Ecua atulie ustaa Yanga utakuja tu
Muktasari:
- Kurasa za magazeti zilimpamba, vipindi vya redio vikamjadili sana na mitandao ya kijamii picha zake zilisambaa, Yanga imepata mtu kweli wa kuiongezea makali timu yao kule mbele.
MCHEZAJI anayeitwa Celestine Ecua ujio wake ulitengeneza habari kubwa sana katika vyombo vyetu vya habari hapa nchini.
Kurasa za magazeti zilimpamba, vipindi vya redio vikamjadili sana na mitandao ya kijamii picha zake zilisambaa, Yanga imepata mtu kweli wa kuiongezea makali timu yao kule mbele.
Hapa kijiweni tunaamini waliofanya hivyo kwa Ecua hawakukosea kwa vile huko alikotoka alitoka kufanya mabalaa na ndiyo maana alimaliza akiwa mchezaji mwenye thamani zaidi wa msimu uliopita Ivory Coast alikokuwa anaichezea Asec Mimosas.
Ukizingatia wachezaji bora wa msimu huko Ivory Coast waliowahi kuja Tanzania kabla yake, wameonyesha kitu na kuweka alama zao kwenye ligi yetu jambo ambalo halikutufanya tuwe na wasiwasi na Ecua.
Lakini mambo ni tofauti kwa mshambuliaji huyo raia wa Chad kwani anachokifanya uwanjani hivi sasa ni kinyume na matarajio ya wengi na bado hajaonyesha yale makali ambayo wakati anakuja tulitabiri atakuwa nayo.
Anapokuwa uwanjani amekuwa na pupa katika ufanyaji wa maamuzi pindi awapo na mpira. Kuna nyakati pale anapotakiwa kupiga pasi hapigi na anapotakiwa kutopiga ndiyo anapiga na upo muda anaotakiwa kufunga hafanyi hivyo.
Uchoyo wake mara kadhaa umechangia kuinyima Yanga mabao kwa vile kuna muda ambao mwenzake anakuwa yupo katika nafasi sahihi ya kumpa pasi ya mwisho ili afunge lakini hafanyi hivyo na kupiga nje au kufanya anayoyajua.
Inaonekana kama Ecua anakabiliwa na presha ya kutaka kuwaonyesha Yanga yeye ni mchezaji wa daraja la juu na hawakukosea kumsajili jambo ambalo mara nyingi linamfanya ashindwe kuwa na ufanisi unaohitajika.
Anahitajika kubadilika sana vinginevyo anaweza kujikuta hadumu sana katika timu hiyo kwa vile Yanga huwa haina simile kwa mchezaji wa kigeni ambaye inamuona hana mchango mkubwa kwenye timu yao.