Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ticha Star; Msomi aliyeiheshimisha dansi, anakuja kwa kasi albamu ikipikwa

TICHA Pict

Muktasari:

  • Mashabiki wengi wa muziki wanaona muziki huu unazidi kudidimia kutokana na kupoteza mvuto wake na wasanii wenyewe wameishiwa, hata hivyo, Meserecordias Wilfred Lema ambalo si jina ngeni katika fani hiyo anadhihirisha hilo.

KAMA ulidhani muziki wa dansi umepotea, soma makala haya kwani wakati wengi wakidhani hivyo, kumeibuka tumaini jipya la kuhakikisha unabaki salama na kuendelezwa kwa nguvu zote.

Mashabiki wengi wa muziki wanaona muziki huu unazidi kudidimia kutokana na kupoteza mvuto wake na wasanii wenyewe wameishiwa, hata hivyo, Meserecordias Wilfred Lema ambalo si jina ngeni katika fani hiyo anadhihirisha hilo.

Mwanamuziki huyo anayefahamika kwa jina la kisanii la Ticha Star, ameendelea kufanya makubwa katika muziki wa dansi na kuthibitisha elimu na sanaa vinaendana.


NI NANI TICHA STAR

Ni  mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya Mzee Wilfred Lema, na mkewe Bi. Zenobia Lema.

Ni mzaliwa wa Mkoa wa Kilimanjaro na kwa sasa anaishi jijini Dodoma na mbali na muziki ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dodoma akiwa pia na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika masuala ya Uhandisi wa Mazingira.

TICH 01

R. KELLY, MICHAEL JACKSON WAMVUTA

Safari ya muziki ya Ticha Star ilianza tangu akiwa mwanafunzi wa Azania Secondary School alipokuwa akiimba nyimbo za wasanii wa RnB wa kimataifa kama R. Kelly, Joe Thomas na Michael Jackson.

Baada ya kuhitimu masomo yake katika University of Dar es Salaam mwaka 2008, aliingia rasmi studio na kutoa wimbo wake wa kwanza 'Gheto' aliowashirikisha Inspector Haroun Babu pamoja na KBazil.

Hiyo ilimfanya kukaa kwa muda mfupi katika Bongo Fleva kabla ya kuhamishia nguvu katika dansi aliko hadi sasa.


KAANZIA MBALI

Mwaka 2018 alianza rasmi kufanya muziki wa jukwaani katika kumbi mbalimbali za starehe jijini Dodoma kwa kutumia nyimbo za dansi zilizopendwa zamani na za wakati huo, kama 'Acha tamaa', Aminata, Rangi ya chungwa na nyingine nyingi.

Kutokana na kazi hiyo, alijozolea umaarufu mkubwa na hapo ndipo alipopatia wazo la kuanzisha bendi yake binafsi ili kumpa sapoti kila anapokuwa jukwaani kikazi.

Mwaka 2020 alianzisha bendi yake ya T Band Internationale iliyomsaidia kufanya maonyesho ya jukwaani na kutambulisha nyimbo zake kwa mashabiki  na hadi sasa ameshatoa nane zikiwemo 'Ukinipenda', 'Sabrina', 'Mazoea', 'God is Good', 'Chawa' na 'Watoto wa Mungu'. Wimbo wa 'Chawa' ndio pekee wenye video rasmi ukiwa katika mahadhi ya Amapiano.

TICH 02

CHANGAMOTO ZA KUJITAFUTA

Nyota huyu anayetamba na kazi mbalimbali kama 'Gheto', aliowashirikisha Inspector Haroun Babu pamoja na KBazil, 'Ukinipenda', 'Sabrina', 'Mazoea' na nyingine nyingi, anasema muziki unahitaji pesa na akili ili kufikia malengo, pia umakini ni muhimu.

Anasema katika kufanya sanaa yake amekutana na chamoto mbalimbali, ikiwemo ya watayarishaji wa muziki kuchelewesha kumaliza nyimbo kwa wakati na wakati mwingine kutengeneza tofauti na maelekezo ya mwanamuziki.

Pia  mwanamuziki kusimamia wimbo wake mwenyewe bila kuwa na usimamizi ni changamoto kwani kuutangaza wimbo siku hizi inahitaji mambo mengi ikiwamo muda, fedha, connection, umakini na ufuatiliaji, na katika hali ya kawaida ni ngumu kwa mwanamuzikikuweza kufanya yote mwenyewe.

“Promotion ya muziki wa siku hizi inahitaji fedha, connection, muda na umakini mkubwa, hivyo ni vigumu kwa mwanamuziki kufanya kila kitu mwenyewe bila management,” anasema Ticha STAR.

Changamoto nyingine ni kutokuwepo na mikataba ya kazi wakati wanamuziki wa dansi tunapokwenda kufanya kazi kwenye kumbi za starehe.

"Wakati mwingine mwenye ukumbi anaweza kuamua kukulipa anachojisikia yeye, sio mlichokubaliana awali na kwa kuwa huna mkataba wowote naye, unashindwa kupata haki yako."


TUZO ZAZIDI KUMWEKA KILELENI

Usiku wa Mei 1, 2026 kwenye Ukumbi wa Ngoreme Park, Ticha Star aliandika historia baada ya kutangazwa mshindi wa kipengele cha 'Best Collabo' kwenye tuzo za Cheza Kidansi Music Awards kutokana na wimbo wake wa 'Watoto wa Mungu'.

Katika tuzo hizo, pia aliibuka na tuzo ya 'Best Upcoming Artist.

Hii si mara ya kwanza kwa Ticha STAR kufanya vizuri katika tuzo hizo. Mwaka 2022 aliibuka mshindi kupitia wimbo 'Ukinipenda' aliomshirikisha marehemu Catty Soul, kabla ya kurejea tena mwaka 2024 na 'Nimekumiss' aliomshirikisha Melody Mbassa.

Anaongeza ukiacha mafanikio ya kupata heshima ya kubeba tuzo tano  za kitaifa, pia amejitangaza na kufahamika kitaifa na kimataifa na kuongeza idadi ya mashabiki wanapenda nyimbo zake duniani kote.

TICH 03

DANSI HAIJAFA, HAYA YAZINGATIWE

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Ticha Star anasisitiza muziki wa dansi bado una nafasi kubwa lakini unahitaji mfumo mpya wa kuutangaza, uwekezaji na wanamuziki vijana zaidi.

"Japokua muziki huo ndiyo muziki mama katika taifa letu, lakini hadhi yake imeshuka kidogo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo upungufu mkubwa wa wanamuziki wapya kwenye tasnia hiyo, kukosa mbinu sahihi za kujitangaza, kukosa muda wa kutosha kwenye vyombo vya habari na kukosa mapromota wanaoendana na soko la muziki."

Amepongeza juhudi za matamasha kama Asante Tanzania Festival yaliyoandaliwa na Christian Bella pamoja na uwepo wa tuzo za Cheza Kidansi Music Awards ambazo zimeendelea kuupa muziki huo uhai mpya.

Kutokana na mafanikio yake katika muda mfupi, wengi sasa wanaamini Ticha Star ni miongoni mwa sura mpya zinazoweza kuurudisha muziki wa dansi katika hadhi yake ya zamani Tanzania.

“Ninaamini muziki wa dansi utarudi kwenye chati muda si mrefu kutokana na juhudi zinazofanywa sasa,” anasema Ticha Star.


MJIANDAE, ALBAMU INAKUJAA

Kwa sasa msanii huyo yupo katika maandalizi ya album yake ya kwanza inayotarajiwa kutoka mwishoni mwa mwaka 2026 ikiwa na nyimbo sita ikiwemo Kwa sasa Ticha STAR amejikita kwenye kuandaa album yake ya kwanza ambayo inategemewa kuwa na nyimbo 6 ikiwemo 'Ukinipenda remix', 'Sabrina remix', 'Watoto wa Mungu remix', 'Ameniroga', 'Msinishauri' na 'Nimekumiss remix'.