SAFA yampa Mosimane mikoba ya kuinoa Bafana Bafana
Muktasari:
- Mosimane aliwahi kuiongoza Bafana Bafana kati ya mwaka 2010 na 2012, kabla ya kuendelea na safari yake ya ukocha katika klabu mbalimbali ndani na nje ya Afrika Kusini.
Johannesburg. Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA) limemtangaza Pitso Mosimane kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo ‘Bafana Bafana’ huku likimpa majukumu mazito.
Mosimane mwenye umri wa miaka 62, anarejea kuiongoza timu hiyo kwa mara ya pili, akichukua nafasi ya kocha Mbelgiji, Hugo Broos, huku akipewa kazi ya kuhakikisha timu hiyo inapata mafanikio makubwa.
Kocha huyo anatarajiwa kuiongoza Bafana Bafana, katika harakati za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, kombe la Africa Nations League pamoja na kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2030.
Afrika Kusini ipo Kundi D, pamoja na Guinea, Eritrea na Kenya katika kuwania kufuzu AFCON 2027.
Uteuzi huo umetangazwa leo Jumanne, Septemba Mosi, 2026 na Rais wa SAFA, Danny Jordaan, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Johannesburg.
Kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu Afrika Kusini, Pitso Mosimane
“Nimemfahamu Pitso kwa miaka mingi na nimewahi kufanya naye kazi. Natarajia kuendeleza ushirikiano wetu na kufanya kazi kwa maslahi ya soka la Afrika Kusini na Bafana Bafana,” amesema Jordaan.
Mosimane aliwahi kuiongoza Bafana Bafana kati ya mwaka 2010 na 2012, kabla ya kuendelea na safari yake ya ukocha katika klabu mbalimbali ndani na nje ya Afrika Kusini.
Ujio wa Mosimane umekuja wakati Bafana Bafana ikiwa imetoka kuweka historia katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 mwaka huu katika nchi za Marekani, Canada na Mexico, kwa kufuzu kwa mara ya kwanzaa hatua ya 16 bora.
Akizungumza baada ya kutangazwa, Mosimane amesema amerejea akiwa na imani kuwa bado ana mchango mkubwa wa kutoa katika soka la nchi yake.
“Ninachukua jukumu hili nikijua kwamba bado nina kitu cha kutoa katika soka, hasa katika nchi yangu. Nafanya hivyo nikiwa na uzoefu wa miaka mingi, lakini pia nikiwa na uelewa mkubwa zaidi wa maana ya kuiongoza Bafana Bafana,” amesema.
Kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu Afrika Kusini, Pitso Mosimane
Mosimane ni miongoni mwa makocha maarufu na wenye mafanikio makubwa Afrika Kusini.
Katika kipindi cha kazi yake, amefundisha klabu mbalimbali kubwa na kushinda mataji makubwa ndani na nje ya nchi.
Amewahi kuzifundisha SuperSport United, Mamelodi Sundowns za Afrika Kusini na Al Ahly ya Misri, kabla ya kuendeleza safari yake ya ukocha katika nchi za Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE) na Iran.
Macho ya mashabiki wa soka Afrika Kusini yanaelekezwa kwake kuona kama ataweza kuendeleza mafanikio ya Bafana Bafana na kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri kuelekea AFCON 2027 na Kombe la Dunia 2030.