Kesi ya Man City yatikisa England, Tuchel afichua jambo
Muktasari:
- Man City imekutwa na hatia ya kuvuruga taarifa zake za kifedha, huku Tume Huru ikieleza klabu hiyo iliongeza mapato yake kwa takribani Pauni 900 milioni katika kipindi cha miaka tisa kupitia mfumo wa ufadhili uliofichwa pamoja na mikataba ya udhamini iliyoelezwa kuwa ya kughushi.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel amefichua baadhi ya wachezaji wa Manchester City wana wasiwasi kuhusu hatma yao baada ya klabu hiyo kukutwa na hatia ya kukiuka kanuni za kifedha.
Man City imekutwa na hatia ya kuvuruga taarifa zake za kifedha, huku Tume Huru ikieleza klabu hiyo iliongeza mapato yake kwa takribani Pauni 900 milioni katika kipindi cha miaka tisa kupitia mfumo wa ufadhili uliofichwa pamoja na mikataba ya udhamini iliyoelezwa kuwa ya kughushi.
Hata hivyo, City imeendelea kusisitiza kuwa haina hatia na imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Tuchel amekiri kuwa hali hiyo imewaweka katika sintofahamu baadhi ya wachezaji wake wanaohusishwa na City, akiwemo Marc Guehi, Elliot Anderson na Nico O'Reilly.
Wachezaji hao wamekuwa wakipokea simu na ujumbe mwingi kuhusu kinachoendelea katika klabu hiyo, huku O'Reilly akiwa tayari amerejea Manchester kwa ajili ya matibabu ya jeraha.
Tuchel alisema wasiwasi huo ni jambo la kawaida kwa wachezaji vijana ambao hawajui hatma ya klabu wanayoichezea.
“Je, wana wasiwasi? Nadhani hiyo ni hali ya kibinadamu kabisa unapokuwa hujui kinachoendelea katika klabu uliyoisaini,” alisema Tuchel.
“Bado ni vijana, wana malengo makubwa. Wameambiwa hawana hatia kabisa na hawajui kinachoendelea.”
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea aliongeza kuwa suala hilo limekuwa likijadiliwa mara kwa mara ndani ya kambi ya England.
“Tunazungumza kuhusu hilo wakati wa chakula cha jioni na mezani tukiwa watu wanane au 12. Bila shaka tunazungumza pia wakati wa kifungua kinywa,” alisema.
Tuchel alisema habari hizo zimekuwa “kero” kwa kiasi fulani, ingawa alisisitiza kuwa wachezaji hao wameendelea kuonyesha umakini wakati wa mikutano na mazoezi.
“Ni mada kubwa kambini. Tulikuwa na muda wa mapumziko kati ya mechi na ni jambo kubwa. Linawezaje kutokuwa mada? Tunazungumza nao, lakini kwa muda mfupi,” aliongeza.
HATIMA YAO ENGLAND
Tuchel pia alisema huenda akaendelea kuwachagua wachezaji wanaohusika na Manchester City hata kama klabu hiyo itashushwa daraja kutoka Ligi Kuu ya England kama sehemu ya adhabu, endapo rufaa yao haitafanikiwa.
“Daima nitajaribu kuchagua kikosi bora kwa ajili ya kambi, tukio au mashindano. Sitawahi kuwatenga kwa sababu hawachezi Ligi Kuu katika nchi yao. Tunahitaji kuangalia kila suala kwa namna yake,” alisema.
AMHURUMIA STERLING
Wakati huohuo, Tuchel ameelezea masikitiko yake kuhusu hali anayopitia Raheem Sterling, ambaye kwa sasa hana klabu baada ya kuondoka Chelsea.
Sterling, ambaye aliwahi kuichezea England, alikiri kosa la kuendesha gari kwa njia hatarishi baada ya kupata ajali akiwa katika gari lake aina ya Lamborghini lenye thamani ya takribani Pauni 270,000.
Mchezaji huyo pia alikiri kosa la kuwa na nitrous oxide na kukataa kutoa sampuli baada ya kusimamishwa na polisi mwishoni mwa Mei. Anasubiri uamuzi wa adhabu au kupelekwa katika Mahakama ya Crown mwezi Novemba.
Tuchel alikuwa miongoni mwa watu waliomsukuma Chelsea kumsajili Sterling kutoka Manchester City kwa Pauni 47.5 milioni mwaka 2021.
Licha ya kutokuwa amewasiliana naye katika wiki za hivi karibuni, Tuchel alisema anaendelea kumhurumia mchezaji huyo.
“Ninamuhurumia sana na nahisi amekuwa akipambana tangu alipoondoka Man City, wakati alipokuwa katika kilele cha maisha yake ya soka,” alisema.
Tuchel aliongeza kuwa anasikitishwa kumuona Sterling akipitia kipindi kigumu, akimtaja kama baba aliyejitolea kwa watoto wake na mtu aliyekuwa akipenda familia.
“Inaonekana amepitia kipindi kigumu. Sina uhakika ni kwa kiasi gani ni kosa lake. Wakati mwingine unaweza kuingia katika mzunguko wa ajabu wa maisha, mzunguko unaoshuka. Mawazo yangu yako kwake na ninaamini anaweza kubadilisha hali hiyo. Namtakia kila la heri,” alisema Tuchel.