Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maji yakimwagika EPL, TPLB isisubiri kuzoa na mwiko

ZENGWE Pict


KUANZIA msimu ujao wa 2026/27 Ligi Kuu England itakuwa na mabadiliko kadhaa yanayolenga kunogesha mashindano hayo ya soka na kudhibiti matumizi ya fedha na ujanja unaofanywa na klabu zilizo chini ya mmiliki mmoja.


Kuanzia uwanjani, kipa atatakiwa akae na mpira chini ya sekunde nane na ikitokea amekaa nao zaidi ya muda huo, timu pinzani itapewa kona. Hii ni katika kudhibiti makipa wasipoteze muda.


Badiliko jingine ni la kuzuia wachezaji kumghasi refa. Kwa mujibu wa kanuni mpya, ni manahodha wa timu tu ndio wataruhusiwa kuongea na mwamuzi iwapo kuna jambo wanaloona halikwenda sawa katika uamuzi.

Iwapo kipa ndo atakuwa nahodha, atalazimika kumtaarifu refa kuwa jukumu la kuongea naye amemkabidhi mchezaji mwingine wa ndani ili kuokoa muda iwapo tukio limetokea mbali na kipa.

ZENG 01

Pia, iwapo mchezaji anayepiga penalti ataugusa mpira mara mbili kabla ya mchezaji mwingine kuugusa,  refa ataamuru penalti irudiwe badala ya kuwa mpira wa adhabu kuelekea goli la mpiga penalti.

Ili kuongeza uwazi katika matumizi ya teknolojia ya refa msaidizi wa video (V.A.R), mwamuzi atalazimika kutangaza uamuzi wake kwa mashabiki kupitia vipaza sauti au spika zilizofungwa uwanjani baada ya kuangalia marudio ya picha za video.

Pia ligi hiyo maaarufu duniani itaanza kutumia teknolojia kinayojiendesha (Semi-Automated Offside Technology, SAOT) ili kupunguza muda unaopotea wakati wa tukio la kuotea.

Nje ya uwanja, kuanzia msimu ujao kanuni mpya za kifedha zitadhibiti klabu kutumia fedha nyingi katika mishahara ya wachezaji, uhamisho wa wachezaji na ada za hadi kufikia asilimia 85 ya mapato ya klabu.

ZENG 02

Pia klabu zimezuiwa kuuza mali zisizohusu mpira wa miguu (kama vile hoteli au timu za wanawake) kwa timu zilizo na uhusiano ili kuziongezea uwezo wa kuendana na kanuni za fedha.

Kuhusu matangazo ya televisheni, kuanzia msimu huu Sky Sport inarusha moja kwa moja mechi 215 kwa msimu mmoja, wakati wapigapicha za televisheni wataruhusiwa kuingia vyumba vya kubadilishia nguo na waandishi wa kampuni iliyopewa haki za matangazo wataruhusiwa kufanya mahojiano na wachezaji ambao watakuwa wakitoka uwanjani baada ya kufanyiwa mabadiliko.

Mabadiliko hayo yameshatangazwa hata kabla ya msimu kuisha na  hivyo klabu na wachezaji wanajiandaa kwa ajili ya mabadiliko na kupewa mbinu za kukabiliana nayo kuepuka kuathiri timu.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakizungumzwa kwa muda mrefu na kuchunguzwa sababu za kutokea kwake na athari kabla ya kukaribisha mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni na kuangaliwa ni yapi yanaweza kusaidia kuboresha uendeshaji.

ZENG 03

Mfano mwaka juzi Chelsea ilijiuzia hoteli mbili ili kutokiuka Kanuni ya Faida na Uendelevu (Profit and Sustainability Rule, PSR). Mwezi wa saba mwaka jana, Everton iliiuzia kampuni yake tanzu timu ya wanawake, hali kadhalika Aston Villa.

Kwa hiyo, si suala la waendeshaji wa Ligi Kuu kusubiri hadi mwishoni mwa msimu ndio ianze kukaribisha mapendekezo ya kanuni mpya ili kuboresha uendeshaji wa mashindano hayo makubwa nchini kama ambavyo Bodi ya Ligi (TPLB) inafanya hivi sasa.

Mabadiliko hayo ya kanuni yalishajadiliwa kwa kina na yakapitishwa katika mkutano mkuu wa klabu za Ligi Kuu, ambazo ndio wanahisa wa kampuni inayoendesha ligi hiyo, kabla ya kuanza kwa msimu huu.

Ni muhimu sana TPLB iwe na kitengo kinachofuatilia kasoro na ubora wa kanuni na kukaribisha mijadala ya wazi kabla ya kitengo hicho kuandaa mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni na kuyapeleka katika mkutano husika kwa ajili ya kupitishwa.

ZENG 04

Na ni lazima mabadiliko hayo yawe yameshajulikana na kupitishwa angalau msimu mmoja kabla ya kuanza kutumika ili kuzipa nafasi klabu kujiandaa.

Haya mazoea ya kutangaza kupokea mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni kabla ya kuanza kwa msimu ndio yanayofanya kuwe na mabadiliko mabovu yanayotumiwa vibaya na Kamati ya Masaa 72.

Ni lazima mabadiliko yanayopendekezwa yawe hadharani mapema ili wadau wa soka wayajadili kwa kina faida na hasara zake kabla ya kuwasilishwa kwenye mkutano wenye mamlaka ya kuyapitisha.

Na ni muhimu kwa mchakato wa kupata maoni au mapendekezo ya kanuni mpya uongozwe au ushikwe na Bodi ya Ligi kwa kuweka hadharani maeneo yanayokusudiwa kubadilishwa na si kama chombo hicho kinavyofanya kwa kuomba kila mtu apeleke mapendekezo yake.

Huko si kuongoza mchakato bali ni kujipa kazi isiyo muhimu ya kuchambua mapendekezo mengi yanayoweza kuwasilishwa iwapo mwamko kwa wadau utakuwa mkubwa.

Pia iwapo mwamko utakuwa mdogo, mwaliko huo wa mapendekezo unaweza kutumiwa kama kichaka cha kutumbukiza mabadiliko ya hovyo kwa kisingizio kuwa wadau hawakujitokeza au walioitikia wito ndio hao waliopendekeza hayo.

Tunahitaji mbinu za kisayansi kufanya mabadiliko ya kanuni na si hizi za kisiasa.