Uswisi yatinga 16 bora Kombe la Dunia, Algeria ikiaga mashindano
Muktasari:
- Uswisi katika mechi hiyo ya hatua ya 32 bora iliyochezwa kwenye Uwanja wa BC Place uliopo Vancouver, Canada ilitangulia kupata bao katika dakika ya 10 lililofungwa na Breel Embolo, aliyemalizia pasi nzuri ya kiungo nyota wa kikosi hicho, Johan Manzambi.
VANCOUVER, CANADA: TIMU ya taifa ya Uswisi imekata tiketi ya kucheza hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Algeria maarufu kama Les Fennecs.
Uswisi katika mechi hiyo ya hatua ya 32 bora iliyochezwa kwenye Uwanja wa BC Place uliopo Vancouver, Canada ilitangulia kupata bao katika dakika ya 10 lililofungwa na Breel Embolo, aliyemalizia pasi nzuri ya kiungo nyota wa kikosi hicho, Johan Manzambi.
Bao hilo la Embolo ni la pili kwake kufunga katika Kombe la Dunia 2026, huku akifikisha jumla ya mabao manne akiwa na kikosi hicho cha Uswisi, baada ya kufunga pia mawili katika fainali za mwaka 2022 zilizofanyika nchini Qatar.
Kufunga mabao mawili katika fainali za Kombe la Dunia za 2022 na mawili pia 2026 kunamfanya Embolo kuwa mchezaji wa kwanza wa timu ya taifa ya Uswisi kufunga zaidi ya bao moja katika fainali mbili tofauti. Hata hivyo, bado yupo nyuma ya Xherdan Shaqiri mwenye mabao matano na Josef Hügi aliyefunga mabao sita.
Bao hilo la Embolo liliifanya Uswisi kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0, licha ya Algeria kucheza soka la kuvutia, ambapo timu hiyo ilimiliki mpira kwa asilimia 59, huku wapinzani wao wakimiliki asilimia 41.
Wakati Algeria ikijitafakari namna ya kusawazisha, ilishtukizwa mapema katika dakika ya 46 ya kipindi cha pili baada ya Dan Ndoye kuifungia Uswisi bao la pili, lililovunja matumaini ya timu hiyo kutoka Afrika Kaskazini.
Matokeo hayo yanaifanya Uswisi kufuzu hatua ya 16 bora, ambapo itakutana na mshindi wa mechi kati ya Colombia na Ghana, zitakazocheza alfajiri ya kesho, Jumamosi, Julai 4, 2026, saa 10:30.
Historia ya Uswisi katika Kombe la Dunia ni ndefu na yenye mafanikio ya kawaida, ambapo timu hiyo imeshiriki mara 13 hadi sasa tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1934. Imeshiriki pia mwaka 1938, 1950, 1954, 1962, 1966, 1994, 2006, 2010, 2014, 2018, 2022 na 2026.
Katika Kombe la Dunia lililofanyika Ujerumani 2006, Uswisi ilitolewa katika hatua ya 16 bora bila kufungwa bao lolote katika muda wa kawaida wala wa nyongeza, kwani iliondolewa kwa mikwaju ya penalti 3-0 dhidi ya Ukraine baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 120.
Uswisi ilikuwa timu ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kuondolewa mashindanoni bila kufungwa bao hata moja katika muda wa kawaida au wa nyongeza, rekodi iliyowekwa kwenye michuano hiyo iliyofanyika Ujerumani 2006.
Mbali na hilo, Uswisi pia iliandika rekodi mbovu kwa kuwa timu ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kushindwa kufunga hata penalti moja baada ya sare katika mechi ya mtoano, kufuatia kukosa mikwaju yote mitatu dhidi ya Ukraine.
Mafanikio makubwa ya Uswisi ni kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia mara tatu, mwaka 1934 nchini Italia, 1938 nchini Ufaransa na 1954 ilipokuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Hata hivyo, haijawahi kufika hatua ya nusu fainali wala fainali.
Kwa upande wa Algeria, maarufu kama Les Fennecs, imekuwa moja ya timu muhimu kutoka Afrika katika historia ya Kombe la Dunia, ambapo kikosi hicho kinashiriki michuano hiyo kwa mara ya tano tangu kilipoanza kushiriki mwaka 1982. Kimeshiriki pia 1986, 2010, 2014 na 2026.
Katika ushiriki wake wa kwanza wa Kombe la Dunia lililofanyika Hispania mwaka 1982, Algeria iliishangaza dunia baada ya kuifunga Ujerumani Magharibi, iliyokuwa inaongoza Kundi la Pili, kwa mabao 2-1, ingawa ilitolewa hatua ya makundi baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu.
Timu hiyo ilirejea tena kwenye Kombe la Dunia 1986 lililofanyika Mexico na kuangukia Kundi D lililokuwa na Brazil, Hispania na Ireland ya Kaskazini. Algeria ilimaliza mkiani mwa kundi hilo kwa kupata pointi moja.
Baada ya kushiriki fainali hizo za 1986, Algeria ilichukua miaka 24 kurejea tena Kombe la Dunia, lililofanyika nchini Afrika Kusini 2010, ambapo ilimaliza pia mkiani mwa Kundi C nyuma ya vinara Marekani, England na Slovenia.
Mafanikio makubwa ya Algeria ni kufika hatua ya 16 bora katika Kombe la Dunia 2014 lililofanyika Brazil, ambapo ilifungwa mabao 2-1 na Ujerumani katika dakika ya 120 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 za kawaida, Juni 30, 2014.