Sávio aanza kwa kasi spurs, afunga bao la kwanza
Muktasari:
- Sávio alifunga bao hilo usiku wa kuamkia leo katika mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Carabao, Tottenham ilipoichapa Charlton Athletic 5-1.
LONDON, ENGLAND: Saa 48 tu baada ya kukamilisha usajili wake kutoka Manchester City, kiungo mshambuliaji wa Brazil, Sávio, ameanza maisha yake Tottenham Hotspur kwa kishindo baada ya kufunga bao lake la kwanza akiwa na miamba hiyo ya Kaskazini mwa London.
Sávio alifunga bao hilo usiku wa kuamkia leo katika mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Carabao, Tottenham ilipoichapa Charlton Athletic 5-1.
Mchezaji huyo wa Brazil amejiunga na Spurs akitokea Manchester City kwa ada ya awali ya Pauni milioni 75, ambayo inaweza kufikia Pauni milioni 85 kutokana na nyongeza zilizowekwa kwenye mkataba.
Sávio amesaini mkataba wa miaka mitano na Tottenham, na tayari ameanza kuonyesha thamani yake katika kikosi hicho baada ya kuhitaji dakika chache tu kuandika jina lake kwenye ubao wa wafungaji.
Mabao mengine ya Tottenham katika ushindi huo yalifungwa na Mikey Moore, Dominic Solanke, Kevin Danso na Ben Davies, na kuifanya Spurs kusonga mbele katika mashindano hayo.