Prime
Okello ametua Yanga na madeni kibao Jangwani
UDADISI ukafanya nifuatilie vizuri ukurasa wa staa mpya wa Yanga, Allan Okello. Anajulikana kwa jina la ‘Star boy’. Sijui kwa kijana wa kawaida mwanamume aliyekomaa huwa inaishia mwaka gani. Nilipoenda katika ukurasa wa Wikipedia nikagundua Okello ana miaka 25.
Labda jina la Star Boy lilimganda akiwa kwao Uganda angali akiwa anachomoza. Kwa uchunguzi wa haraka haraka nadhani jina lenyewe limemganda kwa sababu ana sura ya kitoto. Inanikumbusha sura ya staa wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Norway, Ole Gunnar Solskajer. Umri mkubwa lakini sura ya mtoto wa shule ya msingi.
Kwa sasa Star boy siyo jina linalomfaa sana kama Yanga wanavyotaka kulitumia kwa sababu ana miaka 25 na Julai mwaka huu atatimiza miaka 26. Kwa wachezaji mpira huu ni umri wa kutimiza majukumu uwanjani bila ya kutumia kisingizio cha umri mdogo. Miaka 17 hadi 20 ndiyo unaweza kutumia kisingizio cha umri mdogo katika mchezo wa mpira wa miguu.
Miaka 25 ni ya mchezaji kuwa tayari amepevuka na yuko tayari kubeba majukumu makubwa ndani ya timu na ikiwezekana kuongoza wachezaji wengine ndani na nje ya uwanja. Okello ana mambo mengi ya kufanya Yanga. Kifupi ana madeni mengi ambayo anapaswa kuyalipa moja kwa moja katika kikosi cha sasa cha Yanga.
Deni la kwanza kabisa ni kuthibitisha bado soko la wachezaji wa Afrika Mashariki kwa klabu kubwa za Tanzania ni mali. Siku hizi wakubwa wetu wanakimbilia zaidi Afrika Magharibi, Congo na kuna watu wameanza kugusa soko la Afrika Kusini. Wakubwa wetu wamekimbia kusajili wachezaji kutoka Uganda na Kenya.
Mchezaji wa mwisho ambaye Yanga walimchukua moja kwa moja kutoka Uganda alikuwa ni Gift Fred ambaye alishindwa kupata nafasi mbele ya Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamunyeto. Baadae akajiondokea zake kurudi nyumbani. Sikumwona kama mchezaji mbaya lakini ushindani ulikuwa mkubwa kwake.
Ukimzungumzia Khalid Aucho ni kweli ni mchezaji kutoka Uganda, lakini Yanga hawakumchukulia Uganda. Walimchukulia nje ya Uganda wakati alipoachana na timu moja ya Misri.
Soko la Uganda limekuwa likidharauliwa katika siku za karibuni baada ya kutawala mpira wetu kupitia kwa kina Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza ‘Diego’, Joseph Owino na wengineo wengi.
Okello ana deni kutoka kwa Waganda wenzake na ana deni kutoka kwetu. Deni la kuthibitisha mchezaji anaweza kuwa staa Uganda na akatamba katika mpira wetu kama ilivyokuwa zamani. Inabidi aifanye kazi hiyo kiume kuwakilisha ligi ya Uganda hapa kwetu. Namba zake zinavutia na tunataka kuona kama anaweza kuzihamishia hapa.
Okello pia ana deni jingine kwa mtu aliyemsajili. Tulimwona Injinia Hersi Said akipanda ndege na kwenda kumsajili Okello kwa mbwembwe nyingi.
Wachezaji ambao wamesajiliwa katika dirisha kubwa lililopita wengi hawajafikia matarajio ya Wanayanga kwa sababu mbalimbali. Okello ana jukumu la kuthibitisha Hersi hakosei mara nyingi baada ya kusifiwa kuitengeneza Yanga imara.
Kina Mamadou Doumbia, Moussa Balla Conte, Lassana Kouma, Andy Boyeli na wengineo hawajaonyesha maajabu makubwa tangu wasajiliwe Yanga.
Hii ndiyo sababu ya Yanga kwenda tena sokoni katika dirisha hili dogo na kumchukua Okello pamoja na staa wa Angola anayefahamika kwa jina la Depu. Kama niliowataja wangekuwa wametisha sidhani kama Hersi na washkaji zake wangetafuta wachezaji wapya katika nafasi zao.
Kinachowabeba Yanga ni ukweli wamekuwa na mafanikio katika mpira wetu. Lakini huwa wana timu yao ya msingi ambayo ipo tayari kuendelea kufanya vizuri kama wageni wakishindwa.
Kina Pacome Zouzoua, Maxi Nzingeli, Prince Dube, Clement Mzize, Duke Abuya, Mudathir Yahya na wengineo wapo tayari kuendeleza ubora wa Yanga kama wageni wakishindwa. Ni kama tulivyoona katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 kule Unguja na Pemba.
Baada ya mbwembwe nyingi za kusajiliwa kwake Okello ana deni la kuhakikisha haingii katika kundi la kina Doumbia. Inapaswa aonekane ni mchezaji aliyekuja kuleta kitu kipya katika kikosi cha Yanga hasa katika michuano hii ya kimataifa ambayo imerudi tena. Hakuna ambaye atamsamehe kwa kusema ni kijana mdogo kama ambavyo sura yake inadanganya. Ni mtu mzima.
Deni jingine ambalo Okello analo ni namna usajili wake umekwenda. Kwa muda mrefu alikuwa anahusishwa na watani wa Yanga, yaani Simba. Imeonekana kama kulikuwa na umafia wa uhamisho wake kwa Injinia Hersi kuupora uhamisho wa mchezaji ambaye alionekana anaelekea kwa watani wao.
Inasemwa mabosi wa Simba walikuwa wanamtaka Okello tangu dirisha kubwa lililopita lakini aliyezuia ni Kocha Fadlu Davis ambaye alimpendelea zaidi kiungo wa Afrika Kusini, Neo Maema.
Mabosi wa Simba hawakuwa na jinsi. Lakini majuzi Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amekiri wao pia walimtaka Okello lakini wakachoshwa na dau lake.
Okello akifanya vizuri Yanga itawaumiza Simba. Akifanya vibaya Yanga itawafurahisha Wanasimba kwa sababu itaonekana Yanga wana tabia ya kuparamia mambo yao bila ya kuwa makini.
Ilitokea kwa Balla Conte wakati akionekana garasa Jangwani. Walau watu wa Yanga wameshusha pumzi baada ya staa huyo kung’ara katika michuano ya kombe la mapinduzi. Walikuwa wanasemwa vibaua na watani zao.
Deni jingine ambalo Okello analo ni kuhakikisha Yanga wanafanya poa katika michuano ya kimataifa. Huku ndani Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu au FA haliwezi kuwa jambo jipya. Yanga wanahitaji waende mbali katika michuano ya kimataifa.
Sijui kama Okello atacheza katika mechi mbili za kundi la Yanga michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na Yanga atacheza na Al Ahly ugenini na nyumbani. Hizi ndio mechi ambazo zimemleta Okello nchini na sio vinginevyo.
Na labda tu nimkumbushe Okello alikosa penalti muhimu katika pambano la Uganda dhidi ya Tanzania pale Morocco katika michuano ya Afcon. Kwa Waganda sijui wamemchukuliaje lakini kwa ushindani mkubwa uliopo katika mpira wetu inakuwa ngumu kwa mashabiki kumsamehe kirahisi. Mpira wetu una ushabiki mwingi mitaani na mitandaoni.
Kifupi ajiandae kukabiliana na presha kubwa ya mashabiki wa pande zote mbili. Mashabiki wake mwenyewe na mashabiki wa mtani. Majirani waliotuzunguka huwa hawana ushabiki mkubwa wa mpira katika kiwango cha Simba na Yanga.
Nadhani kina Aucho na Okwi watakuwa wamemwambia kinachoendelea katika mpira wa Tanzania. Hakina mfano wake. Labda unaweza kutufananisha na mashabiki Misri, Tunisia, Morocco na Algeria. Basi.
Tuna unazi uliopitiliza unaoweza kumweka mchezaji katika presha kubwa. Ukifanikiwa kama walivyofanikiwa kina Pacome ndipo unaweza kuishi kama mfalme.
Vinginevyo jiandae kukabiliana na presha kubwa kutoka kwa mabosi wako, mashabiki na wachambuzi. Ndivyo mpira wetu ulivyo na hiki ndicho kinachomsubiri Okello.