha mkataba wa moja kwa moja mshambuliaji wa Manchester United Marcus Radhford ambaye msimu huu anacheza kwa mkopo katika kikosi chao.

Inaelezwa Barca inatakiwa kulipa takribani Euro 30 milioni ili kubadilisha mkataba wa Rashford kuwa wa moja kwa moja lakini kiasi hicho kinaonekana kuwa kikubwa kwao.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mundo Deportivo, Barcelona kwa sasa inaendelea kutathmini hali yao ya kifedha kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu nyota huyo wa England mwenye umri wa miaka 28.

Ripoti hizo pia zinaeleza Aston Villa inafuatilia kwa karibu hali ya Rashford na wako tayari kuingia kwenye mbio za kuiwania saini yake iwapo Barcelona itashindwa kukamilisha dili hilo.

Rashford ameendelea kuwa mmoja wa majina makubwa kwenye soko la usajili kutokana na kiwango bora alichoonyesha akiwa na Barca kwa msimu huu.

Manchester United imeendelea kusisitiza kwa mabosi wa Barca, hawapo tayari kupunguza hata senti katika bei ya Rashford ya sasa na wakishindwa kutoa kiasi cha pesa kinachohitajika watamuuza kwenda klabu nyingine. Mkataba wa sasa wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.


Robin Roefs

CHELSEA imeripotiwa kutafuta golikipa mpya dirisha lijalo la majira ya kiangazi na kipa wa Sunderland, Robin Roefs ni miongoni mwa wale inaowahitaji.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Mirror, Chelsea imevutiwa sana na maendeleo ya kipa huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 23 ambaye ameonyesha kiwango kizuri na utulivu mkubwa langoni msimu huu licha ya kutokuwa na uzoefu mkubwa.

Roefs ameendelea kujijengea jina kama mmoja wa makipa vijana wanaochipukia kwa kasi Ulaya, jambo lililoifanya Chelsea kuanza kumwangalia kama chaguo lao la muda mrefu kwa sababu hawaridhishwi na kiwango cha Roberto Sanchez.


Rodri

KIUNGO wa kimataifa wa Hispania, Rodri, hana presha kuhusu hatma yake Manchester City licha ya kubakiwa na mwaka mmoja katika mkataba wake.

Kwa mujibu wa tovuti ya Marca, nyota huyo, 29, kwa sasa akili yake yote ipo katika kumalizia msimu vizuri akiwa na wababe hao  badala ya kujadili suala la mkataba mpya au kuondoka.

Rodri ameendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi Man City kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuiongoza safu ya kiungo na kudhibiti mchezo.

Kauli yake inakuja wakati ambao kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazomhusisha na Real Madrid.


Gabriel Jesus

ARSENAL inaripotiwa kuwa tayari kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa Brazil, Gabriel Jesus kwa ada inayokadiriwa kufikia Pauni 30 milioni dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Taarifa kutoka tovuti ya Caught Offside, mshambuliaji huyo, 29, ameanza kuhusishwa na klabu kubwa za Italia, zikiwamo AC Milan na Juventus, ambazo vinafuatilia hali yake kwa karibu.

Jesus amekuwa akipitia changamoto ya majeraha katika vipindi tofauti tangu ajiunge na washika mitutu hao hali inayosababisha asionyeshe kiwango kilichotarajiwa. Kwa sasa Arsenal wako tayari kusikiliza ofa nzuri kwa ajili ya mchezaji huyo.


Said El Mala

BRENTFORD imeingia katika orodha ya klabu zinazoiwania saini ya winga chipukizi wa FC Cologne na timu ya taifa ya Ujerumani, Said El Mala.

Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Mail, Brentford sasa inashindana na Brighton na Chelsea ambazo pia zimekuwa zikifuatilia maendeleo ya mchezaji huyo, 19, kwa karibu.

Hata hivyo, kwa sasa bado haijafahamika ikiwa Cologne wako tayari kumuuza mapema fundi huyo au wataendelea kumlea kama sehemu ya mipango yao ya muda mrefu.


Ethan Ampadu

LEEDS United inadaiwa kuwa na mpango wa kumwongeza mkataba kiungo wao wa kimataifa wa Wales, Ethan Ampadu, 25.

Kwa mujibu wa tovuti ya Football Insider, Ampadu naye yuko tayari kuendelea kubaki Elland Road, hali inayofanya mazungumzo hayo kuwa na uwezekano mkubwa wa kufikia makubaliano haraka.

Ampadu amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu Leeds kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali ikiwemo kiungo wa kati na beki wa kati, jambo linalomfanya kuwa mhimili wa timu.


Morgan Rogers

CHELSEA imeonyesha nia ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Aston Villa, Morgan Rogers, dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa klabu nyingine kubwa Ulaya.

Kwa mujibu wa Talksport, Arsenal, Manchester United pamoja na Paris Saint-Germain nazo ni miongoni mwa timu zinazoiwania saini ya  kiungo huyo, 23.

Rogers ameendelea kuvutia macho ya vigogo wengi Ulaya kutokana na kiwango chake bora akiwa Aston Villa.


Jacobo Ramon

REAL Madrid inafikiria kutumia kipengele cha kumnunua beki wao wa zamani Mhispania, Jacobo Ramon, 21, ambaye kwa sasa anaichezea Como 1907 ya Italia.

Awali ilielezwa Madrid haikuwa na uhakika wa kumsajili fundi huyu jambo lililoifanya Chelsea kuanza kumnyemelea.

Jacobo ambaye alitokea Madrid wakati anajiunga na Como, katika mkataba wake kuna kipengele ambacho kinaipa nafasi Madrid kumsajili kwanza kabla ya timu yoyote.