Kocha Al Hilal adai likizo iliathiri viwango
Muktasari:
- Matokeo hayo yanaipa Al Hilal pointi tatu muhimu na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya mtoano huku Tusker ikianza vibaya na kulazimika kutafuta ushindi katika michezo yake iliyosalia ili kuendelea kuwa na matumaini ya kusonga mbele kwenye Kombe la CECAFA Kagame 2026.
KOCHA wa Al Hilal ya Sudan, Guy Bukasa Misakabu amesema ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tusker ya Kenya ni mwanzo mzuri kwa timu yake katika Kombe la CECAFA Kagame 2026, lakini akikiri kuwa wachezaji wake bado hawajafikia viwango bora vya utimamu wa mwili baada ya kurejea kutoka mapumziko mafupi.
Misakabu amesema jambo muhimu kwa sasa ni kuanza mashindano kwa ushindi ili kuongeza morali ndani ya kikosi chake kuelekea michezo inayofuata ya hatua ya makundi.
“Tumetoka mapumzikoni muda mfupi uliopita na wachezaji bado hawajawa fiti kwa asilimia mia moja. Lakini, jambo la muhimu ni kwamba tumeanza mashindano kwa ushindi. Hilo linatupa nguvu ya kuendelea kupambana katika mechi zijazo,” amesema kocha huyo.
Katika mchezo huo wa Kundi C, Al Hilal ilianza kwa kutawala mchezo tangu dakika za mwanzo, ikitengeneza mashambulizi ya mara kwa mara yaliyowalazimu mabeki wa Tusker kufanya kazi kubwa.
Ubora wa Al Hilal ulizaa matunda dakika ya 29 baada ya beki Kamaradini Mamudu kupachika bao la kuongoza, akimalizia vizuri shambulizi lililoanzia upande wa kulia.
Baada ya kuruhusu bao, Tusker ilijaribu kujibu mapigo na kusogea mbele kutafuta kusawazisha dakika ya 36, Aboud Omar alipata nafasi nzuri, lakini shuti lake lilikosa mwelekeo na kuiacha Al Hilal ikienda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Dakika ya 90+5, mchezaji wa akiba Salim Adams alihitimisha ushindi wa Al Hilal baada ya kumalizia mpira uliomkuta ndani ya eneo la hatari na kumshinda kipa Francis Odour Onyango, akifunga bao lililozima kabisa matumaini ya Tusker kusaka sare.
Matokeo hayo yanaipa Al Hilal pointi tatu muhimu na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya mtoano huku Tusker ikianza vibaya na kulazimika kutafuta ushindi katika michezo yake iliyosalia ili kuendelea kuwa na matumaini ya kusonga mbele kwenye Kombe la CECAFA Kagame 2026.