PSG yampigia hesabu Julian Alvarez
Muktasari:
- PSG inaonekana kutaka kuongeza nguvu mpya katika safu yao ya ushambuliaji, ili kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kitaifa na kimataifa msimu ujao.
PARIS Saint-Germain inataka kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Argentina, Julian Alvarez, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Nyota huyo wa ameendelea kuvutia klabu kubwa za Ulaya kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao na mbali ya PSG, huduma yake pia inahitajika na Arsenal ambayo ilihitaji kumsajili tangu dirisha la usajili mwaka jana.
PSG inaonekana kutaka kuongeza nguvu mpya katika safu yao ya ushambuliaji, ili kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kitaifa na kimataifa msimu ujao.
Mkataba wa sasa wa Alvarez unatarajiwa kumalizika 2030 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 49 za michuano yote, amefunga mabao 20 na kutoa asisti tisa.
Mabosi wa Atletico wanadaiwa kuwa tayari kumuuza staa huyu lakini kwa timu itakayokuwa tayari kutoa zaidi ya Euro 100 milioni kama ada yake ya uhamisho.
Ederson
MANCHESTER United imeongeza juhudi kuwafuatilia viungo wawili, Ederson, 26, kutoka Atalanta na Mateus Fernandes, 21, wa West Ham United. Ederson ameendelea kung’ara Serie A kutokana na uwezo wa kucheza kama box-to-box, na Man United ipo tayari kulipa takribani Pauni 50 milioni ili kumnunua. Man United inataka kuimarisha safu ya kiungo cha kati kwa kuziba pengo litakaloachwa na Casemiro anayetarajiwa kuondoka.
Ben White
BEKI wa Arsenal, Ben White anataka kujua hatma yake kwanza katika kikosi cha Arsenal kabla ya kukubali ofa ya kujiunga na Everton katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Beki huyo wa England mwenye miaka 28 ameendelea kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Arsenal katika misimu ya hivi karibuni, lakini ushindani wa nafasi ndani ya timu umemfanya kutopewa muda mwingi wa kucheza. Everton wanaripotiwa kutaka kumsajili.
Jacobo Ramon
REAL Madrid bado hawajafanya uamuzi wa kutumia kipengele cha kumnunua beki wao wa zamani Mhispania, Jacobo Ramon, 21, ambaye kwa sasa anaichezea Como ya Italia. Kutokuwa na uhakika kwa Madrid kunaweza kuipa Chelsea nafasi ya kuingia kwenye mbio za kumsajili beki huyo kijana. Jacobo ambaye alitokea Madrid wakati anajiunga na Como, katika mkataba wake kuna kipengele ambacho kinaipa nafasi kumsajili kabla ya timu yoyote.
Robert Lewandowski
FC Porto imeonyesha nia ya dhati ya kumsajili mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Poland, Robert Lewandowski, 37, kwa uhamisho wa bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Hata hivyo, bado kuna uwezekano mkubwa wa Lewandowski kusaini mkataba mpya na Barcelona na akaendelea kubaki Hispania. Lewandowski ameendelea kuwa mmoja wa washambuliaji wenye uzoefu mkubwa Ulaya.
Joao Gomes
ATLETICO Madrid iko karibu kufikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa Wolves, Mbrazil, Joao Gomes mwenye umri wa miaka 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Inaripotiwa kuwa dili hilo linaweza kuigharimu Atletico kiasi cha Pauni 39 milioni na tayari makubaliano binafsi kati ya mchezaji na wawakilishi wa wababe hao wa Madrid yameshafanyika. Gomes anadaiwa kuwaambia mabosi wa Wolves hataendelea kusalia katika kikosi.
Lois Openda
LEEDS United inaonekana kuwa mbele katika mbio za kumsajili mshambuliaji wa Juventus na Ubelgiji, Lois Openda, 26, katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Hata hivyo, Coventry City pia imeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo inayeaminia atasaidia kikosi michuano ya Ligi Kuu England msimu ujao. Kwa upande wa Leeds, Openda ameahidiwa kuwa kipaumbele safu ya ushambuliaji.
Jannik Schuster
WEST Ham United, Leeds United na Brighton zinadaiwa kuingia katika vita dhidi ya Brentford kwa ajili ya kumsajili beki raia wa Austria, Jannik Schuster, 19, kutoka RB Salzburg, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Brentford ilionekana kuwa mbele katika mbio hizo, lakini sasa ushindani kutoka klabu nyingine za Ligi Kuu England zinaonekana kufanya dili hilo kuwa gumu zaidi.